Nipo tayari kuvaa viatu vya Bocco- Waziri Jr
DODOMA: Mshambuliaji wa KMC Waziri Junior amesema yupo tayari kuvaa viatu vya mshambuliaji mkongwe John Bocco na kufanya yale aliyokuwa akifanya mchezaji huyo wa Simba.
Ametoa kauli hiyo wakati akizungumzia maandalizi ya mchezo wa Ligi Kuu dhidi ya Dodoma Jiji utakaopigwa kesho Uwanja wa Jamhuri mkoani Dodoma ambapo amesema yeye ni moja wa washambuliaji watakaorithi mikoba ya Bocco huku akiwataka washambuliaji wengine kuhifadhi takwimu zao.
Mpaka sasa Waziri amefunga mabao 50 kwenye Ligi Kuu akiwa amehudumu kwenye vilabu Saba katika misimu 9 aliyocheza kwenye ligi hiyo namba sita kwa ubora Afrika.
Nyota huyo mwenye mabao 11 kwenye ligi msimu huu amesema idadi ya mabao aliyofunga yanampa kila sababu ya kuamini kuwa ana uwezo wa kuvaa viatu vya Bocco na kusisitiza kuwa anaheshimu makubwa aliyoyafanya akiwa Azam Fc na Simba pamoja na Taifa Stars.