loader
Picha

Mabeyo: Msiozeshe watoto, waacheni wasome

MKUU wa Majeshi ya Ulinzi nchini, Jenerali Venance Mabeyo ametoa mwito kwa wazazi kuwekeza katika elimu kwa watoto wao ili waweze kutimiza ndoto za maisha yao, badala ya kuwaoza wakiwa na umri mdogo.

Jenerali Mabeyo ametoa mwito huo wakati wa harambee ya kuchangia ujenzi wa Kanisa Katoliki Parokia ya Ilumya iliyofanyika Kijiji cha Masanza Kona kata ya Kiloleli wilayani Busega na kuhudhuriwa na Kamati ya Ulinzi na Usalama.

Kamati hiyo iliongozwa na Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Anthony Mtaka, mwakilishi wa Mkuu wa Mkoa wa Mara, Dk Vicent Naano, marafiki wa mkuu wa majeshi kutoka Dar es Salaam, Wajenzi Enterprises ,wafanyabiashara wa Simiyu na waumini wa kanisa hilo.

Mkuu wa majeshi ya ulinzi huyo pamoja na kuongoza harambee ya kuchangia ujenzi wa kanisa hilo, alisema wazazi wanapaswa kutoa kipaumbele cha elimu kwa watoto, badala ya kuwakatisha masomo hususan wa kike ili waolewe.

"Sasa hivi mmewekewa shule ya sekondari hapa na mimi nimeshiriki kujenga shule hii, sasa wazee wangu mlioko hapa changamkieni elimu, watoto muwapeleke shule, waacheni wasome, elimu ndiyo ufunguo wa maisha, wasiposoma hata mkiomba nafasi za kuingia jeshini hakuna nafasi," alisema.

Wakizungumza kwa niaba ya waumini wa Parokia ya Ilumya, Makamu wa Askofu wa Jimbo Katoliki la Shinyanga na Padri, Kizito Victor na Paroko wa Parokia ya Masanza, Padri Michael Gumalija wamemshukuru Mkuu wa Majeshi na viongozi na wadau wengine wote waliochangia na kuahidi kushirikiana na wafadhili wote kuhakikisha kanisa linajengwa.

Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Anthony Mtaka alisema kipaumbele cha kwanza cha mkoa huo ni elimu, hivyo Mkuu wa Majeshi amesaidia kufikisha ujumbe wa kuhamasisha elimu kwa wazazi, jambo ambalo limekuwa sehemu ya kampeni ya mkoa ya kupinga mimba za utotoni ambazo zinaua ndoto za watoto wa kike.

Katika harambee hiyo, jumla ya fedha zilizopatikana ahadi na taslimu ni Sh milioni 273.1, kati ya hizo fedha taslimu ni Sh milioni 111.9.

Aidha fedha zinazohitajika katika ujenzi huo ni Sh milioni 782 kwa ajili ya kukamilisha kujenga jengo lenye uwezo wa kuchukua waumini zaidi ya 1,200 kwa mara moja.

MKUTANO wa 38 wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa ...

foto
Mwandishi: Shushu Joel, Busega

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi