Ngoma chanzo cha mabinti kupata mimba – Msambatavangu
DODOMA; MBUNGE wa Iringa Mjini, Jesca Msambatavangu amesema moja ya sababu za wanafunzi katika Halmashuri ya Bagamoyo kutokwenda shule ni kuhudhuria sherehe za ngoma.
Amesema kwa kiasi kikubwa sherehe hizo za ngoma zinakwamisha juhudi za serikali za kuhakikisha kila mtoto anapata haki ya elimu.
Msambatavangu ameyasema hayo leo Novemba 4, 2023 -Bungeni jijini Dodoma wakati akichangia hoja za Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC), Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC) na Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji ya Mitaji ya Umma (PIC).
“CAG anasema watoto wanapata mimba miaka 13 na miaka 11, watoto darasa la saba hawamalizi, tuna wizara ya elimu, tuna maendeleo ya jamii, watoto wanapotea hatuoni?” alihoji na kuongeza
“Zaidi ya asilimia 50 ya watoto wanatoka na divisheni “zero”, wanatoka na divisheni four kwenye Public School (Shule za Umma),” amesema Msambatavangu.
Amesema, ameshangazwa na kila mtu wakiwemo viongozi kulalamika baada ya ripoti ya CAG hivyo amehoji nani atatatua mambo yaliyojitokeza kwenye ripoti hiyo.
Amesema wabunge wanalalamika kwa sababu hawakubaliani na madudu yalijitokeza hivyo amewaomba Mawaziri waende wakasimamie bila kuchekeana kwa kushugulikia madudu yaliyojitokeza kwenye ripoti ya CAG.