loader
Picha

Mwenge ni utamaduni unaoboresha utamaduni

Taarifa zinaonesha kwamba kuanzia mwaka 1964 baada ya Muungano wa Zanzibar na Tanganyika hadi mwaka 1992, mbio za mwenge wa uhuru zilikuwa zikiratibiwa na kusimamiwa kitaifa na chama cha TANU na ASP na badae CCM kupitia jumuiya yake ya Umoja wa Vijana.

Mwaka 1992 Tanzania iliingia katika mfumo wa vyama vingi, hatua iliyosababisha shughuli za mwenge kuanza kuratibiwa na serikali na hivyo ni mwaka wa 25 tangu mbio za mwenge zirejeshwe chini ya serikali.

Hii maana yake ni kwamba utamaduni wa kukimbiza mwenge wa uhuru hauna itikadi ya kisiasa, dini wala kabila bali ni mali ya watanzania bila kujali itikadi zao.

Licha ya mbio za mwenge wa uhuru kuzindua, kuweka mawe ya msingi na kukagua mradi mbalimbali, wakazi wa mkoa wa Kagera wanachukulia mwenge kama sehemu ya kukumbushia mila na kuendeleza tamaduni zao.

Martha Bilikwija (91), mkazi wa kijiji cha Rwaashonga, kata Bwanjai wilayani Misenyi, anasema alianza kuuona mwenge mwaka 1964 na kwa miaka yote mwenge wa uhuru ulikuwa ukifika maeneo ya vijijini na kusaidia kufufua mila, desturi na tamaduni zilizokuwepo kama vile nyimbo na ngoma za asili. Anasema miaka yote mwenge umekuwa na kazi ya kuwakutanisha watu, wakakaa pamoja katika mkesha, wakala na kunywa huku wakipeana ujumbe muhimu sambamba na kucheza muziki au ngoma za asili.

Bibi huyu anasema amekuwa akifurahia kuona wazee wakipewa kipaumbele kwa kuonyesha michezo ya asili ikiwemo ngoma za mkoa wa Kagera. Anasema tangu akiwa binti mdoho na mpaka sasa anazeeka walikuwa na msemo wa Kihaya usemao: ‘Omwenge tigushubha nyuma’ akiwa na maana kwamba mwenge ukishatoka eneo haurudi bali unasonga mbele.

Akifafanua tafsiri pana ya neno hilo anasema linamaanisha kwamba ukishaamua kufanya maendeleo au kuanzisha kitu usiangalie wala kurudi ulikotoka bali usonge mbele.

Anasema miaka ya nyuma wananchi walikuwa wakilima barabara ili Mwenge wa Uhuru upite bila bughudha huku baadhi wakishiriki kutengeneza madaraja kwa mikono pale ambapo pangeonesha kikwazo kama maeneo yenye maji na maeneo yasiyopitika.

Anasema katika mkesha wa mwenge wa uhuru, enzi zao kijiji kizima wanawake walishiriki ikiwemo kumenya ndizi na kupika huku wanaume wakichinja wanyama kama sehemu ya kitoweo kwa ajili ya chakula.

Anasema wakati huo ngoma za asili na nyimbo za asili ndizo zilizotumika karibu wakati wote wa mkesha wa mwenge. Anasema kila kijiji kiliandaa zawadi mbalimbali kama ishara ya upendo, umoja na kudumisha ushirikiano na kwamba zawadi hizo zilikabidhiwa kwa kiongozi wa mbio za mwenge wa uhuru kitaifa ili iwe ishara ya kukumbuka eneo hilo.

Bibi huyu anasema tofauti na zamani, zama hizi wakimbiza mwenge kitaifa, kimkoa na kiwilaya huandaliwa mazingira mazuri zaidi huku wakipita kweye barabara zinazowafikisha wanakokwenda bila kujaa vumbi kutokana na maendeleo ya miumbonu yaliyofikiwa sasa.

Anashukuru kuona serikali ya mkoa wa Kagera ikiandelea kualika vikundi mbalimbali vya ngoma ili kutambulisha utamaduni wa mkoa na vijana wa sasa kuona ngoma zao.

Deogratias Lucas (65), mkazi wa Kata Bwanjai anasema kwa sasa licha ya mwenge wa Uhuru kuendeleza utamaduni uliopo bado miradi inayozinduliwa na mwenge ni mingi tofauti na zamani.

Anasema wanaosema mwenge wa uhuru hauna umuhimu katika zama hizi wanapaswa kupingwa kutokana na ukweli kwamba, mbali ya kuhuisha tamaduni na kufikisha ujumbe kwa wananchi, mwenge unaleta mshikamano, ushirikiano na furaha pale unapokuwa umewakutanisha watu kwa pamoja.

“Tunapata furaha sana kuona angalau mwenge unatangaza ngoma zetu, watu wanacheza ngoma yao na vikundi vinajitangaza kupitia mbio za Mwenge wa Uhuru huku miradi mbalimbali ya maendeleo ikiongezeka mwaka hadi mwaka,” anasema.

Melania Alberth (75), mkazi wa Mkoa wa Kagera anasema kuwa wazee ndio walishiriki zaidi zamani katika masuala ya kuendelea utamaduni katika mbio za mwenge wa uhuru kulinganisha na sasa.

