NMB yafadhili Mfumo wa Diaspora kwa mil 100/-

BENKI ya NMB na Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, wamesaini Hati ya Makubaliano (MoU), ambapo NMB itafadhili Matengenezo ya Mfumo wa Utunzaji wa Taarifa za Diaspora Kidijiti (Diaspora Digital Hub System) kwa kiasi cha Sh mil 100.

Makubaliano hayo yamesainiwa Ofisi Ndogo za Wizara Dar es Salaam, ambako Mkurugenzi wa Idara ya Diaspora wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi James Bwana, alimwakilisha Katibu Mkuu wa wizara hiyo, Balozi Joseph Sokoine.

Akizungumza wakati wa hafla hiyo, Balozi Bwana aliishukuru NMB kwa kukubali kutoa ufadhili huo unaoenda kufanikisha matengenezo ya mfumo ambapo utakapokamilika utawatambua, kuwasajili na kutunza data za Diaspora wa Tanzania.

Balozi Bwana alibainisha kuwa, mfumo huo ambao utakamilika na kuanza kazi kabla ya Desemba mwaka huu, utakuwa chachu ya ushiriki wa Diaspora wa Kitanzania kidijiti katika shughuli mbalimbali za maendeleo, kibiashara, kiuchumi na kiuwekezaji nchini, licha ya umbali waliopo.

Kwa upande wake, Ofisa Mkuu wa Wateja Wakubwa na Serikali wa Benki ya NMB, Alfred Shao, aliyemwakilisha Ofisa Mtendaji Mkuu wa benki hiyo, Ruth Zaipuna, aliipongeza Wizara ya Mambo ya Nje kwa kuthamini mchango wa NMB na kuamua kuwashirikisha katika mchakato wa matengenezo ya mfumo huo.

Shao alisema kuwa makubaliano hayo ni muhimu kwa ustawi wa taifa na maendeleo ya Diaspora na kwamba Watanzania wanaoishi nje ya nchi ni muhimu sana katika kusukuma mbele gurudumu la maendeleo ya taifa na kwa kutambua hilo, NMB haikusita kufadhili matengenezo ya mfumo huo.

 

 

Habari Zifananazo

Back to top button