Ng’ombe waondolewe pia kote walikovamia
LEO, ng’ombe 433 waliokamatwa katika eneo la ardhi oevu ya Bonde la Ihefu, ndani ya Hifadhi ya Taifa ya Ruaha wilayani Mbarali wanatazamiwa kupigwa mnada mkoani Mbeya.
Hatua hiyo imekuja baada ya Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa wa Mbeya kwa kushirikiana na Mamlaka ya Hifadhi za Taifa (TANAPA) kufanya oparesheni ili kuondoa zaidi ya mifugo 200,000 iliyovamia eneo hilo.
Mbali na kuhatarisha ikolojia ya Hifadhi ya Taifa ya Ruaha, mifugo inahatarisha pia Mto Ruaha Mkuu.
Akitoa taarifa ya uvamizi wa bonde hilo la Ihefu, Mkuu wa Hifadhi ya Ruaha, Godwell Ole Meng’ataki anasema katika kipindi cha miaka miwili wamekamata mifugo 12,758 katika hifadhi hiyo.
Anasema licha ya kuwatoza faini wafugaji kiasi cha kukusanya zaidi ya Sh bilioni 1.2 katika kipindi hicho, wafugaji wameendelea kurejesha mifugo ndani ya hifadhi.
Mkuu wa Wilaya ya Mbarali, Reuben Mfune anasema eneo lililotengwa kwa ajili ya mifugo katika wilaya hiyo linatosheleza mifugo isiyozidi 60,000, lakini wilaya hiyo ina mifugo zaidi ya 200,000.
Tatizo la mifugo kuvamia maeneo ya misitu haliko Ihefu pekee bali pia maeneo mengi, hasa katika mkoa wa Lindi, Pwani na Morogoro ambayo ina mito muhimu kwa ajili ya kutoa maji ya kunywa na hata mabwawa ya kuzalisha umeme.
Mkuu wa Mkoa wa Lindi, Zainab Telack, aliwahi kueleza namna misitu mingi ya mkoa wake inavyovamiwa na wafugaji, akisema baadhi ya wafugaji walioko Lindi wanazungumza lafudhi sawa na waliomaliza misitu mkoani Shinyanga ambako aliwahi kuhudumu pia kama mkuu wa mkoa.
Telack ambaye wasifu wake ni pamoja kusomea shahada ya uzamili katika maendeleo ya vijiji, Chuo Kkiku cha Sokoine cha Kilimo (SUA) anasema kilimo tunachosema ni uti wa mgongo kitashindikana kama hatutakuwa na misitu kwa sababu kilimo chetu kinategemea mvua na misitu ina nafasi kubwa ya kuvuta mvua na kulinda vyanzo vya maji.
Faida nyingine ya misitu kwa mwanadamu na viumbe hai wengine ni kunyonya hewa ukaa na kutoa hewa safi, kuwa makazi ya viumbe mbalimbali na kutoa miti-dawa.
Misitu huwezesha pia ufugaji wa nyuki, kutoa mbao za aina mbalimbali na nishati za kupikia kama mkaa na kuni na hasa kama vitu hivyo vitavunwa kwa njia endelevu.
Pamoja na kwamba Watanzania wanahitaji mifugo kwa ajili ya nyama na maziwa na pia kutoa ajira, ni wakati wa kuhakikisha wafugaji wanafuga kisasa, wanatumia maeneo waliyopangiwa, wanapunguza idadi ya mifugo na kulima malisho kwa ajili ya mifugo yao. Lazima wabadilike, ‘wahifadhi’ mifugo na si ‘kuichunga’.
Ni muhimu Wizara ya Mifugo na Uvuvi kwa kushirikiana na viongozi wa mikoa mbalimbali kuboresha hali ya ufugaji ili kupunguza pia migogoro ya ardhi. Wahusika wasione kigugumizi kupiga mnada kila mahala ng’ombe walikovamia.