‘Ningekuwepo kwenye ajali iliyomuua Sokoine’
EO ni Aprili 12, 2024, ni miaka 40 tangu Waziri Mkuu wa Tanzania, hayati Edward Moringe Sokoine afariki kwa ajali ya gari mkoani Morogoro.
Miongoni mwa watu wanaoikumbuka sana siku hii ni mwanasiasa mkongwe nchini Hamad Rashid Mohamed, ambaye anasema naye ilikuwa awepo katika safari hiyo ya Aprili 12, 1984 iliyosababisha kifo cha Sokoine.
Hamad aliyewahi kuwa Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Waziri wa Afya wa Zanzibar, lakini sasa akiwa ni Mwenyekiti wa cha cha kisiasa cha ADC, anasema siku nne kabla ya ajali hiyo Sokoine alimuagiza aende Zanzibar.
“Siku nne kabla ya ajali ile, aliniagiza (hayati Sokoine) niende Zanzibar kuchukua paper iliyowasilishwa BLM (Baraza La Mapinduzi) na Wizara ya Biashara iliyotoa idhini ya Wazanzibari walioko nje kuingiza bidhaa na kuja kufanya shughuli zao. Mzee Mwinyi alisema “Zanzibar ni njema atakaye aje”.
“Baada ya kumpelekea (Sokoine) wasilisho Dodoma nikiwa katika nafasi ya Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani na Muwakilishi wa Baraza Mapinduzi, hayati Sokoine akaniambia tukimaliza Bunge, mimi na wewe moja kwa moja twende kwa Mwalimu (Nyerere) tukamshauri tuitekeleze hii sera, ili na Watanzania Bara waweze kuwaletea misaada ndugu zao na kufanya shughuli zao za kibiashara ili kupunguza upungufu wa bidhaa. (Hayati Sokoine) akitaka niingie kwenye gari lake.
“Usiku wake kabla ya safari nikapata taarifa ya kuugua sana baba yangu, Sheikh Rashid Mohamed kisiwani Pemba, hivyo ikanilazimu kwenda Pemba kwanza kwa helikopta kumchukua baba kumleta Muhimbili (Hospitali ya Taifa). Nafika Pemba, yeye (Sokoine) akapata ajali.
“Nikamchukua baba na kuwahi Dar (jijini Dar es Salaam). Leo kwangu ni siku nzito kwa kukumbuka tulivyokuwa karibu na hayati Sokoine. Mungu atupe mwisho mwema. Aamin,” amesema Hamad Rashid.