loader
Picha

Oldonyo Lengai unasubiriwa kulipuka tena

Kwa lugha nyingine, mlima huu unatoa ujiuji wa moto (lava) japo ni wenye kiwango kidogo cha joto. Mlipuko wa volkano ya Oldonyo Lengai unakadiriwa kutokea kwa mara ya kwanza mwaka 1883, na kwa mara ya mwisho, ulitokea kati ya Februari na Machi 2008.

Mlipuko huo ulikuwa mwanzo wa mfumo wa kujirudia wa mlipuko wa majivu unaoishi muda mfupi ndani ya mlima huo.

Mkurugenzi wa Sayansi ya Uhai kutoka Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia (Costech), Profesa Mohammed Sheikh anasema utafiti wa mwaka 2013 kuhusu mlima huo, unaonesha kuna uwezekano katika siku za karibuni kutokea kwa mlipuko mwingine kama huo.

Anasema wanasayansi wanajifunza kutoka mitetemo ya Bonde la Ufa la Afrika Mashariki lililotokea kupitia mlipuko wa volkano ya Oldonyo Lengai.

“Hivyo suala la kutokea mlipuko mwingine ni la wakati tu. Wakati wowote kuanzia sasa utatokea,” anasema Profesa huyo.

Alibainisha hayo katika mkutano wa hivi karibuni uliowakutanisha wadau mbalimbali wa jiolojia nchini kujadili kuanzishwa kwa kituo kitakachokuwa kinapata taarifa mbalimbali za majanga nchini, ikiwemo tetemeko la ardhi pamoja na mlipuko wa volkcano.

Mtaalamu huyo anasema jambo hilo linahitaji kuchukuliwa tahadhari kubwa ili hata linapotokea, lisiwe na madhara makubwa kwa jamii kutokana na mlipuko, ingawa mchakato huo unahitaji njia madhubuti za kiufundi na kifedha.

Anasema mlipuko kama huo unapotokea huathiri shughuli za kiuchumi na kijamii kwenye jamii husika kwa viumbe na mazingira, njia za mawasiliano kitaifa na hata kimataifa, utalii na hata uhifadhi wa mambo ya kale.

Anasema, De Schutter alifanya tathmini ya madhara ya mlipuko huo uliotokea mwaka 2008, na kubaini watu zaidi ya 60,000 walikuwa wameathiriwa na majivu ya volkano.

Anasema majivu hayo yalionesha ishara ya kuwa na kiwango cha ‘fluoride’ ambacho ni kiasi kikubwa kulingana na kiwango cha kawaida kilichotolewa na Shirika la Afya Duniani (WHO).

Kiwango hicho kinabainisha, kuwa kiasi kikubwa kama hicho kina madhara katika mazingira hasa kwenye maji ya kunywa ya binadamu.

Kimsingi inabainishwa kuwa, majivu yaliyoanguka ni hatari kwa afya za jamii zinazozunguka mlima hasa kutokana na uvutaji hewa. Kwa mujibu wa WHO, kiwango cha fluoride kilichopo kwenye maji ya ardhini kinachotumika na watu na wanyama ni cha kiwango cha juu kutokana na hali hiyo.

Inaelezewa kuwa, madhara mengine yameonekana kama matatizo ya uvutaji hewa kwa wakazi wa eneo hilo, matatizo ya macho pamoja na ngozi, yakiwemo madhara kwa mazao na mimea.

Profesa Sheikh wa Costech anasema, baada ya mlipuko wa mwaka 2007/2008, zaidi ya watu 10,000 kutoka vijiji jirani vya Naiyobi na Kapenjiro vilivyopo kilomita 25 jirani na mlima huo, waliondolewa.

Hali iliyosababisha kukosekana kwa malisho ya mifugo ingawa baadhi ya makazi yalionesha ni tatizo sugu hasa kwa afya zao, na kuharibiwa kwa mfumo mzima wa kazi za kiuchumi na kijamii hasa Mbuga ya Tanzania ya Serengeti, eneo la Hifadhi ya Ngorongoro na makazi ya Masai.

Volkano katika Oldonyo Lengai ilisababisha mitetemo mikubwa ya dunia iliyosababisha tetemeko la ardhi lenye kipimo cha ‘ritcher 6.0.’

Kenya na Tanzania ziliathirika katika ufuatiliaji wa mifumo ya miji yao ya Arusha na Nairobi. Tafiti mbalimbali kutoka kwa kundi la watafiti kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), zinaonesha kuwa, baada ya mlipuko wa 2008, mayai mengi ya ndege aina ya ‘flamingo’ hayakuatamiwa.

