loader
Picha

TTB kutangaza mambo ya kale kukuza utalii

Mkurugenzi wa Masoko wa TTB, Ernest Mwamwaja amesema moja ya majukumu yao ni kutangaza vivutio vya utalii vilivyopo nchini ikiwemo mambo ya kale kama uwepo wa kimondo cha Mbozi kilicho Mbozi, Songwe.

Amesema hayo katika ziara kwenye kimondo hicho Mbozi na kufanya mkutano na uongozi wa Mkoa wa Songwe ili kujadili namna bora ya kuvitangaza vivutio vya utalii, hasa mambo ya kale. Alisema mambo ya kale ni kivutio kikubwa kwa watalii na wageni wengi wa nje.

“Sisi kama TTB tumeamua kutoa msukumo mkubwa katika kutangaza mambo ya kale. Watalii wa ndani na nje ya nchi huvutiwa kutembelea maeneo kama kimondo,” alisema.

Amesema ni lazima nguvu kubwa itumike katika kutangaza vivutio vya mambo ya kale kwani ndio vinatoa historia nzuri ya taifa na tamaduni.

Alisema mkoa unajiandaa na Siku ya Kimondo Duniani na hiyo ndio itakuwa njia ya kuendelea kutangaza vivutio vya utalii hasa vya mambo ya kale ili kufanya watalii kuongezeka zaidi nchini.

“Lengo letu ni kufikia watalii milioni mbili kwa mwaka na kutokana na vivutio vya Tanzania tuna uhakika idadi hiyo itafikia na kuongezeka,” amesema Mwamwaja na kuongezea serikali imeandaa mazingira mazuri Sekta ya Utalii.

Amesema sekta ya utalii ina mchango mkubwa katika pato la Taifa na mipango iliyopo ni kuifanya kuwa sekta hiyo kuwa sekta kiongozi na kutoa mchango mkubwa kwenye uchumi wa wa kati na viwanda ifikapo mwaka 2025.

Amesema mwito wa TTB kwa watoa huduma za utalii hasa hoteli, wasafirishaji na waongozaji watalii kuandaa safari katika mambo ya kale kama kimondo ni kutanua wigo kwa watalii kutembea maeneo tofauti ya vivutio vilivyopo.

Alisema sekta ya utalii inaweza kuchangia sehemu kubwa katika pato la Taifa kama wadau katika sekta hiyo watashirikiana kuhamasisha na kutangaza utalii wa ndani na nje ya nchini ili kuchochea kuongeza watalii na kufanya kipato kuongezeka kwa mtu mmoja mmoja na taifa.

Mhifadhi Msaidizi wa Kituo cha Mambo ya Kale Kimondo cha Mbozi, Musa Msojo alisema Tanzania imebarikiwa vivutio vingi vya mambo ya kale kama kimondo hicho chenye historia kubwa tangu kilipogundulika mwaka 1930.

“Hii ni nafasi kwa Watanzania na wageni kuja kutembelea kivutio hiki na kujua historia yake kueneza historia na pia kusaidia kukuza pato la taifa kupitia sekta hii ya utalii,” alisema Msojo.

Alisema idadi ya wanaotembelea kivutio hicho ni ndogo kulinganisha na historia yake hivyo kuomba wadau wa utalii kukitangaza kiongeze watalii na kufanya pato la Taifa kuongezeka.

Ziara ya TTB Songwe inalenga vivutio vilivyo katika mkoa huo na kujadiliana na uongozi wa mkoa katika kutafuta njia bora za kuvitangaza vivutio vilivyopo na kuvutia watalii wengi zaidi.

BAADHI ya wafugaji wilayani Rungwe wameitaka Kampuni ya Asas inayojihusisha ...

foto
Mwandishi: Mwandishi Wetu, Mbozi

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi