NMB Mbarali yakabidhi kompyuta shule ya Msingi Vikaye

BENKI ya NMB imekabidhi Kompyuta tano kwa shule ya msingi Vikaye iliyopo kata ya Igava Wilaya ya Mbarali mkoa wa Mbeya.
Akizungumza katika makabidhiano hayo, mwakilishi wa Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbarali, Athumani Kinza ameishukuru Benki hiyo na kutoa rai kwa walimu kuhakikisha kompyuta hizo zinatunzwa katika mazingira mazuri ili zidumu kwa sasa na siku za mbeleni.
“Tupo katika ulimwengu wa kidigitali kila kitu kinahitaji mfumo hivyo uwepo wa Kompyuta utarahisisha mno na kuchangia kasi ya maendeleo, niwapongeze Benki ya NMB kuwajali wananchi wa hali ya chini pia nitoe rai kwa walimu kutunza hizi rasilimali zilizotufikia kwa ajili ya Maendeleo ya Jamii yetu”, amesema Kinza.
Kwa upande wake Kaimu Afisa Elimu Msingi Wilaya ya Mbarali Elizabeth Mbwilo ameishukuru Benki ya NMB kwa kuwasaidia Kompyuta hizo kwani zitawasaidia walimu kuchakata matokeo kwa haraka na kutuma taarifa kwa wakati na pia kusaidia mambo mengine ya kitaaluma.
Meneja wa Benki ya NMB Mbarali, Lugano Mwampeta amesema ni sera ya Benki hiyo kurudisha kwa jamii kwa maeneo mbalimbali kama Elimu, Afya na masuala mengine ya kijamii.
Kwa upande wake Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Vikaye James Mkimbili ametoa shukrani kwa niaba ya walimu wenzake.



