NHIF yaleta unafuu gharama za matibabu

DAR ES SALAAM: MFUKO wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) umeboresha huduma za kitita cha mafao na kuleta unafuu kwa mwananchi katika gharama za ushauri, dawa na matibabu yakiwemo ya kuchuja damu na upasuaji. Kwa mfano katika eneo la kuchuja damu, gharama ya kufanyiwa haemodialysis ni Sh 240,000 lakini bei iliyoboreshwa ni Sh 200,000.

Akizungumza na wahariri wa vyombo mbalimbali vya habari nchini katika semina iliyofanyika Dar es Salaam kuhusu maboresho ya kitita hicho, Mkurugenzi Mkuu wa NHIF, Bernard Konga alisema lengo ni kumfikia mwanachama alipo kwa huduma bora zaidi na kitita kipya kitaanza kutumika Januari, 2024.

Konga alisema gharama hizo hazimgusi mwanachama bali ni kati ya NHIF na watoa huduma ili kuboresha zaidi huduma karibu na wananchi. Alitaja maeneo muhimu yaliyofanyiwa maboresho ili kuleta unafuu huo wa gharama ni ada ya usajili na ushauri wa daktari; huduma za dawa na tiba za upasuaji na vipimo.

Advertisement

Akifafanua eneo la upasuaji, alisema upasuaji wa kidole tumbo kwa gharama ya sasa ya mfuko ni Sh 110,000 na bei iliyoridhiwa ni Sh 150,000 huku upasuaji wa henia ukiwa Sh 150,000 kutoka Sh 110,000. Kuhusu huduma za kuchuja damu, Konga alisema kufanyiwa haemodialysis bei ya sasa ni Sh 240,000 lakini bei iliyoboreshwa ni Sh 200,000.

Katika eneo la ada ya usajili na ushauri wa daktari, Konga alisema kwa sasa bei kwa daktari bingwa mbobezi ngazi ya hospitali ya rufaa ngazi ya taifa na kanda ni Sh 35,000 na bei mpya ni Sh 25,000 na daktari bingwa ni Sh 20,000 kutoka Sh 25,000 huku daktari wa kawaida bei mpya ni Sh 5,000 kutoka Sh 10,000.

1 comments

Comments are closed.