Anasema kuwa maboresho ya sasa ni makubwa kwani mila na desturi kupitia Mwenge zinaendelezwa kupitia mbio zake japo kuna mabadiliko kiasi kulinganisha na zamani huku akisema kuwa kwa sasa Mwenge unaweza ukakimbizwa katika wilaya husika na asiwepo mtu wa kuwaalika wazee.

Ananias Bantangireki (76) mkazi wa mtaa Kisharu, Kata Kashai katika Manispaa ya Bukoba anasema kinachomvutia kwenye mwenge ni pamoja na ngoma za asili na watu kushiriki pamoja katika mkesha, jambo linaloongeza umoja na mshikamano kwa wananchi wa eneo husika.

Anasema kingine kilichomfurahisha katika mbio za Mwenge wa Uhuru mwaka huu mkoani Kagera ni uzinduzi wa miradi na uboreshaji wa barabara ulikopita mwenge.

Anasema mara nyingi miradi ambayo huwa imekwama kwa muda mrefu huwa ‘inakwamuka’ na kisha kuzinduliwa na mbio za mwenge.

Paulo Maganga (78), mkazi wa kata Rusaunga wilayani Biharamulo, anasema kwa sasa ushiriki wa wananchi katika mbio za mwenge umekuwa pia ukiwanufaisha wafanyabiashara kuinua uchumi kuliko miaka ya nyuma ambapo watu walikesha tu bila kuuza bidhaa zao.

Katika muktadha, Thomas Msigaro (66), mkazi wa Nyakanazi wilaya ya Bihalamulo anasema kuwa zamani ilikuwa kijiji husika ndicho huratibu mbio za Mwenge wa Uhuru kwa kujifanyia kila kitu.

“Mabadiliko ya sasa ni kwamba, kampuni mbalimbali za upishi na mapambo zinashindana kufanya vizuri kama kupamba na kupika chakula katika mbio za mwenge ili wapate tena tenda mwaka ujao. Hivyo mwenge unasaidia wananchi kupata kipato,” anasema.

Musa Shomari maarufu kama Moses Nyama, kiongozi wa kikundi cha Kakau Band mjini Bukoba anasema kuwa kila mwaka kikundi chao kimekuwa kikiandaa nyimbo nyingi za mwenge kwa ajili ya kutumbuiza na kufanya vizuri zaidi ili mwaka unaofuata kikundi hicho kichaguliwe na hivyo kutunisha mfuko.

Anasema kwa miaka kumi mfululizo hakuna kikundi kingine cha utamaduni kilichoonesha umaarufu kama kikundi cha Kakau Band hivyo mikesha ya mwenge ndani ya Manispaa ya Bukoba na Halmashauri nyingine mkoani Kagera wamekuwa wakishiriki.

Mtunzi wa nyimbo mbalimbali za asili mkoani Kagera, Mwalimu Mungango maarufu kama JJ Mugango anajinadi kuwa ndiye aliyetunga nyimbo nyingi za hamasa na kuelezea utamaduni mkoani Kagera kuliko mtunzi yeyote.

Anasema kuwa nyimbo zake zinaimbwa na Halmashauri zote pale mwenge wa uhuru unapoingia katika halmashauri zote mkoani humo hivyo kupitia nyimbo zake amekuwa akialikwa kutumbuiza na kujipatia marafiki wapya na umaarufu kupitia mbio za mwenge wa uhuru kila mwaka.

Juma Mohamed, mfanyabiashara ya kuuza nyama katika Manispaa ya Bukoba anasema kuwa mwenge haujabaki katika utamaduni tu, bali pia huwasaidia wafanyabiashara mbalimbali kufanya biashara zao kwa kuuza bidhaa mbalimbali kwa umati wa watu unaojitokeza.

Anasema karibu kila mwaka amekuwa akiuza nyama ya mbuzi na ng’ombe katika mkesha wa mwenge na kujipatia fedha nyingi na hivyo kutamani mwenge uje hata kama ni kila mwezi! Juliana Kamonjo, mkazi wa mtaa wa Mafumbo, Kata ya Kashai, anasema kwenye mkesha wa mwenge huwa anauza vinywaji vya aina zote na nyama ya nguruwe.

Anasema huwa anachinja nguruwe watano hadi sita na wakati mwingine nyama yake inaisha huku wateja bado wakitaka nyama zaidi.

“Kwa kweli kwenye mkesha wa mwenge ninatapa faida japo ni siku moja tu kuliko ninapokuwa katika kijiwe changu cha Society, pale mtaa wa Mafumbo,” anasema.

Gozberth Kamuntu, Ofisa Utamaduni mstaafu wa Halmashauri ya Bukoba anasema kupitia Mbio za Mwenge wa Uhuru, watoto hufaidika na masimulizi mbalimbali ya wazee na kutazama ngoma za asili.

Anatoa mwito kwa vijana nchnini kupenda kujitokeza katika viwanja pale mwenge unapowasili katika maeneo yao ili kujifunza mambo mbalimbali na kupokea ujumbe unaowahusu.

KATIKA maeneo mengi nchini watu wamekuwa wakiishi kwa amani na ...

foto
Mwandishi: Diana Deus

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi