Ng’ombe milioni 10 tu wanatutosha kwa sasa

TANZANIA kwa sasa inakadiriwa kuwa na ng’ombe milioni 40 ambao, zaidi ya asilimia 80 ya wanyama hao ni wa kienyeji na wanafugwa kienyeji pia.

Kwa waliotembelea Maonesho ya Wakulima maarufu Nanenane yaliyofanyika kitaifa mwaka huu mkoani Mbeya walijifunza kwamba endapo wafugaji nchi nzima watatumia ng’ombe walioboreshwa, Tanzania itahitaji kuwa na ng’ombe milioni 10 pekee.

Kwamba hao milioni 10, watatupatia kilo za nyama kama zinazopatikiana sasa na kutoa pia maziwa kama yanayozalishwa sasa!

Mohamed Mbogo, Mkurugenzi wa mashamba ya ng’ombe ya Mbogo Ranches yaliyoko Mbarali mkoani Mbeya na Ubena Zomozi, Chalinze, alisitiza hilo na kuonesha kimahesabu wakati akitoa maelezo kwa Makamu wa Rais, Dk Phillip Mpango.

Katika maonesho hayo, shamba la Mbogo lilionesha pia namna ng’ombe wa asili wanavyokuwa na uzito mdogo kulinganisha na walioboreshwa.

Kwa mfano, alionesha ng’ombe wetu wa asili wa miaka miwili akiwa na wastani wa uzito kilo 196 pekee, lakini aliyeboreshwa wa umri huohuo kwa dume la boran akifikia uzito wa kilo 347.

Mbogo alituonesha pia ng’ombe aina ya boran aliyeboreshwa kwa kutumia mbegu ya Sussex, mwenye umri wa miaka miwili, akiwa na kilo 451.

Shamba hilo pia lilileta ng’ombe wa mbegu wa boran wa miaka mitatu mwenye na uzito wa kilo 625. Pia shamba hilo lilileta ng’ombe wa maziwa wanaotoa maziwa maradufu kulinganisha na ng’ombe wa asili.

Katika maonesho hayo, shamba la Mbogo pia lilionesha  aina takribani nne za mbuzi, kuanzia wa asili na walioboreswa huku hata kwa kuangalia kwa macho wale wa asili walionekana wadogo kulinganisha na walioboreshwa ingawa wote wana umri sawa.

Moja ya mbegu ambayo Watanzania wanapaswa kuichangamkia ni mbegu ya Galla-goat ambayo asili yake ni Somalia.

Nilimwona Makamu wa Raia akiguswa vilivyo na maelezo hayo baada ya kutembelea banda la shamba hilo na kuwataka waandishi wa habari kusaidia kuwaeleza wafugaji namna ambavyo wanaweza kunufaika na mifugo  yao kama watabadilika kifikra.

Baadaye nilizungumza na Mohamed Mbogo, akaniambia amekuwa akiwashangaa sana baadhi ya wafugaji wenye makundi makubwa ya ng’ombe wa asili ambao wanaweza kupunguza kwa kuuza na kuanzisha ufugaji wa ng’ombe walioboreshwa na kupata tija kubwa kuliko ilivyo sasa.

Aliniambia kwamba wenzetu katika nchi jirani ya Kenya ambako ndiko walichukua mbegu aina ya boran wamenufaika sana na aina hiyo ya ng’ombe na wafugaji huko wanazidi kubadilika.

Alisema anapendekeza wafugaji wa Tanzania kuchangamkia mbegu hiyo kwa sababu kimsingi ni ng’ombe wa asili aliyeboreshwa.

“Huyu ng’ombe ametokana na ng’ombe wa asili, anavumilia magonjwa na kuchunga malisho yoyote kama ng’ombe wa asili,” aliniambia Mbogo na kuongeza kwamba wakianza na huyo siku moja watafika kwenye aina ya Sussex.

Kuhusu mbuzi alisisitiza wafugaji watapata mafanikio makubwa kwa kuchanganya mbegu na kufanya ufugaji wenye tija na kwamba hilo linawezekana kama wafugaji watabidili mtazamo.

Sisi waandishi wa habari tunaishi kuandika kama hivi. Ni vyema Wizara ya Mifugo na Uvuvi ikune kichwa, ije na mikakati ya kuhakikisha wafugaji wanabadilika na kuendesha ufugaji wa kisasa kwa sababu inawezekana kwa asilimia 100.

Habari Zifananazo

Back to top button