Nguvu ya mazungumzo ilivyomaliza mgogoro Kariakoo

MKOA wa Dar es Salaam ni moja ya mikoa inayoongoza nchini kwa shughuli mbalimbali za kiuchumi, kijamii na ndio mkoa unaoongoza kwa kuwa na idadi kubwa ya watu ambapo kwa mujibu wa Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2022, una jumla ya watu milioni 5.38 sawa na asilimilia 8.7 ya Watanzania wote.

Kariakoo ni moja ya maeneo maarufu ya biashara, huitambulisha Dar es Salaam ikiwa na takribani wafanyabiashara 35,000 wenye maduka ya kuuza bidhaa mbalimbali na hivyo kulifanya eneo hilo kuwa Soko la Kimataifa kwa nchi nane za Ukanda wa Afrika Mashariki ambazo hufuata huduma katika soko hilo.

Inakadiriwa kwa siku moja mapato yanayopatikana katika biashara eneo hilo ni zaidi ya shilingi bilioni sita fedha ambazo kiasi zinaingia kwenye mapato ya serikali na nyingine zinaendelea kuzunguka kwa wafanyabiashara katika shughuli zao za kila siku.

Si hivyo tu bali Kariakoo ni moja ya chanzo cha mapato ya serikali yatokanayo na kodi na tozo mbalimbali kutoka kwa wafanyabiashara eneo hilo.

Mei 12, mwaka huu, wafanyabiashara katika eneo hilo, kupitia tangazo lao walitangaza kuwepo kwa mgomo wa kutofungua maduka usio na kikomo kuanzia Mei 15, mwaka huu wakitoa sababu kuu tatu za mgomo huo kuwa ni urasimu bandarini.

Sababu nyingine ni Sheria ya Usajili wa Stoo, kamatakamata ya mizigo ya wafanyabiashara inayofanywa na kikosi kazi cha Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) inayosababisha mianya ya rushwa.

Baada ya kutangaza mgomo huo, ulianza kama walivyopanga na juhudi za kuwasihi zilianza kufanywa na aliyekuwa Mkuu wa Mkoa huo, Amos Makalla (amehamishiwa Mwanza), katika siku ya kwanza ya mgomo eneo hilo na kuzungumza na wafanyabiashara hao.

Hata hivyo, juhudi zake hazikuzaa matunda ndipo baadaye alasiri siku hiyo, Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa alifika eneo hilo na kuwasihi wafanyabiashara wafungue maduka huku akitoa maagizo ya kusitisha kikosi kazi cha TRA kuendesha kamatakamata eneo hilo na kuzuia utekelezaji wa sheria ya usajili wa stoo katika eneo hilo.

Katika maagizo hayo aliahidi Mei 17 kufanya mkutano na wafanyabiashara kusikiliza kwa undani changamoto, kero na maoni yao na kisha hatua stahiki zichukuliwe kumaliza mgogoro huo na kuwasihi wafungue maduka ili huduma ziendelee kwani soko hilo linatoa huduma kwa raia wa kigeni pia.

Pamoja na kauli hiyo, baadhi ya wafanyabiashara hawakufungua maduka kwa madai wanasubiri mkutano wajue mwafaka kwanza.

Alfajiri ya Mei 17 wakiwa na shauku ya kumsikiliza Waziri Mkuu kujua mustakabali wa madai yao, wafanyabiashara wa Kariakoo na wawakilishi kutoka mikoa mbalimbali nchini walifurika katika Ukumbi wa Anautoglu kumsubiri kiongozi.

Saa nne kasoro ukumbi ulishajaa na kuomba mkutano ufanywe nje ili kila mmoja asikilize na mkutano ukahamishiwa Viwanja vya Mnazi Mmoja.

Waziri Mkuu, Majaliwa akawasili uwanjani hapo saa nne asubuhi akiwa na watendaji wengine wa serikali, Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Mwigulu Nchemba, Waziri wa Uwekezaji, Viwanda na Biashara, Dk Ashatu Kijaji, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Angellah Kairuki na Waziri wa Mambo ya Ndani, Hamad Masauni.

Majaliwa akatumia takribani saa tano akiwa amesimama kusikiliza kero, changamoto na maoni ya wafanyabiashara lengo likiwa kujua kwa undani kiini cha matatizo na kisha kuyatafutia ufumbuzi.

Majaliwa alitumia njia ya mazungumzo kuhakikisha mgogoro huo unaisha na wafanyabiashara wanarudi kufungua maduka ili biashara ziendelee na hasara ya mabilioni ya fedha isijirudie tena kwa sababu haina tija.

Wafanyabiashara wakapewa nafasi ya kutoa kero zao kwa uwazi, Majaliwa  akisisitiza wasiogope kwa sababu anawalinda na hakuna atakayewadhuru bali kinachoangaliwa ni kujua kiini cha tatizo ili suluhu itafutwe na kero hizo ziishe.

Nguvu ya mazungumzo ikaonekana, wafanyabiashara wakatoa ya moyoni huku wakielezea jinsi kikosi kazi cha TRA kinavyotumia mwanya wa kamatakamata bidhaa za wafanyabiashara kutengeneza mazingira ya rushwa na kusema wamechoka.

Benard Kaduna na Abraham Majembe wakaiomba serikali kupeleka bungeni sheria kinzani ikiwemo ya Usajili wa Stoo ili zifutwe kwa sababu zimekuwa kero kwa mazingira ya biashara nchini.

Walieleza sheria hiyo inataka kila tarehe 15 ya mwezi mfanyabiashara apeleke mchanganuo wa hesabu zake TRA na wanaposhindwa wanatozwa faini ya Dola za Marekani 300.

Kuhusu TRA na kamatakamata mtaani wafanyabiashara hao wamemuambia Majaliwa imetokana na sheria zisizotekelezeka zinazosababisha wafanyabiashara kukwepa kodi na kutoa rushwa kwa baadhi ya maofisa wa mamlaka hiyo na baadhi ya askari wanaofuatilia mizigo kukagua.

Mfanyabiashara wa Kariakoo na maeneo mbalimbali nchini, Fredy Kalelo maarufu kama Vunja bei akazungumzia sheria iliyo mbioni kuanza kutumika ya Deconsolidated na kuomba isitishwe kwanza kwa sababu inataka kila mfanyabiashara anayeagiza mzigo nje aende mwenyewe bandarini kuutoa.

Anasema wafanyabiashara wengi nchini hawana uwezo wa kuagiza mzigo kwa kontena binafsi bali huchangia kontena na wafanyabiashara wengine ili kuwa rahisi kusafirisha.

Mwenyekiti wa wamiliki wa malori madogo na kati ya kusafirisha mizigo, Chuki Shabani akasema kero kubwa ni wataalamu wa kodi kuibua vyanzo vya kodi visivyotekelezeka na kuwakandamiza wafanyabiashara kwa kuweka utitiri wa kodi.

Mwakilishi kutoka Zanzibar, Omar Hussein alisema Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA), upande wa Bara kuna changamoto ya utozaji kodi za kibandari ambazo baadhi ni kandamizi.

Baada ya kusikiliza kero hizo Majaliwa akatoa maagizo saba kwa watendaji wa serikali pamoja na kuunda kamati ya watu 14 ikiwemo wajumbe saba kutoka serikalini na saba kutoka kwa wafanyabiashara.

Kamati hiyo imepewa kazi ya kupitia kero zote zilizowasilishwa katika mkutano huo na kuangalia zinazotekelezeka na zile zisizotekelezeka na kuzipatia ufumbuzi na kuzunguka katika masoko nchini kuchukua kero kwa wafanyabiashara wengine.

Mbali na hayo, Majaliwa akatoa maagizo saba yakiwemo kuvunja vikosi kasi vyote vinavyofanya operesheni Kariakoo kwa wafanyabiashara na kusema kodi itakusanywa na maofisa wa TRA.

“Tuna maofisa wetu wa TRA waliosomea kazi ya kukusanya kodi tuwatumie hawa ili wanapokosea tuwaadhibu kwa kukiuka maadili,” anasema Majaliwa.

Pia amepiga marufuku askari polisi kukagua risiti za mizigo ya wafanyabiashara kwa kuwa kazi yao ni kulinda watu na mali zao na watakagua watakapopewa kibali cha kufanya hivyo. Kuhusu tozo za usajili wa stoo, ameagiza kusitishwa kutumika kwa kanuni za kutekeleza sheria hiyo ili ziangaliwe upya.

Kupitia mazungumzo hayo ikawa njia ya suluhu, kwani baada ya kusikiliza kero ya wafanyabiashara kukamatwa na kupelekwa kwenye maghala, Majaliwa akawataka wafanyabiashara ambao mizigo yao imekamatwa wakutane na kamati aliyounda ambayo ina wajumbe kutoka TRA waangalie njia nzuri ya kumaliza iachiwe.

Katika kero zao, wafanyabiashara wakamwambia Majaliwa kuwa maagizo yanayotolewa na viongozi wa ngazi za juu serikalini, akiwemo rais na wengine hayatekelezwi na watendaji na wanadai ni kauli za kisiasa.

Majaliwa akajibu hilo, akawataka watumishi wa serikali kutekeleza maagizo yote ya viongozi wakuu wa serikali, rais, makamu wa rais, waziri mkuu, Rais wa Zanzibar na kamwe  isijirudie kauli kwamba agizo la viongozi ni la kisiasa.

Hoja kuhusu wafanyabiashara kuchangia usafirishaji wa mizigo kwenye kontena moja, amewaagiza TRA kuangalia utaratibu wa kila mwenye mzigo ndani ya kontena hilo kutambulika katika kodi iliyolipwa ili wasibughudhiwe.

Katika kero ya sheria kinzani, Majaliwa ameagiza Wizara ya Uwekezaji, Viwanda na Biashara kuchukua sheria zote zinazokinzana na kuziwasilisha zifanyiwe marekebisho ili kuondoa changamoto.

Katika madai ya rushwa inayochukuliwa na watumishi wa serikali kwa wafanyabiashara hao, Majaliwa amekemea vitendo hivyo na kusema vina athari kubwa kwa taifa na havitoi tafsiri halisi ya maisha ya baadaye.

Mazungumzo na hatua zilizochukuliwa na Majaliwa zikafungua na kurejesha tena imani ya wafanyabiashara hao kwa serikali na hapo wakatangaza kuacha mgomo na kufungua maduka kuendelea na biashara huku wakitegemea kupata mrejesho wa kamati iliyoundwa kushughulikia kero hizo.

Habari Zifananazo

Back to top button