loader
Picha

Yanga wajiandae vizuri kuwakabili Waethiopia

Yanga hapo awali ilikuwa ikishiriki katika mashindano ya Ligi ya Mabingwa wa Afrika, nafasi iliyoipata baada ya kutwaa ubingwa wa Tanzania Bara msimu uliopita wakati Simba ilikuwa ikishiriki Kombe la Shirikisho kabla ya kutolewa.

Yanga nao walitolewa katika mashindano ya Ligi ya Mabingwa wa Afrika baada ya kufungwa na Towship Rollers ya Botswana kwa jumla ya mabao 2-1 yaliyopatikana katika mchezo uliofanyika kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam kabla ya kutoka suluhu katika mchezo wa marudio.

Baada ya Yanga kutolewa katika mashindano ya Ligi ya Mabingwa wa Afrika, timu hiyo imeangukia katika Kombe la Shirikisho kwa mujibu wa utaratibu wa Shirikisho la Soka la Afrika (Caf) ulianza kutumika miaka michache iliyopita.

Wawakilishi hao pekee wa Tanzania sasa watacheza dhidi ya timu ya Ethiopia ya Welayta Dicha FC, ambao mchezo wa kwanza umepangwa kuchezwa jijini Dar es Salaam kati ya Aprili 6 na 8 mwaka huu kabla ya kurudiana nchini Ethiopia.

Kifupi Waethiopia hao kabla ya kufikia hatua ya kucheza na Yanga walicheza na Zimamoto ya Zanzibar na kutoka nayo sare ya kufungana bao 1-1 katika mchezo uliofanyika kisiwani Zanzibar kabla ya kurudiana na wenyeji kushinda kwa bao 1-0.

Timu hiyo ya Ethiopia baada ya kuitoa Zimamoto, walipata nafasi ya kukutana na Zamalek ya Misri, ambapo katika mchezo wa Ethiopia wenyeji walishinda kwa mabao 2-1 kabla ya kurudiana Misri na wao kufungwa idadi kama hiyo ya mabao na mchezo huo kuamuliwa kwa penalti na Wahabeshi walishinda 4-3.

Ukiangalia haraka haraka utabaini kuwa timu hiyo ya Ethiopia siyo nzuri sana, lakini Yanga wanatakiwa kujiandaa vizuri ili kuhakikisha wanashinda kwa mabao mengi kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam ili kujiwekea hazina ya kutosha katika mchezo wa marudiano ugenini.

Baada ya ratiba kupangwa Jumatano katika Makao Makuu ya Caf Cairo, Misri, wadau wengi wa soka pamoja na vyombo vya habari nchini, tayari vinaipa nafasi Yanga kufuzu kwa hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho la Afrika.

Tunasena kuwa katika soka hakuna timu nyepesi na kama hao Welayta Dicha FC waliweza kuwatoa Zamalek ambao mara kadhaa wamewahi kutwaa ubingwa wa Afrika, basi pia wanaweza kufanya maajabu kwa Yanga, hivyo wasidharauliwe kabisa.

Yanga wanachotakiwa kufanya, kwanza ni kuusoma vizuri mchezo wa wapinzani wao, kuwasoma pia wachezaji wao hatari na jinsi ya kuwazuia na kutumia vizuri udhaifu wao kwa kuwafunga mabao mengi. Mabao mengi ni akiba tosha.

Baada ya kuisoma timu hiyo kwa upande wa kiufundi kwa kujua makali yao na udhaifu wao, wanachotakiwa kufanya Yanga ni kuangalia pia hali ya hewa ya huko wanakotoka wapinzani wao.

Ethiopia ni nchi ya ukanda wa juu na yenye baridi, hivyo Yanga wasiangalie tu upande wa ufundi wakasahau hilo la hali ya hewa kwani wanaweza kujikuta wakiumbuliwa na timu hiyo inayoitwa na wengi kuwa ni vibonde.

Yanga wanaweza kupiga kambi Mafinga au Njombe au hata kuna sehemu moja inaitwa Kitulo mkoani Njombe, ili kuzoea hali ya hewa ya baridi ya Ethiopia badala ya kufanya maandalizi jijini Dar es Salaam, ambako kipindi hiki kuna joto kali.

Mfano mwezi ujao, mjini Addis Ababa hali ya joto ya chini inaweza kufikia hadi nyuzi joto 12 wakati ile ya Dar es Salaam inaweza kuwa 30 hadi 23, hivyo baridi inaweza kuwasumbua wachezaji wa Yanga wakiwa nchini Ethiopita.

Yanga wanatakiwa wajiandae katika hali zote kuanzia kisaikolojia, kiufundi na mambo mengine yote ili kuhakikisha wanaitoa timu hiyo ya Ethiopia na kufuzu kwa hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho la Afrika.

Yote kwa yote, Yanga wanaweza kupenya na kucheza hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho, lakini hilo halitakuja bila ya kuwa na maandalizi mazuri na ya uhakika kwa ajili ya kuwakabili Waethiopia hao, ambao hawana jina kabisa Afrika.

KATIKA gazeti la leo, kuna habari kuhusu Mamlaka ya Mapato ...

foto
Mwandishi: Mwandishi Wetu

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi