Ni jambo la kutia moyo DRC kushirikiana na Uganda, Burundi kukabili waasi

KWA muda mrefu Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) imekuwa ikilalamikia mataifa jirani zake kuwa badala ya kusaidia katika utatuzi wa mgogoro, yanachangia katika mgogoro wake na makundi ya waasi katika eneo la Mashariki.

Miongoni mwa mataifa yaliyotajwa kuwa ni wachochezi wa mgogoro huo ni pamoja na Uganda na Burundi ambayo yalikuwa yakituhumiwa kusaidia moja ya makundi ya waasi kwa kuyapa silaha na pia wakati mwingine kushiriki moja kwa moja kwa upande wa waasi.

Vyombo mbalimbali vya habari ndani na nje ya DRC wiki iliyopita viliripoti kuhusu makubaliano yaliyofikiwa kati ya Serikali ya DRC kwa nyakati tofauti na nchi za Uganda na Burundi kwa ajili ya ushirikiano kijeshi katika kufanikisha mapambano dhidi ya waasi.

Advertisement

Hizi ni habari njema kwa wapenda amani popote pale duniani ambao walikuwa wakiwahurumia wananchi wa DRC waliokuwa wakiteseka na vita visivyokuwa na sababu yoyote.

Ni dhahiri ushirikiano huo ni mwanzo wa kumalizika kwa uasi ndani ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo kwa kuwa nguvu ya mapambano dhidi ya makundi ya waasi itakuwa kubwa na sio vita ya DRC peke yake.

Ushirikiano wa kijeshi kati ya DRC na Uganda maana yake ni kuwa utakuwa ni mwisho wa makundi yaliyokuwa yakitumia kutoelewana kwa Uganda na DRC kufanya mashambulizi katika vijiji vya mikoa ya Mashariki.

Maana yake ni kwamba nguvu iliyokuwa ikitumiwa na DRC kupambana na makundi ya waasi itakuwa kubwa kwa kuwa itashirikisha nguvu na vikosi vya nchi nne kutoka Afrika Mashariki yaani majeshi kutoka Kenya, Uganda, Burundi na Jeshi la DRC lenyewe hivyo kuwanyima nafasi waasi hao ya kujificha.

Ushirikiano huu pia unamaanisha kuwa upitishwaji wa silaha kutoka nje ya DRC kuelekea katika eneo la Mashariki mwa DRC utakuwa mdogo kwa kuwa njia zilizokuwa zikitumika kupitisha silaha sasa zitakuwa katika udhibiti wa washirika wa DRC kitu kitakachokuwa msaada mkubwa kwa DRC.

Naamini kama Uganda na Burundi ambazo zilikuwa zikilalamikiwa, sasa zimekuwa rafiki wa DRC, nchi zingine zinazotajwa katika mgogoro huo zitakuwa rafiki wa DRC na kujiunga pamoja katika kupambana na waasi wanaosumbua wananchi katika nchi yao na kuwakosesha amani huku wengine wakikimbia makazi yao.

Kutokana na ushirikiano huo wa kijeshi, mataifa mengine yanayopakana na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo yaimarishe ushirikiano ili kuwezesha mapambano dhidi ya waasi yawe rahisi na hatimaye kuiwezesha DRC kuwa na amani na utulivu.