loader
Picha

Watanzania kuzindua Boeing ya ATCL kwa bei poa

KAMPUNI ya Ndege Tanzania (ATCL) imetangaza nauli za ndege mpya Boeing 787-8 Dreamliner kwa safari kati ya mikoa ya Dar es Salaam, Mwanza na Kilimanjaro kwa mwezi Agosti tu mwaka huu.

Ndege hiyo mpya ni miongoni mwa ndege saba zilizonunuliwa na serikali. Kwa mujibu tangazo la kampuni hiyo jana, abiria wanaosafiri kati ya Da es Salaam na Mwanza watalipa Sh 113,000 kwa safari ya kwenda tu pamoja na kodi. Abiria watakaosafiri kwa ndege hiyo kwenda na kurudi kati ya mikoa ya Mwanza na Dar es Salaam watalipa Sh 206,000 pamoja na kodi. Abiria wanaosafiri kati ya Kilimanjaro na Mwanza watalipa Sh 93,000 kwa kwenda tu pamoja na kodi.

Abiria wanaosafiri kati ya mikoa hiyo kwenda na kurudi watalipa Sh 166,000 pamoja na kodi. Abiria wanaosafiri kati ya Kilimanjaro na Dar es Salaam kwa kwenda tu watalipa Sh 98,000 pamoja na kodi. Abiria wanaosafiri kati ya mikoa hiyo kwenda na kurudi watalipa Sh 176,000 pamoja na kodi. “Wale wasafiri wa kutoka Dar - Kilimanjaro, Dar - Mwanza na Kilimanjaro - Dar, wakati ni huu kuonja asali ya anga kwa bei sawa na bure. Fanya booking yako mapema kuwahi nafasi.

Safiri nasi kwa kutumia Dreamliner kwa Agosti pekee,” imesema ATCL kwenye tangazo hilo lililotolewa kwenye akaunti ya kampuni hiyo katika mtandao wa kijamii wa twitter. ATCL imebainisha kuwa ndege yake mpya yenye uwezo wa kubeba abiria 262, itawasili mwezi huu. Ndege hiyo itafanya safari nchini kwa mwezi mmoja kabla ya kuanza safari za kwenda Mumbai, India.

Juzi Rais John Magufuli alisema, anataka ndege zinazosimamiwa na ATCL zianze kufanya kazi vizuri. Kwa mujibu wa Rais Magufuli, Serikali imenunua ndege saba, tatu zimeshakuja, tatu nyingine zimekaribia kuja zikiwemo mbili zenye uwezo wa kubeba watu 150 na nyingine ya watu 262. Mei tano mwaka huu, ATCL kupitia akaunti yake ya twitter ilitoa tangazo lililosema ‘muda si mrefu unaweza kusafiri moja kwa moja mpaka Mumbai kutoka Dar es Salaam na ndege yetu ya Air Tanzania Boeing 787 Dreamliner’.

Kwa mujibu wa Mkuu wa Idara ya Biashara, Lily Fungamtama ndege hiyo ina uwezo wa kwenda safari ya moja kwa moja kwa saa 18. Fungamtama amesema, kabla ya mwisho wa mwaka huu, wanatarajia kupokea ndege nyingine mbili hivyo kuongezeka kwa safari za masafa ya mbali. Amesema, kwa sasa shirika hilo linafanya safari ndani ya nchi katika mikoa ya Kilimanjaro, Mwanza, Mbeya, Tabora, Kigoma, Bukoba na visiwa vya Zanzibar huku wakifanya safari za Songea lakini kwa sasa wamesitisha kwa ajili ya kiwanja kinafanyiwa marekebisho.

MKUU wa Mkoa wa Iringa Ally Hapi amekataa ombi la ...

foto
Mwandishi: Basil Msongo

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi