NSSF yajitosa mchango wa diaspora kukuza uchumi

MFUKO wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) umeunga mkono mchango mkubwa unaotolewa na Watanzania Wanaoishi Nje ya Nchi (Diaspora), katika kujenga uchumi wa taifa kwa kutoa Sh milioni 50 kufadhili matengenezo ya mfumo wa kidijiti wa utunzaji wa taarifa zao.

Hayo yalisemwa Ijumaa Dar es Salaam na Mkurugenzi wa Uthaminishaji, Takwimu na Usimamizi wa Hadhari wa NSSF, Ibrahim Maftah aliyemwakilisha Mkurugenzi Mkuu wa NSSF, Masha Mshomba, wakati wa hafla ya utiaji saini wa makubaliano na Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki kufadhili matengenezo ya mfumo huo.

Mkurugenzi wa Uthaminishaji, Takwimu na Usimamizi wa Hadhari wa NSSF, Ibrahim Maftah (kushoto) akimwakilisha Mkurugenzi Mkuu wa NSSF, Masha Mshomba (hayupo pichani) wakibadilishana hati jijini Dar es Salaam,  baada ya kutiliana saini makubaliano ya ufadhili wa matengenezo ya mfumo wa kidigitali wa kutunza taarifa za Diaspora.

 

“NSSF tunatambua na kuthamini mchango wa Diaspora katika kujenga uchumi wa taifa na wakati wote mfuko umekuwa moja ya wadau muhimu katika shughuli za matukio mbalimbali za Diaspora,” alisema Maftah.

Alisema ushiriki wa NSSF katika kufanikisha kuanzishwa kwa mfumo huo ni kuunga mkono Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan katika kuhakikisha Diaspora wanachangia kikamilifu maendeleo ya taifa.

Alisema mfumo huo utakapoanza utatoa utaratibu wa kazi mbalimbali za Diaspora kufanyika kwa mtandao jambo ambalo ni fursa kwa NSSF kutangaza fursa mbalimbali za miradi ya uwekezaji kama vile nyumba, viwanja, hoteli na shughuli nyingine zinazotolewa na mfuko.

Naye Mkurugenzi wa Idara ya Diaspora Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi James Bwana akizungumza kwa niaba ya Katibu Mkuu Balozi Joseph Sokoine, aliishukuru Bodi ya NSSF kwa kukubali kufadhili matengenezo ya mfumo huo, ambao utakapokamilika utawatambua, kuwasajili na kutunza taarifa za Diaspora wa Tanzania waliotapakaa duniani kote kupata huduma muhimu.

Balozi Bwana alisema mfumo huo utakuwa chachu ya ushiriki wa Diaspora wa Kitanzania kidijiti katika shughuli mbalimbali za maendeleo ikiwamo biashara, uchumi na uwekezaji licha ya umbali waliopo.

“Kwa niaba ya uongozi wa wizara na serikali kwa ujumla natoa shukrani za dhati kwa uongozi mzima wa NSSF wa kukubali kushirikiana nasi katika jambo hili muhimu kwa kutoa shilingi milioni 50,” alisema Balozi Bwana.

Alisema NSSF ni wadau muhimu wa kutoa huduma kwa Diaspora ambapo pamoja na huduma hizo kupitia dirisha la uwekezaji, wizara imekuwa na mazungumzo na NSSF ili kuangalia namna wanavyoweza kushirikiana zaidi katika eneo la uwekezaji kupitia uendelezaji wa viwanja vilivyopo katika Balozi za Tanzania nje ya nchi.

Habari Zifananazo

Subscribe
Notify of
guest
0 Comments
Inline Feedbacks
View all comments
Back to top button
0
Would love your thoughts, please comment.x
()
x