loader
Picha

Mahakama yaonya washitakiwa Chadema

MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam imewaonya washitakiwa saba wanaodaiwa kuwa wafuasi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kwamba wasipofika mahakamani tarehe itakayopangwa, watakamatwa na kufutiwa dhamana.

Washitakiwa hao kati ya 31 wanakabiliwa na kesi ya kufanya mkusanyiko usio halali kinyume na sheria na kwamba hawakufika mahakamani hapo jana kesi yao ilipoitwa.

Wakili wa Serikali, Ester Martin alidai jana mbele ya Hakimu Mkazi Karim Mushi kuwa, kesi hiyo imekuja kwa ajili ya kutajwa lakini washitakiwa saba kati ya 31 wanaokabiliwa na kesi hiyo, hawajafika mahakamani.

Wakili Martin alidai kuwa upande wa mashitaka hauna taarifa yoyote ya kutohudhuria mahakamani kwa washitakiwa hao hivyo wanaomba mahakama iwape hati ya kuwakamata.

Aliwataja washitakiwa hao ni Edna Kimaro, Jonathan Lema, Ramadhan Mombo, Ezekiel Nyenyembe, Raphael Mwaipopo, Athuman Mkawa na Jackson Masilingi.

Wakili wa utetezi, Alex Massaba alidai kuwa huenda wateja wake wapo nje wanasubiri kuitwa kwa sababu hawajui kama kesi hiyo imehamishiwa kwa hakimu mwingine kutoka kwa Hakimu Mkazi, Godfrey Mwambapa kwenda kwa Hakimu Mushi.

Hata hivyo, aliuomba upande wa mashitaka katika kesi hiyo kukamilisha upelelezi kwani imekuwa ikitajwa kila mara inapopangwa.

Kutokana na hoja hizo, Hakimu Mushi alisema kwa kuzingatia maombi ya wakili wa utetezi, mahakama hiyo haitatoa hati ya kuwakamata washitakiwa hao, ila kama hawatafika mahakamani tarehe itakayopangwa, bila kutoa taarifa mahakama hiyo itawakamata na kuwafutia dhamana.

Aliahirisha kesi hiyo hadi Julai 12, mwaka huu kwa ajili ya kutajwa na kwamba washitakiwa wote wako nje kwa dhamana.

Washitakiwa wote kwa pamoja wanadaiwa kuwa Februari 16, mwaka huu maeneo ya Kinondoni katika eneo la Mkwajuni, Wilaya ya Kinondoni walifanya mkusanyiko usio wa halali na kinyume cha sheria.

Ilidaiwa kuwa mkusanyiko huo ulikuwa na nia ya kufanya uvunjifu wa amani na kusababisha taharuki kwa wananchi.

WAZIRI wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Kangi Lugola ameagiza ...

foto
Mwandishi: Francisca Emmanuel

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi