loader
Picha

Mauzo zao la karafuu yavunja rekodi

Mafanikio hayo yamekuja baada ya wananchi kuhamasika kuuza karafuu zao katika Shirika la Taifa la Biashara (ZSTC) na kuachana na kuuza karafuu yao kwa magendo. Akizungumza wakati wa kuelekea kwenye Jukwaa la Biuashara linalofanyika hapa Zanzibar Machi 16, Mkurugenzi Mwendeshaji wa ZSTC, Dk Said Seif Mzee anasema shirika linajivunia mafanikio hayo makubwa ambayo yametokana na wakulima kufahamu majukumu yao katika zao la karafuu ambalo ndiyo uti wa mgongo wa Zanzibar. Jukwaa la kutangaza fursa za Biashara Zanzibar limeandaliwa na Kampuni ya Magazeti ya Serikali (TSN) kwa kushirikiana na Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais. TSN ndiyo inachapisha gazeti hili, Daily News na SpotiLeo.

Anasema magendo ya karafuu yalikuwa kikwazo katika kufanikisha maendeleo ya zao hilo kwa zaidi ya miaka 10 na kwamba katika kipindi hicho, idadi ya tani zilizouzwa msimu huu hakijawahi kufikiwa. Anasema katika msimu wa mavuno ya karafuu wa mwaka 2017-2018 magendo yalidhibitiwa kwa kutumia vyombo vya dola huku wakulima wenyewe wakiamua kusema ‘sasa basi kwa kuuza karafuu kimagendo’ na hivyo kuitikia wito wa kuuza karafuu yao kupitia Shirika la Taifa la Biashara.

“Shukrani zetu za dhati ziwaendee wakulima ambao wamekubali wenyewe kuachana na magendo ya karafuu na kuuza karafuu kwa ZSTC,” anasema na kuongeza kwamba hatua hiyo inachangia serikali kudhibiti mapato yatokanayo na zao hilo na hivyo kuchangia katikia huduma mbalimbali kwa wananchi. Magendo ya karafuu yamekuwa yakifanyika zaidi katika kisiwa cha Pemba na inasadakika kwamba karafuu ilikuwa ikisafirishwa kwenda Mombasa katika nchi jirani ya Kenya kwa kutumia bandari bubu.

Akitoa takwimu za mafanikio ya mavuno ya karafuu mwaka huu, Dk Mzee anasema hadi kufikia Januari 5 ya mwaka 2018 jumla ya tani za karafuu 8,470 zenye thamani ya Sh bilioni 118.2 zilinunuliwa kutoka kwa wakulima katika kipindi cha mwaka wa fedha 2017-2018. Dk Mzee anafahamisha kwamba kwa muda wa miaka sita mfululizo, Serikali imekuwa ikinunua karafuu kwa wakulima kwa bei ya Sh14,000 kwa kilo moja, bila ya kujali bei hiyo kama inaweza kushuka katika soko la dunia au la.

Je, nini kimewavutia wakulima wa karafuu, hususaani wa Pemba kuachana na magendo ya karafuu na kuitikia wito wa kuuza karafuu yao kwa ZSTC kwa asilimia 100? Waziri wa Biashara Viwanda na Masoko wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Balozi Amina Salum Ali, anasema serikali inatoa asilimia 80 ya faida inayopatikana katika mauzo ya karafuu ambayo inakwenda moja kwa moja kwa mkulima.

Anasema hakuna nchi yoyote duniani inayozalisha karafuu na kutoa faida ya asilimia 80 kwenda moja kwa moja kwa mkulima zaidi ya Zanzibar na kwamba hizo ni juhudi za makusudi zinazofanywa na SMZ katika kumjali mkulima na kwamba ni hatua ambayo imevutia wateja. Aidha anasema mageuzi makubwa yaliyofanywa na ZSTC nayo yameleta mafanikio makubwa ikiwemo kuanzishwa kwa mfuko wa maendeleo ya karafuu (CDF).

Akizindua msimu wa karafuu huko Kizimbani Mkoa wa Kaskazini Pemba, Rais wa Zanzibar, Dk Ali Mohamed Shein alisisitiza kwamba Serikali haitolibinafsisha zao la karafuu kwa maana ya kuliingiza katika soko huria. Dk Shein alisema uamuzi huo lengo lake kubwa ni kuhakikisha wakulima wananufaika na mavuno ya kilimo cha zao hilo huku wakiwezeshwa pamoja na kufaidika na mikopo ambayo lengo lake kuwawezesha kiuchumi. Alisema hilo haliwezi kamwe kufanywa na wafanyabiashara huria. Dk Shein alisema kuanzishwa kwa Mfuko wa Maendeleo ya Karafuu lengo lake kubwa ni kuwawezesha wakulima kuwa kitu kimoja na kuweza kuzipatia changamoto mbalimbali zinazotokana na uzalishaji wa karafuu.

“Tumeanzisha mfuko wa uwezeshaji wa wakulima wa karafuu ambao lengo lake ni kuzipatia ufumbuzi changamoto mbalimbali za wakulima wa karafuu ikiwemo mikopo,” alisema. Mkurugenzi wa masoko wa ZSTC, Salum Ali anasema Mfuko wa Maendeleo ya Wakulima wa Karafuu umeanza kazi ya usambazaji na utoaji wa miche ya mikarafuu bure kwa wakulima. Anasema hizo ni sehemu ya juhudi za kurudisha ubora wa zao la karafuu na kuifanya Zanzibar kuongoza kwa uzalishaji wa zao hilo kama ilivyokuwa katika miaka ya 1960.

Anakiri kwamba mikarafuu mingi kwa sasa imechakaa ambapo kazi kubwa inayofanywa na Mfuko wa Maendeleo ya Karafuu ni kuimarisha vitalu vya uzalishaji wa miche ya bora mikarafuu katika visiwa vya Unguja na Pemba. Anazitaja juhudi hizo kuwa ni pamoja na kuwahamasisha wakulima binafsi kuanzisha vitalu vya miche ya mikarafuu pamoja na vile vitalu vinavyomilikiwa na Idara ya Kilimo.

Ofisa wa Idara ya Maendeleo ya Kilimo anayeshughulikia karafu, Badru Mavura anasema wamiliki wa vitalu binafsi sasa wamepiga hatua kubwa na wanazalisha miche ya mikarafuu na kuiuza kwa watu wengine wanaohitaji. “Tumepata mafanikio makubwa. Kwa mfano watu binafsi wapatao 10 tumewapatia elimu ya kumiliki vitalu binafsi ambavyo vitazalisha miche ya mikarafuu kwa ajili ya wakulima,” anasema.

Mkulima Mohamed Shindoma, mkazi wa Wete Pemba anataka Serikali kuendelea na mikakati yake ya kumiliki zao hilo kwani hofu yake ni kwamba likiingia katika mikono ya sekta binafsi linaweza kuyumba na kupoteza mwelekeo wa kibiashara kama ilivyo kwa mazao mengine ikiwemo mwani na mbata. Anasema katika msimu uliomalizika amefanikiwa kujipatia Sh milioni 120 kwa kuvuna karafuu katika shamba la familia yao lenye ukubwa wa eka 50. Anasema sehemu ya fedha hizo zimetumika kwa ajili ya kuimarisha shamba ikiwemo kupalilia na kuweka ulinzi kufuatia kuibuka kwa matukio ya wizi wa karafuu.

“Mimi ni miongoni mwa watu ambao tunafaidika na maendeleo ya kilimo cha karafuu ambapo Serikali inatupa mikopo na fedha za kuyasafisha mashamba yetu na vifaa vya kuanikia karafuu, sasa zao hili likibinafsishwa na kuingia katika soko huria nani atatupa mahitaji kama hayo?” Anahoji. Shirika la Taifa la Biashara kupitia Mfuko wa Maendeleo ya Karafuu limetoa jumla ya Sh milioni 300 kama mikopo kwa wakulima wa karafuu zikilenga kuimarisha kilimo hicho.

Mkopo wa fedha hizo uliotumika kwa ajili ya kusafisha mashamba kwa maandalizi ya kilimo cha karafuu pamoja na kununua majamvi ambayo hutumika kwa ajili ya kuanika karafuu ili kuziweka katika mazingira ya usafi wa hali ya juu. Kisiwa cha Pemba kinaongoza kwa uzalishaji wa karafuu kwa asilimia 98 na sasa wakulima wengi kisiwani humo wakihamasika kuotesha mikarafuu mipya ili kuchukuwa nafasi ya ile iliyozueleka na ambayo haitoi mavuno mengi kwa sasa.

“Faida ya zao la Karafuu tumeziona na sasa kazi yetu kubwa ni kuotesha mikarafuu mipya ili ichukue nafasi ya zamani ambayo imezeeka na kupungua uzazi wake,” anasema Seif Hamad, mkazi wa Mtambwe, eneo linaloongoza kwa uzalishaji wa karafuu kisiwani Pemba. Kuhusu Jukwaa la Biashara litakalofanyika hapa Zanzibar, Dk Mzee anasema litasaidia sana kuibua fursa na kutafuta changamoto mbali mbali za kibiashara kwa manufaa na maslahi ya wananchi wa Zanzibar.

“Sisi ZSTC tunaunga mkono kuwepo kwa Jukwaa la Fursa za Biashara kwa sababu litasaidia kuibua fursa na kuboresha harakati za kibiashara zilizopo kwa kutoa manufaa makubwa kwa wawekezaji wa ndani na nje,” anasema. Jukwaa la Biashara Zanzibar ambalo ni la tano kuandaliwa na TSN, linafadhiliwa na Shirika la Taifa la Hifadhi ya Jamii (NSSF), Tanesco, Bohari la Dawa (MSD), Nabaki Afrika, MarLink na Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (Ewura).

Wadhamini wengine ni Benki za NMB, Azania Bank Ltd, NBC, Benki ya Watu wa Zanzibar (PBZ) na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA). Jukwaa pia linadhaminiwa na Radio ya Tanga Kunani (TK 88.5 FM), Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Maji na Nishati Zanzibar (ZURA), Watumishi Housing Corporation (WHC), Tigo Pesa, Baraza la Taifa la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi (NEEC), Mamlaka ya Usimamizi na Udhibiti wa Sekta ya Hifadhi ya Jamii (SSRA) na Mamlaka ya Usimamizi wa Shughuli za Bima (TIRA).

UTALII unachangia asilimia 25 ya pato la ndani Zanzibar na ...

foto
Mwandishi: Khatib Suleiman

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi