Nishati safi ndio mpango mzima

Waziri wa Nishati,January Makamba akipata maelezo ya mkaa mbadala uliokwishakamilika

MPANGO wa serikali ni kuhakikisha asilimia 80 ya Watanzania wanatumia nishati safi ya kupikia mpaka ifikapo mwaka 2033.

Tayari mikakati imeshaanza na kwa kuanzia Waziri wa Nishati Januari Makamba, amegawa mitungi 100 ya gesi kwa kila mbunge lengo likiwa ni kuhamasisha wananchi wao juu ya matumizi ya nishati safi ya kupikia.

Katika maonesho ya wiki ya nishati Dodoma hivi karibuni, Waziri Makamba alisema wabunge watatakiwa kugawa mitungi hiyo hadharani huku wakitoa maneno ya hamasa kwa wananchi wao.

Advertisement

“Hiyo ni bajeti ya serikali kwa wabunge ili wakahamasishe wananchi wao kwenye matumizi ya nishati safi ya kupikia… kwenye majimbo yao huko kuna baba lishe, mama lishe, wabunge wanatakiwa kuigawa mitungi hiyo hadharani na kutoa maelekezo ya hamasa kwa wananchi wao,” anasema Makamba.

 

Takwimu zinaonesha kuwa, asilimia nane tu ya Watanzania ndio wanaotumia nishati safi hivyo Rais Samia Suluhu Hassan ametoa maelekezo ndani ya miaka 10 asilimia 80 ya Watanzania watumie nishati safi ya kupikia.

“Rais Samia ametuelekeza tutengeneze dira, mikakati na mwelekeo na pia kuanzisha mfuko wa nishati safi ya kupikia ili kuweka ruzuku itakayowawezesha wananchi wa kipato cha chini kumudu bei ya gesi, hii ni kazi kubwa lakini inawezekana na kazi inaendelea,” anasema Makamba.

“Serikali ya Awamu ya Sita imeamua kulivalia njuga suala la nishati safi ya kupikia ikiwa ni moja ya jitihada zake za kuboresha maisha ya Watanzania hasa kinamama… tutapambana kuhakikisha mama anatumia nishati safi,” ameongeza Makamba.

Matumizi ya nishati chafu kama kuni, mkaa athari zake ni kubwa ikiwemo magonjwa katika mfumo wa upumuaji, mazingira hatarishi wakati wa kutafuta kuni, wanyama hatarishi na athari katika masomo kwa watoto wa kike kwani badala ya kutumia muda mrefu kusoma, muda mwingi wanautumia kutafuta kuni kwa ajili ya kupikia.

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa anasema serikali imejipanga vizuri katika kuhamasisha wananchi watumie nishati safi na kwamba wameshafanya kikao cha ndani na hivi karibuni watakuwa na kikao kikubwa cha taifa kwa kushirikiana na Zanzibar juu ya uhamasishaji kwa wananchi katika matumizi ya nishati safi.

“Wizara ya nishati kwa pamoja na ofisi ya makamu wa rais na kwa maelekezo ya kiongozi wa nchi, tumeunda kamati ya kitaifa inayoratibu utoaji elimu, lakini pia kuonesha fursa na wajasiriamali ambao watahitaji kuingia kwenye sekta hii lakini hasa kuhamasisha Watanzania wabadilike na kuwa kwenye matumizi ya nishati mbadala,”.

Waziri Mkuu anasema, mikakati ya serikali ni kuanza na taasisi ya elimu kupitia wanafunzi kwenye shule za bweni, jeshini na kwenye makambi mbalimbali.

“Mahali pote kwenye mkusanyiko wa watu zaidi ya 100 basi kuwe na matumizi ya nishati mbadala,” anasema.

Waziri Mkuu anasema huo ndio muelekeo wa taifa na kwamba wale waliokwishapata elimu hiyo waisambaze kwa wengine.

“Nchi bado inahitaji teknolojia ya nishati safi hivyo wadau na wataalamu jaribuni kubuni nishati mbadala kwa manufaa ya Watanzania.”

Kila mmoja anona umuhimu wa nishati safi ya kupikia, Spika Dk Tulia Ackson anapongeza jitihada zilizofanyika za kutumia wabunge katika kuhamasisha wananchi wao katika matumizi hayo.

Anasema Wabunge ni watu sahihi kwasababu wana ushawishi mkubwa kwa wananchi wao hivyo anaamini jambo limefika mahala pake na lengo litatimia.

“Hawa wabunge ni watu sahihi kuwapa hiyo kazi ya kuhamasisha kwa sababu wanawafikia watu wengi na wana ushawishi huko kwenye majimbo yao niwaombe watu mbalimbali wakiwemo waandishi muunge mkono juhudi hizo,” ameongeza Spika.

Baada ya kutembelea mabanda ya maonesho ya nishati kwenye viwanja vya Bunge, Spika anafurahishwa na ubunifu kwenye nishati mbadala ya kupikia na kwamba hata wanaopenda kutumia mkaa wametengenezwa mazingira bora.

“Naamini huko baadae tutafikia sehemu ambayo hatutatumia mkaa kabisa na hata kama tutatumia basi utakuwa mbadala ambao hautaharibu mazingira,” anasema Dk Tulia Ackson.

Katika harakati za kutumia nishati safi, serikali haipo peke yake, mdau wa nishati safi, Leonard Kushoka tayari ana kiwanda kinachojishughulisha na utengenezaji wa mashine za mkaa mbadala cha Kuja na Kushoka kilichopo Tabora.

Kushoka aliwahi kuibuka mshindi kwenye shindano la kubuni utengenezaji wa  mkaa mbadala kitaifa na kupata sh milioni 300.

“Shindano lile ndio limefanya Wizara ya nishati waniite, mazingira waniite… nina zaidi ya tani 300 za mkaa mbadala ziko stoo… nawaambia Watanzania kitu hiki kinawezekana,” anasema.

“Tunajishughulisha na utengenezaji wa mashine za mkaa mbadala, mafunzo kwa jamii jinsi ya kuuzalisha na kuhamasisha matumizi ya mkaa mbadala.”

Anasema hiyo ni nishati ya kupikia inayokwenda kuwa mbadala wa mkaa akitumia mabaki ya mazao mbalimbali.

“Miti ukiikata unakwenda kuchoma mkaa, unapata nishati ya kupikia, kwa kawaida kazi kubwa ya miti ni kuvuta hewa yenye simu na kutoa hewa safi, kwa hiyo mtu anaekata mti na kwenda kuchoma mkaa anakata kitu kilichohifadhi sumu muda mrefu, kwa vyovyote italeta madhara,”.

Anasema ndio maana watu wanaotumia mkaa wanashauriwa kutumia eneo la wazi ili ile sumu isije kumdhuru.

“Sasa sisi tunatengeneza mkaa mbadala kupitia mabaki ya vyakula, je chakula kina sumu? Hakina, hatua ya kwanza ni kukusanya mabaki ya vyakula na kuchoma… haya mafunzo tunayatoa bure lakini kwa watu wanaonunua mashine zetu.”

Anasema watu wanalima mahindi na mazao mengine wanapovuna, yale mabaki wanayatupa, lakini kama wangekuwa wana elimu juu ya utengenezaji wa mkaa mbadala wangetengeneza.

“Kwa msisitizo wa serikali, tunaamini sasa somo hili litaeleweka na Watanzania wengi watajifunza namna ya kuteneza mkaa mbadala.”

“Takwimu zinaonesha kuwa watu wanaokata miti na kuchoma kienyeji wanakata tani 10 hadi 12 za miti kupata tani moja ya mkaa na anaezalisha mkaa mbadala anatumia tani tatu za takataka kupata tani moja ya mkaa… unaona kiwango kikubwa kinachookolewa endapo teknolojia ikitumika.”

“Natamani wabunge wahamasike kununua mashine na kupelekea vijana wao majimboni kwa sababu hii mashinde ukinunua ni kiwanda tosha na watu wanajiajiri.”

Anasema soko lake kubwa la mkaa mbadala lipo Dar es Salaam na hasa kwa mama ntilie walio stedi ya mabasi ya Magufuli.

“Gunia la mkaa Dar es Salaam ni sh laki moja sasa kwanini nihangaike kuuza mkaa Tabora wakati gunia ni sh elfu 10?”

Anasema Dar es Salaam inatumia zaidi ya asilimia 50 ya mkaa wa Tanzania, hivyo ukiiokoa Dar es Salaam na matumizi ya nishati chafu utaikoa sehemu kubwa ya nchi.

Mdau huyo anaamini mambo yatakuwa sawa na siku moja Watanzania wataachana na matumizi ya nishati chafu na kila mmoja atatumia nishati safi.

1 comments

Toa Jibu

Barua-pepe haitachapishwa. Fildi za lazima zimetiwa alama ya *