loader
Picha

Waziri aagiza 25% makato iwekezwe

VIONGOZI wa vyama vya wafanyakazi nchini wametakiwa kujitafakari na kutumia vizuri makato ya wafanyakazi kwa kuwekeza katika miradi, badala ya kutumia fedha hizo kuendeshea ofisi tu.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais(Tamisemi), Selemani Jafo ametoa agioz hilo jijini Dodoma jana wakati akizindua rasmi ununuaji wa hisa kutoka Taasisi ya Talgwu Microfinance PLC ili kuuza kwa wanachama wake.

Jafo amesema viongozi wa vyama vya wafanyakazi wanatakiwa kujitafakari badala ya kutumia asilimia mbili za makato ya wafanyakazi kuendeshea ofisi, watumie asilimia 25 ya fedha hizo, katika kuwekeza kwenye vitega uchumi.

Jafo amesema vipo vyama vya wafanyakazi ambavyo havifanyi vizuri, hata kama Talgwu inafanya vizuri kwani imeamua kuuza hisa asilimia 49 za Microfinance kwa wanachama na asilimia 51 zinabaki kuwa za mamlaka yenyewe.

Amesema, viongozi wengi wa vyama hivyo wakiwemo makatibu wamekuwa wakitumia vibaya makato hayo ya wanachama, wengi wao hata baada ya kuondoka madarakani wameanzisha vyama vyao vya wafanyakazi ili kuendelea kupata fedha hizo za makato.

“Viongozi tafakarini mwenendo wenu namna mnavyohudumia wanachama wenu, jiulizeni michango ya makato ya wanachama imetumika kwa jambo gani,” alisema.

Alisema wafanyakazi wengi wanakuwa na maisha magumu baada ya kustaafu kutokana na ukweli kwamba wanakuwa hawana mishahara na hawajawekeza popote, hivyo kuwafanya wafe mapema.

Alisema usimamizi wa michango ya wafanyakazi, umekuwa ukifanywa na sekretarieti peke yake, watu wamekuwa wakikatwa na hawapewi mrejesho wa makato yao. Jafo alisema wakati akiwa mbunge alikusudia kupeleka hoja binafsi bungeni kuomba vyama vya wafanyakazi visitumie fedha zote za makato ya wafanyakazi kwa ajili ya uendeshaji, lakini sasa ni waziri hana budi kulisema hilo

Amewapongeza Talgwu kwa kuingia kwenye soko la hisa na kuamua kuuza hisa kwa wanachama wake, lakini akasema wanaweza kufanya vizuri zaidi kwa kuanzisha viwanda vikiwemo vya kubangua korosho ili kuachana na mtindo wa kusafirisha zao hilo likiwa ghafi nje ya nchi.

Mkurugenzi Mkuu wa Talgwu Microfinance, Jackson Ngalama amesema, taasisi hiyo imejipanga katika kuboresha maisha ya wanachama wake 58,000 kwa kupanua mtaji wake.

Alisema wazo la kuuza hisa kwa wanachama wanataka kuongeza mtaji kwa kupata Sh bilioni 6.037 kutoka kwa wanachama 6,037 ambapo kila mwanachama anaweza kununua hisa kuanzia 50 kwenda juu kwa hisa moja kuuzwa Sh 1,000.

Amesema, uuzaji wa hisa hizo ukifanikiwa wataongeza kiwango cha mikopo na idadi ya wakopaji. Pia watashusha riba ya kukopa kutoka asilimia 17 hadi 15, wataongeza muda wa kukopa kutoka miezi 36 hadi miezi 60.

Amesema, wanachama watakaonunua hisa watakuwa na faida nyingi zikiwamo za kuwa na uhakika wa kupata gawio kila mwaka, kutumia hisa zao kama dhamana, kutimia taasisi kama jukwaa la kustaafia na watakuwa na uwezo wa kukopa baada ya kustaafu.

Mwenyekiti wa Talgwu Taifa, Selemani Kikungo alisema, wao kama mamlaka kupitia taasisi hiyo Talgwu Microfinance PLC, wamejipanga kuhakikisha wanaboresha maisha ya wafanyakazi wao kwa kuwapa fursa ya kununua hisa za microfinance yao.

Serikali imeagiza viongozi wa Mamlaka ya Usafirishaji Nchi Kavu na ...

foto
Mwandishi: Magnus Mahenge, Dodoma

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi