Nguvu ya pamoja yatakiwa maadili kwa watoto
MKUU wa Wilaya ya Nyang’hwale mkoani Geita, Grace Kingalame amewataka wazazi au walezi kuunganisha nguvu na walimu wa watoto wao shuleni ili kuhakikisha wanaimarisha maadili ya watoto.
Kingalame ametoa kauli hiyo kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Geita wakati akizungumuza na wazazi na wanafunzi waliohitimu darasa la saba na kidato cha nne katika shule za Royal Family mjini Geita.
Amesema kwa kipindi hiki hivi kuna wimbi kubwa la mmomonyoko wa maadili na hivo makundi yote ya kijamii ikiwemo wazazi, viongozi na walimu wanapaswa kuwajibika kwani suala la maadili ni mtambuka.
“Lengo kubwa ni kumulinda mtoto wa kitanzania, lengo kubwa ni kuondoa ukatili kwenye jamii yetu, kwa hiyo tukishirikiana kwa pamoja, tukiibua uovu bila kuoneana aibu, tunaweza kupiga hatua.”
Amewataka wazazi na walezi kuiunga mkono serikali kwa kuhakikisha wanapeleka watoto shule kwani elimu inatolewa bure kwenye shule za umma na hakuna sababu ya kumwachisha mtoto shule.
“Mzazi ambaye anafanya kwa kusudi kukatisha masomo ya mtoto wake huyo anatuchokoza tu, ni kwamba kila mzazi apelike mtoto shule na hili sasa siyo ombi ni kwamba peleka mtoto shule.”
Mkurugenzi wa Taasisi ya Royal Family, Mhandisi Lazaro Philipo amesema shule zake zinaunga mkono suala la maadili ya watoto kwa kuimarisha usimamizi na kuongeza elimu ya kidini kwa watoto wote.
“Maadili ndiyo kila kitu, huwezi kuwa na elimu bora, ukiwa na maadili mabovu haisaidii, kwetu sisi kama Royal Family hicho ndicho uti wa mgongo wetu, kwama mwanafunzi anaposoma awe na maadili.
“Tunaamini kwamba maadili yanaanza na hofu ya Mungu, pasipo kuwa na hofu ya Mungu siyo rahisi kuwa na maadili kwa sababu mtoto lazima awe na hofu kwamba ninapofanya hivi Mungu hapendi.”
Amesema shule imejipanga kudhibiti mabadiliko ya nyendo za watoto hasa wanapoingia rika barehe kwa kusimamiwa na walezi wao kuwapa elimu pamoja na kuwapa elimu ya kidini.
Mmoja ya wazazi, Vicent Ntale amekiri shule zinazowekea mkazo elimu ya dini zinawasaidia wazazi kwani mtoto anakua akiwa na elimu ya kawaida sambamba na elimu ya dini .