DAR ES SALAAM: MFUKO wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) umetangaza kuboresha kitita cha huduma na bei ikiwemo kuongeza dawa mpya 247 ambazo hazikuwepo tangu kupitishwa kwa kitita hicho miaka nane iliyopita mnamo 2016.
Lengo ni kufikia mahitaji ya wanachama kwa kuzingatia hali halisi ya sasa.
Hayo yameelezwa leo na Mkurugenzi wa NHIF, Dk Bernard Konga katika mkutano na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam kuelekea miaka 24 ya utoaji huduma wa mfuko huo na kusema kuwa mabadiliko ya kitita hicho yamezingatia tafiti za kisayansi nchi nzima.
–
“Hatujabadilisha gharama ama ada ya mwanachama kujiunga na mfuko wa NHIF. Tulichoboresha ni malipo ya NHIF kwa watoa huduma kwa niaba ya mwanachama,” amesema Mkurugenzi huyo.
Amesema kitita hicho kitaanza kutumika kuanzia Machi mosi, 2024 na kimegusa maeneo makuu matatu, mosi, huduma ya usajili, ushauri na wakati wa kumwona daktari, pili huduma ya dawa na eneo la tatu na mwisho ni huduma za upasuaji na vipimo
Kiongozi huyo amesema wapo mbioni kuanza kutoa huduma ya Bima ya afya kwa wote kupitia Sheria mpya iliyosainiwa na Rais Samia Suluhu Hassan mwezi Novemba, 2023.
“Tutapita kutoa elimu kanisani, mskitini mashuleni na maeneo mengine. Kwakuwa Serikali imeamua kumkomboa mwananchi ni lazima kuwe na Bima ya afya kwa wote.” Amesema kiongozi huyo.