loader
Picha

Moi kupasua ubongo kwa ‘ultra sound’

TAASISI ya Tiba ya Mifupa Muhimbili (MOI), inaweza kufanya upasuaji mgumu kupitia mbinu mpya za upasuaji wa ubongo kwa kutumia kipimo cha ultra sound baada ya kupata mafunzo kutoka kwa wakufunzi waliotoka nchini Marekani.

Mkurugenzi Mtendaji wa MOI, Dk Respicious Boniface alisema hayo jana alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari kuhusu ujio huo wa wakufunzi kutoka Chuo Kikuu cha Colorado Denver nchini Marekani.

Dk Boniface alisema, wakufunzi hao watakuwepo nchini kwa wiki mbili ambapo watakuwa wakifundisha madaktari jinsi ya kuongeza ujuzi na uwezo wa kuwawezesha kufanya upasuaji mgumu kwa teknolojia hiyo ambayo walikuwa hawajawahi kuitumia.

"Madaktari wetu wamefundishwa mbinu mpya za upasuaji ubongo tangu jana (juzi), mpaka leo (jana), wameshawafanyia upasuaji wagonjwa watatu," alisema.

Daktari Bingwa wa upasuaji ubongo, uti wa mgongo na mishipa ya fahamu MOI, Dk Nicephorus Rutabasibwa alisema, wakufunzi hao waliofika kutokea nchini Marekani, wapo kwa ajili ya kutoa mafunzo na kuwapa mbinu mpya za uchunguzi, matibabu na upasuaji madaktari, wataalamu wa radiolojia pamoja na watumishi wengine.

"Mafunzo yanayotolewa yanahusu matumizi ya kipimo cha 'ultra sound' wakati wa upasuaji wa ubongo na mgongo. Pia matumizi ya darubini maalumu na ya kisasa inayotumika kwenye upasuaji wa kibingwa wa matundu wa mgongo, mishipa ya fahamu na ubongo," alisema Dk Rutabasibwa.

Aliongeza kuwa, kwa kushirikiana na wataalamu wazawa kutakuwa na mashauriano ya kuhuisha mtaala wa mafunzo ya kibingwa ya ubobezi wa upasuaji wa ubongo, mgongo na mishipa ya fahamu yatolewayo MOI kwa ushirikiano na Chuo Kikuu cha Afya cha Muhimbili (MUHAS).

Alisema lengo la kuhuisha mtaala huo ni kuifanya MOI kuwa kituo cha mafunzo cha hali ya juu Afrika kusini mwa Jangwa la Sahara.

Alisema jopo hilo la wakufunzi kutoka Marekani linaongozwa na Profesa Ryan David ambaye ni daktari bingwa wa upasuaji wa ubongo, mgongo na mishipa ya fahamu na Mkuu wa Mafunzo ya kibingwa kutoka chuo hicho.

Alisisitiza kuwa, mafunzo hayo yatakwenda sambamba na upasuaji kwa wagonjwa wa ubongo, mgongo na mishipa ya fahamu ikiwa ni sehemu ya mafunzo kwa vitendo.

Kwa mujibu wa wataalamu hao wa MOI, tatizo la magonjwa hayo ni kubwa, na kwa mwaka wanafanyia upasuaji zaidi ya wagonjwa 60.

Ujio wa madaktari hao utasaidia kupunguza gharama ya kwenda nje ya nchi kwa kiasi kikubwa, kwani mgonjwa mmoja aliyekwenda nje ya nchi alitumia Sh milioni 50 lakini kwa kutibiwa hapa chini gharama haizidi Sh milioni tatu.

WAZIRI wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Kangi Lugola ameagiza ...

foto
Mwandishi: Lucy Ngowi

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi