loader
Picha

Ulemavu si kikwazo, unaweza kufanya unachotaka

Misemo hii ina maana sana kwa binadamu ambaye bado yupo hai. Mtoto Mackson Frank ni miongoni mwa watoto waliobarikiwa vipaji, ingawa katika maumbile yake ya mwili, amezaliwa bila ya kuwa na miguu wala mikono.

Akizungumza na HabariLeo Jumapili, Mackson anaeleza historia yake, changamoto anazokutana nazo na jinsi anavyoshiriki katika michezo na wenzake.

Mackson alizaliwa mwaka 1995 mjini Mtwara, kipindi hicho anakumbuka alikuwa na mama yake ambaye hadi leo anamfahamu kwa jina moja la Ester, lakini baba yake hakuwahi kumuona wala kumsikia sababu anaambiwa alifariki akiwa mdogo.

Anasema hata hivyo akiwa mdogo hajajitambua, alichukuliwa na bibi yake upande wa mama yake na kupelekwa Isanga mkoani Mbeya, ambako aliunganishwa katika kituo cha watoto wanaopewa msaada wa elimu na michezo cha Child Support Tanzania.

“Nilipokuwa kituoni nilijifunza vitu vingi sana kwa kuwa tulikuwa tunajifunza kwa vitendo,” anasema na anaongeza kuwa, kwa kuwa alizaliwa bila ya miguu wala mikono, alianza kufundishwa jinsi ya kushika kalamu kisha kuelekezwa jinsi ya kupiga kinanda baadaye akafanikiwa kuvijua vyote.

Mwaka 2015, Mkuu wa Kituo cha Child Support Tanzania ambaye hamkumbuki jina lake, alimchukua na kumpeleka Dar es Salaam na kuamua kumwanzisha shule, lakini walimkataa kwa sababu hakukuwa na mtu wa kumsaidia kumpeleka chooni.

“Lakini kwangu mimi kuvaa nguo na kwenda chooni hilo sio tatizo. Labda wao hawakuweza kunisaidia kwa kuwa walisema hakuna mtu wa kunisaidia kunipeleka chooni,” anafafanua na anaongeza kuwa baadaye alipata msaada wa ndugu zake upande wa mama yake, ambao waliamua kumchukua na kuishi naye maeneo ya Mburahati, baada ya kupata nafasi katika Shule ya Msingi St Joseph.

Kwa kuwa tayari alikuwa akiweza kushika kalamu na kupiga kinanda, shuleni hapo alijifunza kuandika vizuri lugha ya Kiingereza na kuzungumza kwa ufasaha. Anaandika na kupiga kinanda kwa kutumia sehemu ya kiwiko.

“Nilianza kujifunza kuzungumza lugha ya Kiingereza, kuandika kusoma na kufanya kila kitu kama wanavyofanya wenzangu,” anafafanua Frank kwa kuonesha kwa vitendo na anaoongeza kuwa baada ya hapo akaanza kufuata vitu ambavyo anavitamani na kupenda kama mpira wa miguu.

“Zamani nilikuwa napenda sana mpira, huwa nashangilia ninapoona timu yangu inafunga. Lakini kwa sasa nimeona ni bora niingie kati na mimi nicheze,” anasema na anaongeza kuwa kwa sasa anacheza nafasi ya kipa katika timu yao ya shule, kwa kuwa ana kipaji na anaaminika amekuwa akipangwa kila timu ya shule inapocheza. Anasema mwanzo ilimuwia vigumu kuungana na wenzake katika mchezo wa mpira wa miguu, lakini baadaye alijikuta anaweza na kuwafanya wenzake wamuamini na kumuweka nafasi ya kipa.

Frank anasema katika mpira timu ambayo anaipenda sana ni Simba na mchezaji ambaye anavutiwa naye ni Emmanuel Okwi ambaye anatamani siku zote aendelee kubaki Simba.

Lakini anasema katika soka la kimataifa, anampenda mshambuliaji wa kimataifa wa Ureno, Christian Ronaldo wakati timu anayovutiwa nayo zaidi ni Real Madrid.

Zaidi ya mpira wa miguu, lakini hakuwa nyuma katika kuonesha kipaji chake kingine, Frank anasema yeye ni mtaalamu wa kupiga kinanda, ambako anatumika kuburudisha shughuli za shule.

Anasema ndoto zake anatamani siku moja awe daktari bigwa wa magonjwa ya binadamu, ingawa kwa sasa hajajua atakuwa daktari wa nini. Alisema ndoto hiyo ilianza tangu akiwa mdogo kabisa, kwa kuwa alikuwa akivutiwa na kazi ya udaktari inayofanywa na shangazi yake, Getruda.