Zaidi mayai 3,000 ya flamingo yaliharibiwa. Takribani flamingo milioni 2.5 wa Afrika Mashariki ambao maisha yao yamekuwa yakitegemea Ziwa Natron, hasa kwa kutagia mayai yao kwa kuwa ni sehemu nzuri yenye usalama, chakula, maji safi kwa kuzaliana flamingo na kulelea, waliathirika.

Kwa kuwa siku yoyote kuanzia sasa mlipuko huo unaweza kutokea, Profesa Sheikh anashauri kuimarishwa kwa vyuo vikuu pamoja na taasisi za tafiti ili kufuatilia mwenendo wa shughuli za volcano katika mlima huo.

Taasisi hizo za utafiti kwa kushirikiana na Idara ya Uratibu wa Maafa, zinatakiwa kutoa tahadhari mapema kuhusu mlipuko wa mlima huo kwa wananchi wanaouzunguka. Anasema Costech kwa kushirikiana na vyuo husika, wanatakiwa kuimarisha na kuanzisha kitengo cha kisayansi cha majanga na maafa, pamoja na vituo vingine vya majanga.

Ushauri mwingine ni kutoa elimu kwa wakazi wa eneo hilo pamoja na ushirikiano kati ya wadau mbalimbali wakiwamo wakuu wa mikoa, wilaya, idara ya maafa na wengine.

Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Uratibu wa Maafa kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu, Bashiru Taratibu, anasema Ofisi ya Waziri Mkuu ndiyo waratibu wa masuala yote ya maafa, hivyo wanataka watengeneze kituo kitakachokuwa kinapata taarifa mbalimbali zikiwemo za tetemeko la ardhi na mlipuko wa volcano.

“Uwepo wa kituo hicho utasaidia kutoa taarifa za awali kabla ya janga kutokea, hivyo kusaidia wananchi kujiandaa kukabiliana na majanga hayo kabla hayajaleta maafa,” anasema.

Anaeleza kuwa hatua hiyo ni nzuri katika kuhakikisha umma unapata taarifa mapema kabla ya majanga kutokea, hivyo kusaidia wananchi kujiandaa kukabiliana nayo kabla hayajaleta maafa.

Profesa kutoka Idara ya Jiolojia ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Hudson Nkotagu, anasema mjadala ulikuwa kuanzisha kitengo cha kisayansi cha majanga na maafa ili kukusanya takwimu za kisayansi za kuwasaidia watoa maamuzi na watunga sera wa nchi kuwa na takwimu za majanga mbalimbali za uhakika. Profesa Nkotagu ambaye pia ni Mratibu wa Jukwaa la Nishati la Taifa, anasema:

“Kwa sasa zinafanyika katika vitengo mbalimbali ambapo wakati mwingine hawafahamiani, hiyo tukiwa na kitengo kimoja kinachoratibu kutafiti na kutathmini, itakuwa rahisi kwa watunga sera na watoa uamuzi katika ngazi mbalimbali kufanya vema zaidi.”

Anasema baada ya majadiliano hayo, wadau wameona ni muhimu kuwa na kitengo hicho cha kisayansi na kiteknolojia kinachojitegemea ili kukusanya na kuratibu takwimu zote za majanga na maafa na kuzichambua. Hili likifanyika, litawarahisishia watunga sera na watoa maamuzi katika usimamizi wa majanga na maafa.

Kaimu Mkurugenzi katika Kurugenzi ya Jiolojia katika Taasisi ya Utafiti ya Jiolojia nchini (GST), iliyopo mkoani Dodoma, John Kalimenze, anasema katika rasimu iliyopitiwa ameona kuna changamoto ya mwingiliano wa majukumu kwa kuwa inatamka baadhi ya majukumu yanayotekelezwa moja kwa moja na ofisi yao.

Anasema kisheria, ili taasisi ipitishwe, haipaswi kuwa na majukumu yanayoingiliana na taasisi nyingine. Kutokana na mwingiliano huo, Costech itaandaa timu ya wataalamu kutoka idara mbalimbali kwa ajili ya kupitia upya rasimu hiyo ili kuondoa muingiliano wa majukumu.

KATIKA maeneo mengi nchini watu wamekuwa wakiishi kwa amani na ...

foto
Mwandishi: Lucy Ngowi

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi