loader
Picha

Bajeti SMZ kutotegemea wafadhili

SERIKALI ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ), imeacha kutegemea wafadhili katika bajeti yake ya fedha tangu mwaka 2016 na kujikita katika ukusanyaji wa mapato ya ndani, kuziba mianya yote iliyokuwa ikivujisha mapato.

Uamuzi huo umeleta mafanikio makubwa ikiwemo kutekeleza miradi yake yote ya maendeleo, kulipa viinua mgongo vya wafanyakazi wastaafu wa serikali wapatao 1,057 na kutumia jumla ya Sh bilioni 17.7 katika kipindi cha miaka mitatu sasa.

Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Khalid Salum Mohamed ameyasema hayo wakati anawasilisha Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa mwaka wa fedha 2018/19 kwa Wizara ya Fedha na Mipango.

Alisema katika mipango hiyo, serikali inakusudia kutekeleza vipaumbele vinane, programu saba na kukusanya mapato ya Sh trilioni 1.28 katika mwaka wa fedha 2018/2019.

Alivitaja baadhi ya vipaumbele hivyo ni kuimarisha usimamizi wa ukusanyaji wa mapato ya ndani, kuandaa dira mpya ya maendeleo ya taifa, kufanya sensa ya kilimo na utafiti wa mapato na matumizi ya kaya.

Aidha alizitaja programu zitakazosimamiwa kwa mwaka ujao ni usimamizi wa bajeti na fedha za umma ambayo inatarajiwa kutumia Sh bilioni 57.86 pamoja na programu ya usimamizi na uwekwaji wa mali za umma ambayo imekadiriwa kutumia Sh bilioni 19.92.

Alisema katika utekelezaji wa bajeti ya mwaka wa Fedha 2018/2019, suala la usimamizi mzuri wa mapato ya nchi limepewa kipaumbele na umuhimu mkubwa kupitia vyanzo vya mapato.

Alisema wafanyakazi wa Bodi ya Mapato Zanzibar (ZRB) watawezeshwa kwa ajili ya kuhakikisha mapato yanaongezeka katika vyanzo vipya.

Alisema ZRB imepangiwa kukusanya jumla ya Sh bilioni 485.33, wakati Mamlaka ya Vitega Uchumi (ZIPA) imepangiwa kukusanya jumla ya Sh bilioni 3.75, huku Mfuko wa barabara nchini ukikusanya Sh bilioni 15.63.

Aidha taasisi nyingine za serikali zinazotarajiwa kuongeza pato la taifa ni Mfuko wa Hifadhi ya Jamii (ZSSF) ambao umepangiwa kukusanya Sh bilioni 116.95, huku Shirika la Bima likikusanya Sh bilioni 28.5, Benki ya Watu wa Zanzibar (PBZ) ikikusanya Sh bilioni 70.5.

Alisema katika mwaka wa fedha 2018/19 wana matarajio makubwa ya kuongezeka kwa mapato kutokana na kukamilika kwa mradi wa jengo la abiria katika uwanja wa ndege wa Abeid Amani Karume ambapo ujenzi wake unaendelea.

Alifahamisha mradi huo utasaidia kuongeza idadi ya watalii na wageni wanaoingia nchini kufikia milioni tatu.

Mapema Dk Mohamed alisema ZIPA inaendelea na mikakati yake kuitangaza Zanzibar kama ni moja ya eneo zuri la uhakika la uwekezaji katika Afrika ya Mashariki.

Alisema ZIPA kuanzia mwaka 2016/2017 imefanikiwa kupokea maombi ya miradi ya uwekezaji iliyofikia 56, huku miradi iliyopita ni 38.

Alifahamisha kwamba Zanzibar imeendelea kuwa moja ya kivutio cha uwekezaji kutokana na kuimarika kwa amani na utulivu wa kisiasa katika kipindi chote.

WAZIRI wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Kangi Lugola ameagiza ...

foto
Mwandishi: Khatib Suleiman, Zanzibar

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi