HISPANIA: MSHAMBULIAJI bora wa Michuano ya Mataifa Afrika (AFCON 2023), Emilio Nsue Lopez ametangaza kustaafu kuhudumu timu ya taifa baada ya kuitumikia kwa takribani miaka 10.
Nsue (34) anakumbukwa kama nahodha na mfungaji bora wa muda wote wa Equatorial Guinea akiwa na magoli 22 katika michezo 44 tangu kuanza kulitumukia taifa hilo lililo kitovuni mwa bara la Afrika, mnamo 2013.
Mzaliwa huyo wa Hispania amelisaidia taifa lake kufika hatua ya robo fainali za AFCON 2021 ikiwa ni mara ya pili katika taifa hilo tangu kufanya hivyo mwaka 2012.
Emilio anakipiga katika klabu ya Palma ya kwao Spain, akiwa na uraia pacha. Amecheza ngazi zote za vijana za Hispania hadi mwaka 2011 akiwa katika kikosi cha chini ya miaka 21.
Vyanzo mbalimbali vya habari vya michezo Afrika vinaeleza kuwa sababu ya Lopez kuchukua uamuzi huo ni baada ya AFCON 2023 Equatorial Guinea kutolewa katika raundi ya 16, walivuna (£860,000) pesa ambazo Nsue hakupata mgao wowote, akihusishwa na kwamba alikuwa mtovu wa nidhamu.
Hali iliyomfanya nahodha huyo kutumia (Instagram Live) kukituhumu chama cha soka cha taifa lao kuwa hakijamtendea haki yeye na wachezaji wenza, na kwamba licha ya kukosa huo mgao, pia wameshindwa hata kumpongeza kwa kutwaa kiatu cha ufungaji bora. Chama hicho kikaona kama kimedhalilishwa kikaamua tena kumfungia kucheza timu ya taifa.