loader
Picha

Dar ingekuwaje kama mabondeni wasingehamishwa

“Tunapongeza mafisadi kubanwa, kuhama mabondeni hatutaki.” Kimsingi, nilikuwa ninaunga mkono hatua ya vunjavunja maeneo ya bondeni kwa kuwa ilikuwa muhimu kwa nchi. Niliwakumbusha Watanzania kwamba, wakati wa kampeni, Serikali ya Awamu ya Tano, iliahidi kuwa itajitahidi kurekebisha mambo ‘yaliyokaa tenge.’

Moja ya mambo hayo, ni suala la kuhamisha watu wanaoishi katika maeneo hatarishi yakiwamo ya bondeni). Hata waliokuwa wakilalamika wakiwemo wanasiasa wanaotafuta mahala pa kupatia umaarufu wa kisiasa, yaani ‘kiki’ kama wanavyoita vijana, walikuwa wanajua athari za kujenga mabondeni zilivyo nyingi.

Licha ya kujua madhara hayo yakiwamo kusababisha au kuimarisha mafuriko ambayo huwaathiri kwanza hao hao waliojenga mabondeni na watu wengine, wanasiasa watafuta kiki wengine walijaribu kuwatetea walio mabondeni ili waendelee kukaa mazingira hatari ili linapotokea la kutokea, wapate jukwaa la kuzungumzia.

Kutokana na mvua zinazoendelea kunyesha Dar es Salaam, hadi kufikia juzi wakati ninaandaa makala haya, vifo vya watu 15 vilikuwa vimeripotiwa kutokana na athari za mvua hizo.

Kamanda wa Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Lazaro Mambosasa, alisema watu hao walikufa kutokana na kuangukiwa na kuta za nyumba pamoja na kusombwa na maji.

Ingawa bado kuna watu wanaishi maeneo ya bondeni, na ingawa vifo hivyo ni vingi, hali ingekuwa mbaya zaidi kama serikali isingeshikilia msimamo wa kuwanusuru watu kwa kuwaondoa mabondeni.

Kimsingi, maafa ya mafuriko hayahusishi vifo pekee, bali pia mali za wananchi na hivyo kama watu wasingehamishwa kwa nguvu toka mabondeni wakati ule, wengi wangepoteza mali zao sasa.

Tukiacha hilo la uhatari wa kuishi mabondeni ambapo mimi ninaihimiza serikali kuzidi kuondoa watu waliosalia au kurejea tena mabondeni, ni vema tujadili pia suala la mafuriko na serikali kuchukua hatua dhidi ya visababishi vyake.

Mwanamazingira nguli nchini, Dk Felician Kilahama, aliwahi kuandika makala akisema, mafuriko ni matokeo ya mwanadamu kutokuwa rafiki wa mazingira yake.

UJENZI KWENYE MIKONDO YA MAJI

Mwaka 2015, kama ilivyo ada, Dar es Salaam, ilipata mafuriko na Rais Jakaya Kikwete (wakati huo) alipotembelea Wilaya ya Kinondoni, Ofisa Mwandamizi wa Manispaa ya Kinondoni, Baraka Mkuya, alisema wananchi waliovamia maeneo katika mikondo ya maji na kujenga makazi yao, walikuwa chanzo mojawapo cha mafuriko.

“Chanzo kikubwa cha mafuriko katika maeneo mengi ni wananchi kuvamia mikondo ya maji pamoja na kujenga maeneo ya mabondeni.

Hivyo maji hukosa mkondo na kuingia kwenye makazi badala ya kwenda baharini moja kwa moja,” alisema Mkuya ambaye kitaaluma ni mhandisi.

Mkuya aliweka wazi mbele ya Kikwete kuwa, ili kupata ufumbuzi wa kudumu dhidi ya mafuriko, iwekwe mipango thabiti kuzuia wananchi kuvamia maeneo ya mikondo ya maji na kutojenga mabondeni. Kikwete alianza kuagiza bomoabomoa hizo kunusuru wananchi, kabla uongozi wa Rais John Magufuli haujaendeleza jukumu hilo.

Rais mstaafu Kikwete, aliagiza mamlaka husika ikiwemo Manispaa kubomoa nyumba zilizo katika mikondo ya maji na kujenga mifereji mikubwa ya kudumu.

Kikwete alisema: “Acheni tabia ya kujenga nyumba katika maeneo yenye mikondo ya maji au mabondeni, maana kila msimu mnakuwa waathirika wa mafuriko yanayowarudisha nyuma kimaendeleo. Mkubali kuhama sasa.”

KILIMO NA UFUGAJI

Wakati sababu kubwa inayochangia mafuriko katika Jiji la Dar es Salaam ikitajwa kuwa ni ujenzi katika mikondo ya maji, sehemu nyingine za nchi yetu kama Morogoro sababu zinazotajwa ni kilimo, ufugaji na ukataji miti usio endelevu.

Dk Kilahama anasema, baadhi ya Watanzania wana utamaduni wa kuwa na mifugo wengi kuliko uwezo wa kiikolojia wa eneo husika kuhimili wingi huo.

Anasema wafugaji hao hupenda kuchunga mifugo yao badala ya kufuga kwa kutumia eneo moja. Dhana ya kuchunga mifungo inamaanisha kwamba, wenye mifugo, bila ya kujali wingi wa mifugo waliyo nayo, kila kukicha huitoa kwenye boma na kuipeleka machungani, kisha kuirejesha jua linapokuchwa na giza kuingia.

Anasema nyakati hizi maeneo ya kuchungia mifugo yameendelea kupungua na kusababisha wafugaji kukosa sehemu za kutosheleza mahitaji yao ya kuchungia lakini pia, kutokana na wingi wa mifugo hali hiyo inakuwa mbaya zaidi.

Anasema sababu nyingine ya mafuriko ni kulima katika mikondo ya maji hadi kwenye kingo za mito na kukiuka sheria inayowataka wananchi kufanya shughuli za kibinadamu mita 60 au 30 kutoka kwenye mkondo wa maji kutegemea eneo husika.

Kilimo nchini Tanzania, kwa mujibu wa Dk Kilahama, hasa sehemu za bara, kimeendelea kwa miaka mingi kuwa “sumu” kwa uharibifu wa misitu na uoto wa asili.

Anasema wakulima wengi na kwa zaidi ya miaka hamsini iliyopita tangu tupate uhuru na kujitawala, hawajaweza kuendesha shughuli za kilimo katika misingi iliyo rafiki kwa mazingira yanayowazunguka.

Dk Kilahama anasema sehemu nyingi vijijini kilimo kimekuwa ni cha kuhamahama, njia ambayo ni duni na madhara yake kwa kuharibu misitu na uoto wa asili ni makubwa.

"Hii inatokana na ukweli kwamba mkulima anachagua eneo analoliona linafaa kwa shughuli za kilimo, anafyeka misitu na kuchoma moto miti aliyoifyeka pamoja na uoto mwingine wa asili katika eneo husika. “Eneo hilo mkulima anaweza kulitumia kwa miaka miwili au mitatu na anapoona mavuno yamepungua kutoka takribani zaidi ya gunia kumi kwa ekari moja hadi gunia tatu au nne, anahamia eneo lenye misitu lililo karibu naye, hivyo kufanya kama alivyofanya kwenye eneo lililotangulia," anaandika Dk Kilahama.

MKAA ENDELEVU

Wakati kilimo kinasababisha uharibifu wa misitu, ukataji miti kwa ajili ya kuni na mkaa usio endelevu pia unatajwa kuwa sababu ya kuharibu misitu na kuchangia mafuriko.

Ndio maana mashirika matatu: Shirika la Kuhifadhi Misitu ya Asili Tanzania (TFCG), Mtandao wa Jamii wa Usimamizi wa Misitu Tanzania (MJUMITA) na Shirika la Kuendeleza Nishati Asilia (TaTEDO), yamekuja na Mradi wa Kuleta Mageuzi katika Sekta ya Mkaa Tanzania (TTCS).

Kupitia ufadhili wa Shirika la Maendeleo na Ushirikiano la Uswisi, mradi huo unawawezesha wanavijiji kufanya uzalishaji endelevu wa mkaa ili kulinda misitu inayowazunguka kutokana na kuona faida zake za moja kwa moja.

Bila shaka mradi huo unaohimiza matumizi bora ya ardhi na kuwawezesha wanakijiji kuendesha kilimo kisichoharibu mazingira ukienezwa nchini utasaidia kulinda msitu na vyanzo vya maji.

Ni wakati sasa serikali ichungulie kilichomo katika mradi huo unaoendeshwa katika vijiji 30 mkoani Morogoro na kuusambaza nchini kote. Sera mpya misitu inayoandaliwa, ichote mengi kutoka katika mradi huo wa TTCS.

HASARA ZA MAFURIKO

Kimsingi, mafuriko husababisha hasara nyingi kwa watu na serikali ikiwamo ya watu kupoteza maisha, jambo ambalo serikali makini haiwezi kulifumbia macho.

Mafuriko husababisha watu kupoteza mali na kukosa mahala pa kuishi maji yanapoingia hadi kwenye makazi yao.

Kadhalika, huharibu miundombinu kama barabara na madaraja na kuathiri huduma za usafiri na usafirishaji, hivyo kusababisha kupanda kwa gharama za maisha.

Hali hiyo huilazimisha serikali kutumia gharama kubwa kuokoa maisha ya watu wake wanaoathirika, kuwatafutia mahali pa kuishi na huduma muhimu, na hata kujenga upya miundombinu. Kadhalika, serikali hupoteza mapato kutokana na baadhi ya shughuli za uzalishaji kusimama kutokana na mafuriko.

Kwa msingi, hatua za kuondoa watu mabondeni, kuzuia ujenzi kwenye mikondo ya maji, kusaidia na kusimamia wananchi kulima kilimo hifadhi na miradi kama ule wa kuleta mageuzi ya mkaa nchini (TTCS), inapaswa kupewa kipaumbele.

KATIKA maeneo mengi nchini watu wamekuwa wakiishi kwa amani na ...

foto
Mwandishi: Hamisi Kibari

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi