NIT yakutanisha wadau sekta ya Usafirishaji
DSM: KATIKA kuboresha sekta ya usafirishaji nchini Serikali kupitia chuo cha usafirishaji NIT kwa mara ya kwanza kimeandaa mkutano wa Kimataifa wa kujadili namna bora ya usambazaji na usafirishaji ambao umewakutanisha watafiti kutoka nchi mbalimbali ili kuifanya sekta hiyo kukua zaidi kwa manufaa makubwa ya Taifa.
Akizungumza wakati akifungua mkutano huo Waziri wa Uchukuzi Prof.Makame Mbarawa amesema serikali imewekeza katika miradi mbalimbali na ili iweze kuendelea lazima kuwepo wataalamu mahususi wa uendeshaji hivyo kutokana na mkutano kutaleta matokeo chanya ya kuongeza wataalamu katika sekta ya usafiri.
Aidha amesema nchi yoyote haiwezi kuendelea kama haina sekta mahiri ya usafirishaji na kwamba mkutano huo ni muhimu huku akiwasisitiza wataalamu kutoka nchi mbalimbali kuwafundisha watanzania mbimu bora za usafirishaji.
Mkuu wa chuo cha usafirishaji NIT Mhandisi Zacharia Mganilwa amesema Mkutano huo unaenda kutoa takwimu zitakazowafanya wanaoendesha mashirika ya uchukuzi kuwa bora zaidi na kuleta utendaji wenye tija kwa matumaini makubwa ya serikali ilivyowekeza katika sekta hiyo.
Nae mmoja wa washariki katika mkutano huo Mkurugenzi wa Uthibiti Uchumi Mamlaka Ya Usafiri wa Anga TCAA Daniel Malanga amesema changamoto kubwa iliyopo katika sekta ya usafirishaji ni upungufu wa watalaamu hususani wahandishi na mkutano huo ni muhimu kupeana ujuzi zaidi.
Mkutano huo umehudhuriwa na watafiti wa usafiri kutoka Uingereza ,Marekani ,Austaria na nchi nyingine nyingi na utadumu kwa siku tatu kuanzia leo oktoba 18 hadi oktoba 20.