NFRA yasambaza mahindi kwenye halmashauri 46

WAKALA ya Taifa ya Hifadhi ya Chakula (NFRA), umepeleka mahindi kwenye halmashauri 46 zenye uhitaji na unaendelea kupokea maombi ya maeneo mengine.

Akizungumza na HabariLEO, Ofisa Mtendaji Mkuu wa NFRA, Milton Lupa alitaja baadhi ya halmashauri zilizopelekewa chakula ni Liwale, Nachingwea, Bunda, Mji Geita, Nzega, Sengerema na Monduli. Nyingine ni Ngorongoro, Butiama, Meatu, Kishapu, Longido, Urambo, Handeni, Mkinga, Chemba, Chamwino, Mbulu, Mwanga, Hai, Ikungi, Manyoni, Loliondo, Momba, Mwanga, Kondoa, Musoma DC na Manispaa.

Pia zimo Rorya, Serengeti na Tarime na mkoani Tabora, NRFA imepeleka chakula katika halmashauri zote saba ambazo ni Tabora, Igunga, Tabora Manispaa, Kaliua, Nzega Mji na Nzega na Sikonge. Lupa alisema juzi walipokea maombi kutoka Halmashauri ya Kongwa mkoani Dodoma.

“Tunaendelea kuhudumia halmashauri zinazoleta maombi ya mahitaji ya chakula kwa wananchi wa kata zao, jana (juzi) tumepokea maombi kutoka Kongwa, leo (jana) nimetuma maafisa wangu kwenda kukagua ili tupeleke chakula huku,” alisema Lupa.

Alisema bei ya mahindi wanayopeleka ni kati ya Sh 600 hadi Sh 900 kwa kilo moja kulingana na umbali na eneo.

“Kwa kifupi hadi sasa tuna chakula cha kutosha na tunaendelea kusambaza chakula maeneo mbalimbali tuliyoletewa maombi na wananchi wenye hali mbaya Kitengo cha Maafa, Ofisi ya Waziri Mkuu hutupa taarifa na sisi tunawapelekea chakula bure,” alisema Lupa.

Alisema awali NFRA ilikuwa na uwezo wa kuhifadhi tani 251,000, lakini uwezo umeongezeka baada ya kujengwa vihenge na maghala katika mikoa ya Manyara, Rukwa na Katavi.

Mtendaji huyo wa NFRA alisema Rais Samia Suluhu Hassan siku chache zilizopita alizindua vihenge na maghala ya kuhifadhia chakula mkoani Manyara yenye uwezo wa kuhifadhi tani 40,000 na vihenge na maghala kama hayo mengine yamekamilika ujenzi wake mkoani Katavi na Sumbawanga-Rukwa.

Alisema kwa jumla yatakuwa na uwezo wa kuhifadhi tani 90,000 za chakula na hivyo kuongeza uwezo wa NFRA wa kuhifadhi chakula kutoka tani 251,000 hadi 341,000.

Lupa alisema maghala hayo ni ya kisasa na yana uwezo wa kukausha mahindi hata yenye unyevu na hivyo kuondoa hatari ya mahindi kuwa na sumu kuvu au kuoza.

Alitaja changamoto kadhaa wakiwamo madiwani na wabunge kutaka NFRA kupeleka chakula hicho nyumba kwa nyumba jambo ambalo haliwezekani. Alisema waliafikiana na viongozi hao NFRA iende kata moja na kukaa siku tatu wakiuza chakula kisha kuondoka na kwenda kata nyingine zenye uhitaji.

Lupa alisema changamoto nyingine ni baadhi ya wanasiasa kutaka kutumia chakula hicho kama tiketi ya kisiasa kwa kutaka chakula kitolewe kwa watu wote wa eneo lao hata kama si walengwa.

Alisema walianza kupeleka mahindi Loliondo kuanzia Julai mwaka huu kutokana na eneo hilo kuwa katika hali mbaya ya athari za ukame zilizosababisha njaa kwa binadamu na baadhi ya mifugo kufa. Kuhusu wilaya za Nachingwea na Liwale mkoani Lindi, Lupa alisema walipeleka mahindi kwa sababu tembo walivamia maeneo hayo na kuharibu mazao yote na kuathiri upatikanaji wa chakula kilichotegemewa.

“Kwa wilaya hizo mbili, halmashauri za maeneo hayo zilituletea jambo hilo la uhitaji na kueleza hali ya maisha ya wananchi hao, na sisi kwa maelekezo tuliuza mahindi kwa bei nafuu ili waweze kupata chakula. Kilo moja tuliuza kwa shilingi 500 na halmashauri ikaongezea shilingi 200 kwa kila kilo ili kuwasaidia wananchi wake,” alisema Lupa.

Habari Zifananazo

Back to top button