Ngorongoro wanaokwenda nje ya Msomera waongezewa dau

DAR ES SALAAM: KUNDI la pili la wananchi wanaohamia Msomera Wilaya ya Handeni, Tanga kutoka kwenye Hifadhi ya Ngorongoro lilitarajiwa kuhamia jana.

Serikali inahamisha wananchi walio kwenye Hifadhi ya Ngorongoro kwa hiari, kundi la kwanza lililohusisha kaya 551 likiwa na watu 3,010 na mifugo 25,521 lilishahama mapema.

Aidha, kwa wale watakaohamia maeneo mengine mbali na Msomera, serikali itawapa Sh milioni 15 badala ya Sh milioni 10 wanazopewa wanaohamia Msomera.

Wananchi hao pia wanapewa mahindi gunia mbili kwa kila miezi mitatu kwa muda wa miezi 18 kwa kaya.

Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, Msemaji wa Serikali, Mobhare Matinyi alisema awamu ya pili inahusisha kaya 30 yenye watu 224 na mifugo 393.

“Tunaendelea na utaratibu huu kwa sababu tayari kuna wananchi 500 waliojiandikisha kutaka kuhama kwa hiari na 400 tayari washafanyiwa tathmini ya mali zao zilizoko Ngorongoro kwa ajili ya malipo,” alisema Matinyi.

Alisema pia kumekuwa na uhamaji wa watu waliochagua kwenda maeneo mbalimbali ya nchi mbali na kwenda Msomera.

“Kundi la wanaokwenda nje ya Msomera lina kaya 25 watu 172 na mifugo 213, zoezi litaendelea na tunatarajia baada ya hizi zitafuata nyingine, Januari kaya nyingi zitahama sababu kuna nyumba 350 zimekamilika katika eneo hilo tangu Desemba 31, 2023 na ujenzi wa nyumba bado unaendelea, lengo ni kufikisha nyumba 5,000,” alisema.

Akifafanua zaidi, Matinyi alisema serikali inawahamisha wananchi hao kwa hiari kwa sababu wanahakikisha wananchi hao wanakuwa sehemu ya maendeleo ya nchi lakini pia wanapata huduma muhimu za kijamii kwa vile kuishi mbugani kuna vitu vingine hawawezi kuvipata kutokana na kanuni na taratibu zake.

Alisema kwa vile wakazi wa Ngorongoro ni wafugaji, serikali imejenga majosho kwenye makazi mapya Msomera lakini pia inajenga mnada mkubwa wa kisasa na vituo vya kupokelea maziwa kwa wananchi watakaopenda kuuza maziwa katika vituo hivyo.

“Serikali itahakikisha kila mwananchi anayehamia hapo anapata nyumba ya kisasa yenye vyumba vitatu iliyo katika ekari mbili na nusu, hatimiliki ya ardhi na anaongezewa shamba la ekari tano,” alisema.

Matinyi pia alizungumzia mafanikio makubwa yaliyopatikana katika sekta ya afya tangu kuingia madarakani kwa Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan ambapo alisema vifo vya wajawazito na watoto vimepungua kwa kiasi kikubwa huku vitanda vikiongezwa wodini.

Kuhusu treni ya umeme ya kisasa ya SGR, Matinyi alisema itaanza Julai mwaka huu kama alivyoagiza rais kwenye hotuba yake ya kufunga mwaka 2023.

Alisema wanatarajia baada ya hatua za msingi kufanyika huduma zianze na kuongeza: “Reli ya mizigo ikikamilika, Tanzania itakuwa ndio nchi itakayokuwa na reli ndefu kuliko zote Afrika.”

 

 

 

 

 

Habari Zifananazo

Back to top button