Njaa yamkamatisha mtuhumiwa wa mauaji

Jeshi la polisi mkoani Kagera linamshikilia Paschale Kaigwa (21), mkazi wa Kata Kishogo Halmashauri ya Bukoba kwa tuhuma za mauji ya Hadija Ismail (29) mke wa Mwenyekiti wa Mtaa wa NHC, Kata ya Rwamishenye Manispaa ya Bukoba.

Kaigwa anatuhumiwa kumuua Hadija Februari 13 mwaka huu kisha kukimbia kusikojulikana, ambapo Jeshi la polisi kupitia vyombo vya habari na mabango lilisambaza picha ya mtuhumiwa na kuwaomba wananchi kutoa ushirikiano wa kumkamata na kumfikisha katika vyombo vya sheria.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kagera William Mwampaghale alisema mtuhumiwa alikamatwa Februari 19, 2023 Mtaa wa Katatolwanso, Kata kashai, Bukoba ambapo alienda kuomba chakula kwa shangazi yake, baada ya kujificha vichakani tangu kutokea kwa tukio.

Alisema kuwa mtuhumiwa alipofika kwa shangazi yake majira ya saa 10 jioni aliwakuta watoto wa shangazi yake, ambao walipiga kelele kutokana na kuona picha yake ikitafutwa katika vyombo vya habari na majirani walifika na kumkamata kwa ushirikiano wa polisi.

Kaigwa alikuwa akisaidia kazi za nyumbani kwa marehemu Hadija Baada ya kuokotwa na mumewe, ambaye Ni mwenyekiti wa mtaa mnamo Novemba mwaka 2022, baada ya kumuona akiishi mtaani na kudai kuwa hana makazi ya kuishi.

Habari Zifananazo

Back to top button