Nongwa UWT zamchefua kigogo CCM

UMOJA Wanawake (UWT) wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Mkoa wa Katavi umeonywa kuhusu makundi ya uchaguzi wa mwaka 2020 na 2022 na kutakiwa kuachana na makundi kwani yanaduzama uhai wa umoja huo ndani ya CCM.

Onyo hilo limetolewa na Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Katavi, Iddy Kimanta, wakati akihutubia Baraza la UWT Mkoa katika ukumbi wa mikutano wa CCM Mpanda.

Kimanta ameweka wazi kuwa anafahamu juu ya uwepo wa makundi kwenye jumuiya hiyo, ambayo yanatokana na uchaguzi wa 2020 kwenye jumuiya hiyo katika kuwapata wabunge wanaotokana na UWT.

“Nataka niwaambieni zipo taarifa miongoni mwenu bado mnaendekeza makundi, chaguzi zilishaisha 2020/2022, wewe bado unanongwa uchaguzi umeshaisha, wewe bado unaendeleza nongwa tunaidhoofisha jumuiya, hatujengi upendo ndani ya jumuiya, ukiendelea kununa utazeeka bure,” amesema.

Amewasa wana UWT kuendelea kuwaunga mkono viongozi waliotokana na jumuiya hiyo kwa kuwa ndio wanaoshika uongozi kwa sasa bila kujali yaliyopita.

 

“Tupendane, tuaminiane na kuheshimiana tutajenga jumuiya imara, tukifanya hivyo hayo makundi makundi hayatakuepo unamkanyagia breki mwenzio ili iweje? Amehoji Kimanta.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa UWT Mkoa wa Katavi, Fortunata Kabeja amemshukuru Mwenyekiti wa CCM Katavi kwa kuwakumbusha  UWT kuvunja makundi na kwenda kuimarisha jumuiya hiyo.

Habari Zifananazo

Back to top button