BENKI ya NMB imetwaa jumla ya tuzo 18 za ubora za kitaifa na kimataifa.
Jana benki hiyo ilitangaza tuzo 10 za kimataifa ilizotunukiwa hivi karibuni kwa kuwahudumia wateja wake na Watanzania kwa ujumla na kuwa kinara wa ujumuishaji wa kifedha nchini.
Mbili kati ya tuzo hizo mpya zimetolewa kwa ajili ya Ofisa Mtendaji Mkuu wa Benki hiyo, Ruth Zaipuna ambaye ilishanyakua nyingine tatu kwa kuiongoza NMB kuwa kinara wa huduma za kifedha na mfadhili wa kimkakati wa maendeleo ya taifa.
“Leo tunatangaza tuzo 18 za kitaifa na kimataifa zilizotolewa mwaka huu kwa Benki ya NMB kutambua ubora wa benki hii katika nyanja mbalimbali na katika huduma mbalimbali tunazotoa kwa wateja wetu, wadau wetu na Watanzania kwa ujumla,” alisema Zaipuna.
Zaipuna alisema kwenye tuzo 10 mpya za kimataifa majarida ya World Economic Magazine and the Global Brands Magazine ndiyo yaliyoitunuku NMB Tuzo ya Ofisa Mtendaji Mkuu Bora.
Machapisho hayo yanayoheshimika duniani pia yameipa tuzo za Benki Bora ya Wateja Binafsi na Benki Bora Tanzania kwa mwaka 2022 mtawalia.
Tuzo nyingine ambazo benki hiyo imetwaa hivi karibuni ni pamoja na Benki Bora ya Wateja Binafsi kutoka International Business Magazine na Ubunifu Bora katika Huduma za Kibenki kwa Wateja Binafsi na Benki Bora kwa Wateja Maalumu kutoka International Banker Awards.
Pia zipo tuzo za Benki Bora katika Kilimo Biashara iliyotolewa na Global Brands Magazine na ile ya Platinum Winner Sustainable Bond of the Year kutoka Global Small and Medium Enterprises (SMEs) Finance Forum Awards na Benki Bora ya Wateja Binafsi ya Global Banking & Finance Review.
Upande wa tuzo za kitaifa, Zaipuna aliziorodhesha tuzo tatu za Mamlaka ya Mapato (TRA) ambazo NMB ilizishinda wiki iliyopita ikiwemo ile ya mshindi wa jumla ya taasisi zinazolipa kodi kubwa na kwa kuzingatia misingi na kanuni bora za ulipaji kodi.
NMB pia ilitangazwa kama mshindi wa kwanza, mlipakodi mkubwa zaidi katika kundi la taasisi za kifedha nchini na mshindi wa tatu kama taasisi inayolipa kodi kubwa nchini Tanzania sekta zote.