loader
Picha

Saratani shingo ya kizazi hatari, mateso kwa wanawake

Hata hivyo, mwanamke anaweza kukumbwa na saratani hiyo inayosababisha vifo vingi vya wanawake katika nchi zilizo chini ya jangwa la Sahara ikiwemo Tanzania, hata baada ya umri huo.

Takwimu za mwaka 2010 kutoka Shirika la Afya Duniani (WHO), zinaonesha kuwa, Tanzania ina wastani wa wanawake 6,241, wanaougua saratani ya shingo ya kizazi kila mwaka, huku 4,355 miongoni mwao wakipoteza maisha.

Takwimu hizo zinaongeza hamasa kuwa ipo haja kwa serikali, mashirika na wadau mbalimbali kuweka mikakati ya makusudi kuwanusuru wanawake katika hatari ya kukumbwa na maradhi haya hatari yanapochelewa kugunduliwa.

Ripoti nyingine ya WHO, inasema saratani hiyo ni ya nne kwa kusababisha vifo vya wanawake katika nchi zinazoendelea.

Ripoti ya mwaka 2012 ya WHO, inasema kati ya matukio 75,000 ya waathirika wa saratani ya shingo ya kizazi, 50,000 yametokea barani Afrika.

Hata hivyo, takwimu zilizotolewa mwaka jana na Taasisi ya Saratani ya Ocean Road (ORCI), zinaonesha kuwa idadi kubwa ya wagonjwa waliolazwa katika taasisi hiyo ni wanawake na wengi wao wanakabiliwa na aina hiyo ya saratani.

Aina hii ya saratani inawaathiri watu wa tabaka zote ikishika nafasi ya pili duniani miongoni mwa saratani zinazowapata wanawake. Wagonjwa wapya 529,828 wanagundulika kuugua maradhi hayo kila mwaka duniani, huku asilimia 85 miongoni mwao wakitoka nchi zinazoendelea ikiwamo Tanzania.

Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Saratani ya Ocean Road, Dk Julius Mwaisagile, anasema saratani ya shingo ya kizazi inaongoza miongoni mwa saratani zote nchini kwa kuwa ina asilimia 40 ya wagonjwa wote wanaougua aina mbalimbali za saratani nchini.

Dk Mwaiselage anataja moja ya vyanzo vya saratani hiyo kuwa ni kuanza kufanya ngono mapema na kwamba, wasichana wanaowahi kuanza vitendo hivyo wako kwenye hatari zaidi ya kupata maradhi hayo.

“Saratani ya shingo ya kizazi hapa nchini inaongoza kwa asilimia 40 ikifuatiwa na ya ngozi kwa asilimia 20, saratani ya matiti ni ya tatu ina asilimia 12 ya wagonjwa na ya njia ya koromea kwa asilimia tisa,” anasema.

Mkurugenzi huyo anasema baada ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kupitisha mwongozo wa tiba shufaa, kinachoendelea ni kuhakikisha kila hospitali nchini inatoa tiba hiyo.

“Tunashirikiana na wadau mbalimbali kikiwemo Chama cha Tiba Shufaa (TPCA), kuhakikisha huduma hizi zinapatikana hadi katika ngazi za zahanati hapa nchini,” anasema.

Mkurugenzi huyo anafafanua kuwa, wagonjwa wa saratani wanapitia hatua nne ambazo ni mtu akiwahi katika hatua ya kwanza anatibiwa na kupona.

Katika hatua ya pili anaweza kupona kwa asilimia 50, wakati hatua ya tatu na ya nne mgonjwa anakuwa na kiwango cha juu cha maumivu hivyo anahitaji tiba shufaa ambayo ni muhimu kwake.

“Kwa jumla, tiba shufaa inatumika kwa wagonjwa wa muda mrefu ambao wamekata tamaa, inawaondolea maumivu makali na kuwafanya wawe na matumaini makubwa hata kama hawawezi kupona kabisa,” anasema.

Mkuu wa Idara ya Kinga wa ORCI, Dk Crispin Kahesa, anasema saratani ya shingo ya kizazi hushambulia seli zilizoko ndani ya ngozi laini inayozunguka shingo ya kizazi.

Anasema tafiti mbalimbali zinaonesha kuwa asilimia kubwa ya saratani ya shingo ya kizazi inasababishwa na kirusi kinachoitwa Human Papilloma Virus (HPV) kinachoenea kwa njia ya kujamiiana.

“Saratani ya shingo ya kizazi inachukua nafasi kubwa kwa kinamama na hapa Ocean Road ndipo saratani hii inaongoza kwa wanawake,” anasema Dk Kahesa.

Aidha, mtaalamu huyo wa afya anataja tabia zinazochangia mtu kupata saratani ya shingo ya kizazi kuwa ni pamoja na wasichana kuanza ngono wakiwa na umri mdogo. Anasema tabia nyingine hatarishi ni kujamiiana na mwanaume mwenye wapenzi wengi kwani kunakuwa na uwezekano mkubwa wa kusambaza kirusi hicho iwapo mmoja wa wanawake anaohusiana nao, anakabiliwa na saratani ya shingo ya kizazi.

Uvutaji wa sigara nao unatajwa kumweka mwanamke katika hatari ya kukabiliwa na maradhi hayo, kwa kuwa kemikali iliyo katika moshi wa sigara inasababisha ugonjwa huo.

Anataja kemikali ya benzini inayosafirishwa kwa njia ya damu kuwa inaweza kusababisha saratani sehemu yoyote ikiwemo ya shingo ya kizazi katika mwili wa binadamu.

Kahesa anataja tabia nyingine hatarishi kuwa ni matumizi ya mafuta mengi kwenye chakula au kula vyakula vyenye mafuta kwa wingi, kutokula mboga za majani na matunda na upungufu wa kinga mwilini.

“Shida ni kwamba hivi vitu havikai kimoja kimoja, mvutaji sigara huyo huyo anafanya uasherati na hatari inaongezeka kunapokuwa na visababishi vingi,” anasisitiza.

Anafafanua kuwa, saratani ya shingo ya kizazi inaweza kuanza na kukaa kwa muda mrefu bila kuonesha dalili yoyote na kwamba wakati mwingine inapokuja kuonekana ugonjwa unakuwa katika hatua za mwisho.

Miongoni mwa dalili za saratani hii ni kutoka damu isiyo ya kawaida katika njia ya uzazi, kutokwa na damu baada ya mwanamke kufanya tendo la ndoa na au kutokwa damu katika njia ya uzazi kwa wanawake waliokoma hedhi.

Kahesa anasema dalili nyingine ni kutokwa na damu katika njia ya uzazi iliyo na majimaji ya katika njia ya uzazi, matone ya damu au damu kutoka kipindi ambacho si cha hedhi, kutokwa na majimaji au uchafu ukeni wenye harufu mbaya na wakati mwingine ukiwa umechanganyika na damu.

Kadhalika anasema, mtu anaweza kupata maumivu chini ya tumbo, nyonga na kiuno, kukojoa mkojo wenye damu, kupitisha mkojo na haja kubwa kwenye uke na upungufu wa damu.

Anafafanua kuwa, mtu anaweza kujikinga na saratani ya shingo ya kizazi kwa kuepuka ngono katika umri mdogo, kuwa na mwenzi mwaminifu, kuepuka kuvuta sigara, kupima mara kwa mara saratani japo mara moja kwa mwaka, kupata chanjo ya ‘Human Papilloma Virus’ na kuepuka kula vyakula vyenye mafuta mengi.

KATIKA maeneo mengi nchini watu wamekuwa wakiishi kwa amani na ...

foto
Mwandishi: Claudia Kayombo

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi