loader
Picha

Wenye mitaji wekezeni Dodoma, Kilimanjaro

Mahitaji ya juu ya umeme nchini, yameongezeka hadi kufikia megawati 1,051 mwaka jana, ukilinganisha na megawati 1,026 mwaka 2016/17.

Kwanza, tunaipongeza serikali kwa kuendelea kuimarisha uzalishaji, usafirishaji na usambazaji wa nishati hiyo nchini. Tunatambua lengo la hatua hiyo ni kuwapatia watu wengi mijini na vijijini nishati hiyo; na pia kuvutia wawekezaji, hasa wakati huu ambapo serikali imedhamiria kuifikisha nchi kuwa ya viwanda ifikapo 2020.

Pili, tumevutiwa na taarifa nzuri za upatikanaji wa nishati hiyo, zilizotolewa na viongozi wa Shirika la Umeme nchini (Tanesco) katika mikoa ya Kilimanjaro na Dodoma.

Mathalani, Ofisa Uhusiano Huduma kwa Wateja wa Tanesco Mkoa wa Dodoma, Innocent Lupenza anasema mkoa wa Dodoma una ziada ya megawati 20 za umeme, ambazo zinaweza kutumiwa na viwanda na wawekezaji, watakaokwenda kuwekeza katika mji mkuu huo mpya.

Kwa mujibu wa Lupenza, umeme uliopo mkoani Dodoma ni megawati 48, lakini matumizi ya juu yaliyowahi kufikiwa ni megawati 28, hivyo kuna ziada ya megawati 20.

Hivyo, wenye viwanda, wageni na wawekezaji, umeme uliopo Dodoma unawatosha. Kwa upande wa Kilimanjaro, Meneja wa Tanesco mkoani humo, Mahawa Mkaka anaeleza kuwa umeme unaozalishwa kwa ajili ya matumizi ni wa kutosha na unakidhi mahitaji ya uwekezaji katika sekta ya viwanda mkoani humo.

Mkaka anasema mkoa wa Kilimanjaro wana umeme unaofikia megawati 135, wakati mahitaji ya mkoa huo hadi kufikia sasa ni megawati 34 tu, hivyo ziada ya megawati zingine zaidi ya 80 inatosha kutumika kwa ajili ya wawekezaji wapya, wanaotarajia kuwekeza mkoani humo. Ziada ya umeme huo, inaweza kutosha kuhudumia wawekezaji hata kwa miaka 10 ijayo.

Kwa ujumla, tunaipongeza serikali, kupitia Tanesco, kujitahidi kuzalisha, kusafirisha na kusambaza umeme mwingi wa kutosha katika maeneo mbalimbali.

Taarifa ya kuwepo umeme wa kutosha katika mikoa hiyo miwili, Kilimanjaro na Dodoma, ni ya kutia moyo, hasa katika kipindi hiki cha kuelekea Tanzania ya viwanda.

Tunatamani usambazaji wa nishati hiyo nchini, utaendelea kuimarika pia katika mikoa na wilaya zingine nchini. Ni dhahiri upatikanaji mzuri wa nishati hiyo, utafanya wawekezaji wengi kwenda kuwekeza katika maeneo hayo.

KATIKA gazeti la leo, kuna habari kuhusu Mamlaka ya Mapato ...

foto
Mwandishi: Mwandishi Wetu

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi