loader
Picha

Bodaboda kufungwa tela

WAZIRI wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Kangi Lugola amesema dawa ya madereva wakorofi wa pikipiki za kibiashara maarufu bodaboda, ni kuzifungia matela ili kudhibiti ajali.

Waziri Lugola ameyasema hayo alipotembelea banda la Polisi katika Maonesho ya 42 ya Biashara ya Kimataifa ya Sabasaba katika Viwanja vya Mwalimu Nyerere, Barabara ya Kilwa jijini Dar es Salaam.

Mkuu wa Dawati la Mafunzo katika Kikosi cha Matengenezo ya Magari ya Polisi katika Chuo cha Mafunzo ya Udereva cha Ufundi, Mkaguzi wa Polisi, Hamisi Membe, alimweleza Waziri kuwa, ili kupunguza ajali zikiwamo za pikipiki, wanaendesha mafunzo ya uendeshaji pikipiki.

“Mheshimiwa Waziri, tumesukumwa kutoa nguvu na utaalamu ili kuongeza juhudi za kudhibiti ajali, kupunguza uhalifu, na kuchochea kipato na uchumi kwa watu, kwa kutekeleza sera ya ushirikiano baina ya sekta ya umma na binafsi (PPP) ya mwaka 2008.” amesema Membe.

Waziri Lugola amesema ili kudhibiti mwendokasi, kupunguza ajali za barabarani na kuwaongezea kipato waendesha bodaboda kwa kuongeza idadi ya abiria, upo mpango wa kuzifungia tela maalumu pikipiki za biashara ya usafirishaji.

“Pikipiki zote zitafungwa tela nyuma ili kupunguza mwendo. Abiria sasa hawatakuwa mshikaki tena, bali ni abiria halali na mshikaki sasa baibai maana mwendesha bodaboda sasa hutaweza kupenyapenya teana,” amesema Lugola.

Kabla ya kuyasema hayo aliitoa fursa kwa wananchi kumweleza kero wazipatazo wanapohitaji huduma katika vituo vya polisi.

Mmoja wa wananchi alisema baadhi ya askari polisi wanasababisha ajali na madhara kwa waendesha bodaboda wanapotaka kuwakamata katika makutano ya barabara, hali inayowafanya waendesha bodaboda hao kutimka hovyo na kusababisha ajali.

Akijibu swali la mwananchi aliyetaka kujua ni kosa la nani kati ya mwendesha bodaboda na abiria anayekataa kuvaa kofia ngumu, Lugola alisema: “Ili mtu awe na sifa za kuwa abiria wa bodaboda, lazima avae helmeti.

Akikataa kuvaa, anapoteza sifa za kuwa abiria kwenye bodaboda yako sasa ukilazimisha kumchukua, unakuwa na kosa; lazima avae au umuache.”

Aliwataka waendesha bodaboda kufuata taratibu, kanuni na sheria za usalama barabarani hivyo, kutowaogopa askari na kukimbia hovyo, bali kuwapa ushirikiano wanapotaka kufanya kazi zao kuimarisha ulinzi na usalama wa raia na mali zao barabarani.

“Bodaboda kuweni wastaarabu ili msiendelee kupoteza maisha na viungo vyenu; mjali maisha yenu,” alisema.

Katika hatua nyingine; Waziri Lugola alitoa onyo kali kwa baadhi ya askari katika vituo aliosema wanalichafua Jeshi la Polisi kwa kuwa kero kwa ndugu wanaotaka kujua sababu za ndugu zao kukamatwa na hata wanaowapelekea chakula. Alisema wananchi wana sababu muhimu na haki ya msingi kujua kosa lililosababisha ndugu yao kukamatwa. “Baadhi ya askari wanalipaka matope jeshi kwa kuwambia wananchi hao, toka hapa la sivyo na wewe utaingia huku (rumande); nenda kamsubiri huko akitoka atakamwambia kwanini alikamatwa...” Akaongeza: “Mama anakuja na chakula; kikapu labda kina chai au chakula kingine, tunayo dhamana ya kumlisha mahabusu wetu, kama askari una uhakika kuwa amekula, mwelezeni kwa lugha ya kiungwana, sio anakaa hapo muda wote na chakula chake hajui kinachoendelea...”

MKUU wa Mkoa wa Iringa Ally Hapi amekataa ombi la ...

foto
Mwandishi: Joseph Sabinus

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi