NGOs Kigoma zatumia bil  20.4/- utekelezaji miradi

MASHIRIKA yasiyo ya kiserikali (NGOs) mkoani Kigoma yametumia Sh bilioni 20.4 katika kutekeleza miradi ya maendeleo kwa wananchi katika kipindi cha mwaka mmoja uliopita.

Msajili Msaidizi wa mashirika yasiyo ya kiserikali Mkoa Kigoma, Msafiri Nzunuri alisema hayo akitoa taarifa kwa Mkuu wa Mkoa Kigoma, Thobias Andengenye wakati wa mkutano mkuu wa mwaka wa Baraza la Mashirika yasiyo ya Kiserikali (NACONGO) mkoani Kigoma.

Nzunuri alisema katika miradi hiyo ipo ya afya ikiwemo ujenzi wa majengo 15 ya utoaji huduma na vifaa, magari mawili ya kubeba wagonjwa, ujenzi wa zahanati mbili na ukarabati mkubwa wa wodi mbili za wagonjwa kwenye hospitali ya rufaa ya Mkoa Kigoma.

Advertisement

Aidha, alisema kiasi hicho cha fedha kimeweza pia kutekeleza miradi 15 ya maji ambapo tayari miradi mitano inafanya kazi, katika elimu kumekuwa na ujenzi wa madarasa mapya 15 na ukarabati wa madarasa 13 ambapo pikipiki 16 zimetolewa na kugawanywa kwa maofisa ustawi wa jamii kwenye wilaya za Mkoa wa Kigoma.

Akizungumza kwenye mkutano huo, Mkuu wa Mkoa Kigoma, Thobias Andengenye alisema mashirika yasiyo ya kiserikali ambayo hayana uwazi na uwajibikaji yanapoteza imani ya wafadhili na wahisani katika kutoa fedha kugharimia miradi ya maendeleo ya wananchi.

Alisema yapo baadhi ya mashirika yanayoendeshwa kifamilia huku yakitumika kutakatisha fedha, hivyo yamekuwa kikwazo katika utekelezaji wa shughuli za wananchi kutokana na mambo mengi kufanywa kwa faida yao badala ya maslahi ya jamii.

Kwa upande wake mjumbe wa Baraza Kuu la Nacongo, Angelo Tungaraza alisema kuwa mashirika yasiyo ya kiserikali yamekuwa na mafanikio makubwa katika kutekeleza miradi ya maendeleo kwa wananchi.