Norway yaitabiria Tanzania mazuri afya ya uzazi

SERIKALI ya Norway imeitaja Tanzania kuwa miongoni mwa nchi itakayofikia maazimio ya kimataifa ya kuhakikisha haki ya upatikanaji wa huduma za afya ya uzazi kabla ya mwaka 2030.

Hatua hiyo imetokana na juhudi za serikali hususani utekelezaji wa agizo la Rais Samia Suluhu Hassan la kusimamia haki ya usawa kwa kuwarudisha shuleni wasichana waliokatisha masomo kwa sababu ya mimba.

Akizungumza na wadau mbalimbali wa afya ya uzazi Dar es Salaam jana, Waziri wa Maendeleo ya Kimataifa wa Norway, Anne Tvinnereim’s alisema wanaamini Tanzania itafika mbali zaidi katika kuhakikisha upatikanaji wa huduma za afya ya uzazi (SRH) ili kupunguza vifo vya mama na mtoto, mimba zisizotarajiwa na magonjwa ya zinaa.

Alisema kuwa ushirikiano baina ya Tanzania na wadau wa maendeleo sambamba na utayari wa kisiasa, kumesaidia kuleta mafanikio makubwa katika utekelezaji maazimio hayo.

“Tutaendelea kuiwezesha Tanzania kupitia Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia Idadi ya Watu Duniani (UNFPA) kuhakikisha tunaboresha afya ya uzazi hususani kwa vijana kwani wanahitaji taarifa zaidi za afya ya uzazi na namna ya kupanga maisha yao ili kufikia malengo,” alisema Tvinnereim’s.

Alieleza kuwa haki ya kufanya uamuzi kuhusu afya ya uzazi huwezesha watu kuishi maisha yao kwa uhuru na kwamba upatikanaji wa SRH ni moja ya maeneo ambayo yanaweza kuboresha nafasi za wanawake na wasichana kupata elimu kwa kuwasaidia wanawake kushiriki katika ajira na kuboresha mapato.

Mkurugenzi wa Huduma ya Afya ya Uzazi na Watoto kutoka Wizara ya Afya, Dk Ahmad Makuwani alisema kuwa serikali imekuwa ikifanya jitihada mbalimbali za kuimarisha afya ya uzazi kwani kuna ongezeko la watumiaji wa uzazi wa mpango na kutoa chanjo ya kujikinga na saratani kwa wasichana wenye umri chini ya miaka 18.

Alisema mikataba mingine wanayotekeleza ni pamoja na wa Maputo ambao pamoja na mambo mengine, unaelekeza kupunguza mimba na ndoa za utotoni. Pia wamefanikiwa kutoa chanjo asilimia 95 kwa watoto wenye umri chini ya miaka mitano kwa ajili ya kuwakinga na magonjwa.

Mwakilishi Mkazi wa UNFPA, Mark Schreiner alisema serikali ya Tanzania imefanikiwa katika kuongeza huduma za afya ya uzazi kwa mama, watoto na vijana balehe.

Pia alisema imeweka sera na malengo ya kuboresha huduma za afya ikiwemo ujenzi wa vituo vya afya na kuongeza uwekezaji katika sekta ya afya.

“Mwaka 2021 zaidi ya watoto milioni mbili walizaliwa sawa na asilimia 44 ya idadi ya watu wenye umri wa miaka 15. Uwekezaji mkubwa unahitajika kuboresha huduma za afya ya uzazi, uzazi wa mpango na kuzuia mimba za utotoni,” alieleza Schreiner.

Alisema mwaka 2021, Norway ilichangia Dola za Marekani milioni 25 ambazo zimesaidia kupunguza vifo 14,000 vya uzazi. Wasichana 68,000 wamelindwa dhidi ya ukeketaji.​​​​​​​

Habari Zifananazo

Back to top button