loader
Picha

Lechantre awapa tuzo wachezaji

KOCHA Mkuu Simba SC, Pierre Lechantre juzi aliwaaga wachezaji wake na kuwapa tuzo yake ya benchi la ufundi aliyopata katika tuzo za Mo Simba.

Katika hafla hiyo iliyofanyika Dar es Salaam, Lechantre alikuwa miongoni mwa waliohudhuria na kupewa tuzo ya benchi la ufundi bora iliyokwenda kwa benchi zima la Simba.

Akiwa jukwaani baada ya kupokea tuzo yake, kocha huyo Mfaransa alishukuru kwa tuzo hiyo na kuwatakia Simba kila la heri msimu ujao.

“Anasema anashukuru sana kwa tuzo na anawatakia kila la heri msimu ujao,” alitafsiri kocha msaidizi Masoud Djouma Kifaransa kilichozungumzwa na Lechantre.

Mwishoni mwa tuzo hizo, gazeti hili lilimshuhudia kocha Lechantre akienda walipokaa wachezaji ambapo alimpa tuzo kipa wa timu hiyo, Aishi Manula.

“Hii ni kwa ajili yenu,” alisikika Lechantre akimwambia Manula huku akimkabidhi tuzo hiyo.

Lechantre alikuwa na mkataba wa miezi sita Simba unaotarajiwa kumalizika Juni 18 na kumekuwa na tetesi nyingi juu ya kuondoka kwake, ingawa uongozi wa klabu hiyo haujaweka wazi bado suala hilo.

Katika tuzo hizo za Simba kwa msimu wa mwaka 2017/18, nahodha John Bocco alipata tuzo mbili, ya mchezaji bora na ya bao bora, Manula alipata tuzo ya kipa bora, Erasto Nyoni alichukua tuzo ya beki bora wakati tuzo ya kiungo bora ilikwenda kwa Shiza Kichuya.

Mshambuliaji wa Uganda, Emmanuel Okwi alipata tuzo ya mshambuliaji bora. Okwi pia ndiye kinara wa mabao kwenye Ligi Kuu Bara msimu uliopita akiwa amepachika mabao 20.

Kwa upande wa mchezaji bora wa kike, tuzo ilikwenda kwa mchezaji wa Simba Queens, Zainabu Pazzi huku tuzo ya mchezaji bora chipukizi ikienda kwa Rashid Juma.

Tuzo ya shabiki bora ilikwenda kwa Fii Kambi ambaye alifikwa na umauti mapema mwaka huu.

Fii alikuwa hakosekani kwenye mechi mbalimbali za Simba iwe zinachezwa Dar es Salaam ama mikoani, tuzo yake ilipokewa na mtoto wake.

Msanii Hamisi Mwinjuma ‘mwana FA’ na Salama Jabir walipata tuzo ya mhamasishaji bora mitandaoni huku tuzo ya mhamasishaji bora wa jumla ikienda kwa msemaji wa klabu hiyo, Haji Manara.

Kocha wa Lipuli ambaye aliwahi kuwa mchezaji wa timu hiyo, Suleiman Matola alipata tuzo ya heshima na tuzo ya tawi bora ilikwenda kwa Ubungu Terminal.

Kaimu Rais wa klabu hiyo Salim Abdallah ‘Tray Again’ alipata tuzo ya kiongozi bora na tuzo ya mchakato wa mabadiliko ilikwenda kwa kamati nzima.

MSHAMBULIAJI wa Yanga, Heritier Makambo (pichani) amesema wamesafi ri umbali ...

foto
Mwandishi: Mwandishi Wetu

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi