RAIS wa zamani wa Nigeria, Goodluck Jonathan amewaomba wananchi wa Nigeria kujifunza kwa ndugu zao wa Rwanda namna bora ya kujenga nchi katika umoja na mshikamano na kuepuka ukabila ambao athari yake kubwa ni kusambaratisha umoja wa kitaifa.
Jonathan aliyasema hayo mwishoni mwa wiki wakati akitoa salamu za pongezi katika sherehe za kutimiza miaka 80 ya Chifu wa Owerri katika Jimbo la Imo, Emmanuel Iwuanyanwu ambapo aliwataka wananchi wa Nigeria kuiga kile kilichofanywa na wananchi wenzao wa Rwanda katika kukabiliana na changamoto za kitaifa.
“Wananchi wa Nigeria tuone vile Wanyarwanda walivyokabiliana na changamoto za kitaifa na kufanikiwa kujenga umoja na mshikamano wa taifa. Katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2023, tuchague kuushinda ukabila ambao unaiyumbisha Nigeria hadi leo,” alisema Jonathan katika hotuba yake.
Alisema baada ya mauaji ya kimbari wananchi wa Rwanda waliamua kujenga taifa lao ili kuondokana na ukabila uliowaletea matatizo hayo, na kuongeza kuwa leo hii ukabila Rwanda si kitu tena, na kwamba wanajiona wote kama wamoja.
“Hapa kwetu tumeijenga siasa yetu katika mikono ya ukabila hali inayosababisha kushindwa kuwa na taifa moja lililoshikamana. Vijana mnatakiwa kuangalia kesho yenu na ya watoto wenu, mkiamua kuwarithisha watoto wenu taifa lililoshikamana na lenye umoja bila kujali ukabila, mtakuwa mmeandika historia ambayo haitawasahau,” aliongeza Jonathan.