Anasema anashukuru wanafunzi wa shule hiyo walimu na wafanyakazi wote, wanamchukulia kama mtu wa kawaida na wanampa msaada wa haraka pindi anapohitaji na kuwa akiwa mkubwa, pia ana ndoto ya kuoa kama ilivyokuwa kwa watu wengine na anaeleza anatamani kukutana na mwanamke ambaye ana roho nzuri na tabia nzuri ambaye atampenda kutokana na hali yake.

Anasema kinanda na mpira wa miguu katika maisha yake vitakuwa vitu vya kumfariji na kufanya kama burudani kwake. Kijana huyu anasema hakuna kitu anachochukia, kwani kila kitu kwake anakichukulia sawa kwa kuwa anaamini kinapita, ila ombi lake kwa serikali wawasaidie watu wenye matatizo kama yeye kwa kuwa wanahitaji sana msaada.

Lakini anasema kwa watu ambao wana ulemavu kama yeye au wa aina yoyote, wasikate tamaa kwa kuwa wanaweza kupigana na maisha pia waangalie zaidi vipaji ambavyo mungu amewapatia.

Mwalimu Hafsa Mataka ambaye ni mwalimu wa Frank, anaelezea jinsi anavyomfahamu na amemuona mwanafunzi huyo tangu alipofika shuleni hapo.

Anasema Frank, kwanza anafanya vizuri katika taaluma ambapo matokeo yake sio mabaya hata kama ukifungua mtandao wa shule hiyo na kuangalia.

Mwalimu Mataka anasema katika mtihani wa darasa la nne kuingia darasa la tano, alifaulu kwa wastani wa alama B, kwani matokeo yake yalikuwa mazuri kwa wastani wote. Katika somo la Jiografia, alipata asilimia 80, Uraia (64%), Teknolojia ya Mawasiliano ‘ICT’ (68%), Stadi za Kazi (67%), Kiingereza (80%), Sayansi (82%), Kiswahili (88%), Historia (82%) na Hisabati (72%).

“Masomo yote hayo yapo katika mfumo wa lugha ya Kiingereza, lakini anaweza kushindana na wanafunzi wengine na kuwashinda,” anasema Mwalimu Mataka na anaongeza kuwa kila siku amekuwa akiwaambia walimu na wanafunzi wenzake kwamba anatamani kuwa daktari, jambo ambalo amekuwa akilisisitiza.

Anasema kitu ambacho Frank anakichukia sana ni kitendo cha kukaa peke yake anasema akikaa peke yake anajisikia vibaya na pia hapendi kuchukia, hata wenzake wanapomuudhi kwa utani uliopitiliza yupo haraka kusamehe na kuendelea na furaha kama vile hakufanywa lolote.

Mkurugenzi wa Shule ya St Joseph, Christa Rweyemamu, naye anaeleza kwa kiasi kidogo kwamba anamjua Frank kuwa mwanafunzi ambaye ana jitihada za kipekee katika kujifunza.

Anasema Frank ni mmoja wa wanafunzi ambao anawasomesha bure, hasa baada ya kuvutiwa na kipaji chake na juhudi zake binafsi na kuwa mwanzo walimuona katika Kituo cha Child Support Tanzania na kumuomba wamsaidie ambapo alipofika hapo walimfanyia majaribio na kufanya vizuri kama wanafunzi wa kawaida.

Rweyemamu anasema baada ya kuvutiwa naye walimwandikisha na kuanza kumsomesha, huku wakiona juhudi zake za kushindana kwenye mitihani na kufanikiwa kufanya vizuri.

“Japokuwa hana mikono wala miguu lakini ana uwezo wa kuandika mwandiko mzuri kuliko wanafunzi wenye mikono, tena anaandika haraka, kwa kuwa anapenda ushindani,” anasema.

Anasema alishawahi kumwambia kwamba kitu ambacho anakihitaji katika maisha yake ni kuwa daktari, jambo ambalo Rweyemamu anasema anaweza kufanikiwa kwa kuwa anapambana ili kushinda.

Rweyemamu anasema kutokana na watoto wa namna hiyo kuwepo wengi mtaani na katika vituo wamekuwa wakikosa elimu bora, ndiyo maana ameanzisha mfuko wa kusaidia watoto wasiojiweza ili kuwapa elimu sawa na watoto wengine.

Anasema mfuko huo wa hisani utakuwa ukichangiwa na wazazi na wanajamii, ambao wataguswa na watoto kama Mackson Frank.

KATIKA maeneo mengi nchini watu wamekuwa wakiishi kwa amani na ...

foto
Mwandishi: Mohamed Mussa

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi