loader
Picha

Nchi za EAC zatia fora maonesho ya biashara Dar

NCHI za Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) zimekuwa na mwitikio mzuri katika Maonesho ya 42 ya Kimataifa Dar es Salaam (DITF) yanayoendelea Dar es Salaam, kwani zimeshiriki kwa mafanikio, huku bidhaa zake zikionekana kukubalika kwa wananchi.

Wananchi hao, wakiwemo wa ndani na nje ya jumuiya, wamejitokeza kwa wingi kuangalia bidhaa, kutafuta fursa za masoko kwa washiriki wengine na pia kujifunza teknolojia mbalimbali.

Ukiondoa Sudan Kusini, nchi nyingine zote ndani ya EAC, wenyeji Tanzania, Kenya, Uganda, Rwanda na Burundi, zimeshiriki na kwa pamoja, nchi hizo zipo katika banda la PTA lenye kushirikisha nchi mbalimbali.

Katika mabanda ya nchi za EAC, mbali ya ukarimu wao, hutambulika kirahisi kwa bendera zao, lakini wamekuwa wepesi kuzungumza kwa lugha ya Kiswahili jambo linalodhihirisha umoja kati ya nchi hizo na matumizi ya lugha na kukiwa na wachache sana wasiojua lugha hiyo.

Katika mabanda ya nchi za EAC mbali na kuleta bidhaa mbalimbali za kilimo zilizoongezwa thamani, kila nchi imefika na bidhaa maarufu katika nchi yake kwa lengo la kupata wateja pamoja na mawakala wa kusambaza huduma.

Mmoja wa viongozi kutoka Baraza la Maendeleo ya Biashara nchini Kenya, Peterson Nyachwaya alisema wamefika katika maonesho hayo wakiwa na kampuni 16 kwa lengo la kukuza biashara za nchi yao kwa kutafuta masoko kutoka nje ya nchi.

Alisema kwa kutumia maonesho hayo, wamefanikiwa kutoa ajira kwa watu 15 huku wakiwa na bidhaa za chai kutoka kampuni tatu tofauti, mafuta, viatu na bidhaa nyingine mbalimbali nyumbani, maziwa, nguo za aina mbalimbali, vikoi na kampuni nne zimeleta vinyago, juisi na nyinginezo.

“Kwetu bidhaa zinazonunuliwa sana ni chai, viatu vya Kimasai, nguo za kiafrika,” alisema na kuongeza kuwa, wameleta huduma za kibiashara ikiwemo ukarimu katika hoteli, viwanda vya aina mbalimbali pamoja na huduma katika kuwezesha ufanyaji biashara huku akijivunia kushiriki maonesho hayo zaidi ya 30 wakiwa na kampuni zaidi ya 15 .

Alitaja bidhaa za Tanzania ambazo wananchi wa Kenya wamekuwa wakizipenda kuwa ni asali, vitenge, suti, bidhaa za urembo na kadhalika.

Aliitaka Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (TANTRADE) inayoandaa maonesho hayo, kuondoa changamoto mbalimbali wanazopata kila mwaka mipakani ni kuwapatia barua mapema inayowatambulisha kuepuka kupekuliwa wakiwa njiani, hivyo kuepuka usumbufu na kutaka maonesho hayo kufunguliwa mapema saa mbili asubuhi kama yalivyo mengine ya nchi za EAC, jambo linalosaidia watu kufika mapema na kuendelea na shughuli nyingine.

Alisema mbali ya changamoto hizo, maonesho hayo ni muhimu kwa nchi za EAC kufika nchini kukutana na watu wa aina mbalimbali, hivyo kusaidia muingiliano kufahamu kwa undani tamaduni mbalimbali.

“Pia waandaaji hawa wanatakiwa kujitahidi kuwa na mawakala wa benki za kimataifa humu ndani, kwani inalazimu watu kutoka na kutafuta benki zinazotoa huduma katika nchi zetu, kama sisi hakuna benki ya Kenya humu inabidi kuifuata mjini na kukabiliwa na foleni kubwa,” alisema.

Kiongozi wa msafara kutoka nchini Burundi alieleza kuwa wamefika katika maonesho hayo wakiwa na watu 18, waliojipanga katika mabanda sita.

Kiongozi huyo, Mashimango Wenceslaus alisema wamefika katika maonesho hayo wakiwa na bidhaa mbalimbali ikiwemo vinyago, nguo, vikapu, viti, bidhaa nyingine hasa ambazo zinapatikana kwa wingi Burundi tofauti na nchi nyingine za EAC.

Alisema si mara yake ya kwanza, kushiriki maonesho ya nchini, lakini mara nyingi amekuwa akishiriki yale ya JUAKALI lakini hayo yana watu wengi hivyo wataendelea kushiriki na kualika wengine zaidi kutoka nchini humo.

Alisema uzuri wa maonesho hayo, yanasaidia kuimarisha uhusiano na wengine kubadilishana uzoefu kwa kujifunza katika nchi nyingine zilizoendelea hata ndani ya EAC.

Aliongeza kuwa, kuna bidhaa nyingi zinazotoka nchini kupelekwa nchini mwao ikiwemo vyakula lakini vinyago vinavyotengenezwa kwa mbao nyeusi hupendwa sana na kununuliwa kwa wingi.

“Licha ya kuwa na maonesho haya kwa kila nchi ni vema kuimarisha yale ya nchi za EAC na kuwa katika kila sekta itasaidia kuungana na kuwa wamoja huku nchi ndogo kama yetu ikijifunza na kuinuka kiteknolojia, na hatimaye kuwa na soko la pamoja kupeleka bidhaa nje ya nchi,” alisema.

Alisema watanzania wamezipenda sana bidhaa zao huku kukiwa na watu kutoka nchi mbalimbali, hivyo kudhihirisha kweli ni ya kimataifa. Mmoja wa viongozi wa msafara kutoka Rwanda, Hamisi Buchumi alisema kampuni 12 kutoka nchini humo, wamefika kwenye maonesho hayo wakileta bidhaa za vinyago, michoro ya picha, bidhaa zinazotengenezwa kwa mazao, pilipili, vinywaji vikali vya ndizi na matunda mengine, maziwa, biskuti na nyinginezo.

Alisema pilipili kutoka nchini humo pamoja na nyinginezo, zimekuwa zikinunuliwa kutokana na kuwa na harufu zake za asili bila kuwekwa ladha, huku wengine waliwaona mwaka jana na kujaribu bidhaa zao hivyo mwaka huu kurudi tena.

Alisema, pia kuna madereva wa malori kutoka nchini humo huwa wanasafirisha bidhaa hizo, lakini kuuzwa kwa bei kubwa tofauti na katika maonesho hayo, ikiwemo maziwa na juisi kutoka kampuni za Inyange zimekuwa zikipendwa sana.

Alitaja bidhaa kutoka nchini Tanzania zinazopendwa Rwanda kuwa ni vyakula hasa mchele pamoja na mafuta ya alizeti ambapo kuna fursa kubwa ya biashara ikiwa watanzania watapeleka vitu hivyo.

Alitaka serikali ya Tanzania kujitahidi kutoa elimu na kutangaza manufaa ya mwingiliano wa nchi hizo, kwani watu kutoka nchi nyingine zimekuwa zikitumia fursa ya watanzania kufanya biashara kutokana na kutojiamini kwao na kuogopa kuthubutu.

Alisema Tanzania kuna njia nyingi za karibu kuingia nchi nyingine za EAC, lakinihawajatumia vema, ikiwemo biashara ya hiliki, mdalasini, ndizi kwa ajili ya chakula na kusindika pombe ambapo kuna wafanyabiashara kutoka Rwanda huchukua bidhaa hizo kwa bei nafuu na kuuza kwao kwa gharama kubwa.

Alisema wamekuja na mchoraji picha katika mbao na amemchora Rais John Magufuli anayeuzwa Sh milioni mbili. Maonesho hayo yaliyoanza Juni 28, mwaka huu yatamalizika Julai 13 huku yakiwa na washiriki zaidi ya 2,500 kutoka ndani ya nchi na nchi zaidi ya 33.

MKUU wa Mkoa wa Iringa Ally Hapi amekataa ombi la ...

foto
Mwandishi: Theopista Nsanzugwanko

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi