loader
Picha

JPM ametoa elimu bure wafanyabiashara itumieni

Aliwataka kujiuliza ni kwa nini licha ya uwepo wao nchini, bado taifa linalazimika kutumia rasilimali zake zikiwapo pesa za kigeni, kuagiza na kununua baadhi ya bidhaa kutoka nje ya nchi huku malighafi za kuzalisha bidhaa hizo kama sukari, zinapatikana kwa wingi nchini.

Katika mazungumzo hayo kwenye Mkutano wa 11 wa Baraza hilo uliofanyika Ikulu, Dar es Salaam, Rais Magufuli alisema hakuna sababu kwa taifa hili kutumia fedha nyingi za kigeni kuagiza sukari kutoka nje ya nchi, wakati wafanyabiashara wa Tanzania wana uwezo wa kuzalisha sukari hiyo hapa nchini na hata kuuza nje ya nchi.

Kimsingi, tunaungana na Rais Magufuli kusema, Tanzania ina rasilimali nyingi ambazo Watanzania wakiwamo wafanyabiashara wakizitambua na kuzitumia vizuri, wataliongezea taifa kasi ya kuelekea katika uchumi wa viwanda.

Hii ni kwa kuwa Tanzania kuna madini ya aina mbalimbali, kuna mito, maziwa na bahari, mambo yanayoweza kukoleza kilimo cha umwagiliaji ili kutosheleza mahitaji ya viwanda na pia, hata hali ya hewa ya kawaida, inaruhusu na kuwezesha uzalishaji wa malighafi nyingi yakiwamo matunda na mazao kama pamba na mengine kwa ajili ya viwanda.

Kwa msingi huo, tunasema kinachohitajika kwa wafanyabiashara wetu, ni moyo wa uzalendo na umoja miongoni mwao ili kuanzisha na kufanya uwekezaji mkubwa katika viwanda, kilimo na sekta nyingine.

Bahati kubwa kwa Tanzania ni kuwa, kuna mazingira rafiki ya uwekezaji kutoka kwa wazawa na hata wageni. Tunasema, uwekezaji wa ndani ya nchi ni muhimu kwa kuwa licha ya kuokoa pesa za kigeni zisiende nje kutokana na manunuzi zaidi kuliko kuuza nje, pia unawezesha kutoa ajira kwa wazalendo na kuongeza kiwango cha ukusanyaji kodi kwa maendeleo na manufaa ya nchi.

Sisi tunaamini kuwa, wafanyabiashara nchini wakilitafakari na kulielewa vizuri somo alilotoa Rais Magufuli alipozungumza nao juzi, wataona hata umuhimu wa kuungana na kukopa katika benki na taasisi nyingine za kifedha ili kupata mitaji ya kutosha na endelevu kuanzisha viwanda na uwekezaji mkubwa zaidi nchini.

Uwekezaji huo tunasema, licha ya kusogeza huduma na bidhaa kwa wananchi, utawezesha kupatikana kwa soko la mazao ya wakulima kirahisi, utatoa ajira kwa wananchi na pia, utawezesha taifa kuuza bidhaa zake nje ya nchi zaidi, kuliko kununua na hivyo, kuufanya uchumi wa nchi kuimarika.

Wakati tukisema kwa dhati kuwa JPM ametoa elimu ya bure kwa wafanyabiashara nchini, watambue kuwa hawana budi kuitumia huku wakizingatia kuwa, umoja ni nguvu na pia, mcheza kwao hutunzwa.

KATIKA gazeti la leo, kuna habari kuhusu Mamlaka ya Mapato ...

foto
Mwandishi: Mwandishi Wetu

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi