HIVI karibuni, Tanzania itafanya uzinduzi wa Programu ya Kutathmini Viwango na Usalama wa Barabara (Tanzania Roads Assessment Program-TanRAP), ikiwa ni taifa la kwanza Afrika Mashariki kuwa na programu hiyo.
Programu hii inalenga kupunguza madhara yanayotokana na ajali za barabarani kwa kuimarisha usalama wa barabara. Licha ya kuwa na mchango mkubwa katika kuchangia ajali za barabarani, tatizo la miundombinu isiyo salama limekuwa halitiliwi mkazo tofauti na ilivyo upande wa vyombo vya usafirishaji na hata watumiaji wake.
Uzinduzi wa programu hii, unatarajiwa kuiweka Tanzania katika mazingira mazuri zaidi katika kufanikisha lengo namba tatu na nne kati ya malengo 12 ya dunia ya kupunguza madhara yanayotokana na ajali za barabarani. Malengo haya ni sehemu ya Mkakati wa Muongo wa Pili wa Dunia (2021-2030) wa kuchukua hatua ili kuimarisha usalama barabarani na kupunguza madhara yatokanayo na ajali za barabarani kwa wastani wa asilimia 50 ifikapo mwaka 2030.
Kwa mujibu wa waraka kuhusiana na mkakati huo, lengo namba tatu linatoa maelekezo kwa nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa (UN), kuhakikisha kuwa barabara zote mpya zinajengwa kwa kiwango cha nyota tatu na zaidi, huku lengo namba nne likizitaka nchi hizo kuhakikisha ifikapo mwaka 2030, zaidi ya asilimia 75 za safari za watumiaji wote wa barabara zinafanyika kwenye barabara zenye nyota tatu au zaidi.
TanRAP ni nini?
Hii ni programu ambayo itajikita katika kufanya tathmini za viwango vya kiusalama vya barabara zilizoko nchini ili kubaini vitu vyote ambavyo ni visababishi vya ajali za barabarani au vinavyochangia ukubwa wa madhara ya baada ya tukio la ajali. Programu itajikita katika kutathmini barabara ambazo zimeshajengwa na zile ambazo bado ziko katika hatua ya kubuni, lengo likiwa kuzifanya barabara hizo kufikia viwango vinavyopendekezwa kimataifa.
Ni programu ya kitaifa ambayo itakuwa chini ya Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi, huku ikiendeshwa kupitia Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS), Wakala wa Barabara za Mijini na Vijijini (TARURA) kwa kushirikiana na taasisi na mashirika mengine wadau wa usalama barabarani, yaliyo na yasiyo ya serikali. Programu hii kwa kiasi kikubwa inatarajiwa kuendeshwa kutokana na vyanzo vya ndani vya mapato.
TanRAP inatokea wapi?
Katika kufanikisha utekelezaji wa mkakati wa UN wa kuimarisha usalama barabarani, Jumuiya ya Kimataifa imekuwa ikibuni miradi na kuielekeza sehemu mbalimbali. Miongoni mwa miradi hiyo ni ule wa Hatua 10 za Kuimarisha Usalama Barabarani na Miundombinu yake (Ten Step Plan for Safer Roads Infrastructure), mradi ambao umebuniwa na kundi la Ushirikiano wa Usalama Barabarani la Umoja wa Mataifa (United Nations Road Safety Collaboration Group) na Tanzania kubahatika kuwa nchi ya kwanza kwa mradi huu kutekelezwa kwa ajili ya majaribio.
Mradi huo wa miezi 36 wa Hatua 10 za Kuimarisha Usalama Barabarani na Miundombinu yake umekuwa ukitekelezwa nchini kuanzia mwaka 2020 na Kamisheni ya Uchumi ya Umoja wa Mataifa kwa Afrika (United Nations Economic Commission for Africa-UNECA) wakishirikiana na International Road Federation (IRF), International Road Assessment Programme (iRAP), World Road Association (PIARC) na Tanzania Road Association (TARA) kwa ufadhili wa Mfuko wa Umoja wa Mataifa wa Usalama Barabarani (UNRSF), Global Road Safety Facility (GRSF) na UKAid.
Moja ya malengo ya mradi huu, ni kuwajengea uwezo wataalamu wengi wa ndani ili ushiriki wao kwenye miradi iliyopo na itakayobuniwa ya kuimarisha usalama barabarani, uwe ni wenye tija zaidi. Kupitia mradi huu, Watanzania zaidi ya 300 wamepata mafunzo mbalimbali yaliyoandaliwa na mradi.
Mafunzo hayo ni pamoja na Uhandisi wa Usalama Barabarani (Road Safety Engineering), Ukaguzi wa Usalama Barabarani (Road Safety Audit) na utathmini wa usalama barabarani kwa kutumia mbinu za iRAP. 20 kati yao wakifanikiwa kupata ithibati za kimataifa katika maeneo ya upembuzi wa barabara, utoaji wa alama na nyota kwenye barabara pamoja na lile la uchambuzi wa taarifa za barabara na mapendekezo ya hatua za kuchukua ili kuboresha kiwango cha usalama cha barabara.
Hivyo programu hii inaanza nchini baada ya hatua ya awali ya wataalamu wa ndani kujengewa uwezo na kupitia mafunzo ya takribani mwaka mmoja yaliyofanywa kwa njia mbalimbali na kisha wahusika kutahiniwa na kufaulu kulingana na vigezo ambavyo viliandaliwa na mashirika ya kimataifa yaliyopewa jukumu la kuandaa mafunzo na vigezo vya kupima ufaulu wa wataalamu walioshiriki mafunzo.
Ni nini TanRAP itakuwa inafanya?
Lengo namba 3 na 4 katika mkakati wa kuimarisha usalama barabarani duniani, linataka nchi wanachama wa UN kuhakikisha kuwa zinakuwa na barabara ambazo zina hadhi ya nyota 3 hadi 5 ifikapo mwaka 2030. Lengo hili linazigusa barabara ambazo zilishajengwa kabla ya malengo haya kutolewa na zile ambazo zitaendelea kujengwa.
Kupitia programu hii, wataalamu wetu watakuwa wakifanya upembuzi yakinifu kwa barabara zilizopo ikiwa ni pamoja na kuchukua picha za maeneo yanayofanyiwa kazi, kisha picha hizo zitatumika katika kutoa alama za viwango vya sehemu husika ya barabara, viwango ambavyo ndio vitaleta matokeo ambayo ndio hutumika kuipa barabara idadi ya nyota inazostahili kulingana na ubora au uduni wake.
Kiwango hicho cha alama na nyota ambazo barabara hupatiwa, ndio kitakachowaongoza wataalamu kufanya tathmini ya aina ya vitu hatarishi vilivyoko katika eneo husika na kutoa mapendekezo ya hatua ambazo serikali inaweza kuzichukua ili kuimarisha kiwango cha usalama wa barabara katika eneo husika kulingana na kundi la watumiaji barabara.
Hatua zinazoweza kupendekezwa zinaweza kutofautiana kulingana na kundi moja la watumia barabara hadi jingine kulingana na kiwango cha uwekezaji kinachotakiwa kufanyika na kulingana na kiwango cha faida ambayo itapatikana kwa kuwekeza sehemu hiyo (idadi ya watu wanaoweza kuokolewa dhidi ya ajali za barabarani) na hata kulingana na kiwango ambacho hatua iliyochukuliwa inaweza kuendelea kufanya kazi.
Mathalani, ufyekaji wa miti ambayo ni hatari kandokando ya barabara ili waendesha magari waweze kuona vizuri na kupunguza athari za ajali kwa magari yanayoacha njia, au uwekaji wa vitu vinavyoweza kupunguza mwendo au vibao vya ukomo wa mwendo, ni miongoni mwa hatua za gharama nafuu na zenye mchango mkubwa katika kupunguza athari za ajali kwa watumiaji wa barabara.
Hatua kama uwekaji wa taa za barabarani, utanuzi wa barabara na ujenzi wa madaraja ya watembea kwa miguu, ni hatua ambazo uwekezaji wake ni mkubwa lakini pia hudumu kwa muda mrefu zaidi. Hivyo programu hii inataka kuwe na uwekezaji ulio nafuu lakini wenye matokeo yenye tija.
Sambamba na hayo, wataalamu watakuwa na jukumu la kufanya tathmini za barabara ambazo hazijajengwa ambazo ziko katika hatua ya kubuni (design stage). Katika kutekeleza hili, wakandarasi wanaopewa kazi ya ujenzi wa barabara, watatakiwa wawe wanaandaa michoro ya namna ambayo watafanya ujenzi wa barabara husika kisha kuiwasilisha michoro hiyo kwa jopo la wataalamu watakaokuwa chini ya programu kwa ajili ya kuipitia. Ikiwa jopo hili halitaridhika na kiwango cha ubora wa barabara husika, watakuwa na nguvu ya kurudisha mchoro huo kwa mhusika akauandae upya.
Kina nani watahusika na TanRAP?
Hii ni programu ya Kitanzania ikimaanisha kuwa kila Mtanzania anatakiwa kujivunia, kubwa zaidi ni kujiweka tayari kuisaidia kutimiza majukumu yake ya kuzifanya barabara zetu kuwa salama. Kila Mtanzania anayo nafasi ya kushirikiana na programu kwa njia ya kutoa taarifa kuhusu hali ya barabara eneo alipo na hata mapendekezo ya nini kifanyike ili kuiboresha na wataalamu walio ndani ya programu watafanyia kazi taarifa na mapendekezo yake.
Kimuundo, programu itakuwa chini ya Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi, ikitekeleza majukumu yake kupitia wakala mbili za barabara zilizo chini ya wizara hiyo, Tanroads na Tarura, kwa kushirikiana pia na mashirika yaliyo na yasiyo ya kiserikali kama asasi ya Mabalozi wa Usalama Barabarani nchini (RSA Tanzania), TARA, Chuo cha Usafirishaji nchini (NIT), Bodi ya Mfuko wa Barabara (RFB).
Hitimisho
Ajali za barabarani, ni janga linaloathiri jamii, nchi na dunia kwa ujumla. Baadhi wakiwa wamepoteza ndugu, jamaa na marafiki huku wengi wakijikuta na mzigo wa kuhudumia ndugu na jamaa ambao wamepata majeraha na ulemavu wa kudumu kutokana na ajali za barabarani. Familia nyingi zimepoteza matumaini, ndoto zao na hata kusambaratika kutokana na ajali hizi.
Takwimu za Shirika la Afya Duniani (WHO) zinaonesha kuwa kwa mwaka ajali zinachukua uhai wa watu milioni 1.35 huku wengine milioni 20 hadi 50 wakiachwa na majeraha na ulemavu wa kudumu.