‘Nusu ya umeme Uganda hautumiki’

WIZARA ya Nishati imesema karibu nusu ya umeme unaozalishwa nchini hapa hautumiki.

Akihutubia wanahabari Jumatano, Kaimu Kamishna Msaidizi anayesimamia ufanisi wa nishati na uhifadhi katika Wizara ya Nishati, David Birimumaaso alisema hali hiyo inatisha.

“Uwezo wetu wa matumizi bado uko chini sana, tuna uwezo wa kusambaza Megawati 1600, lakini mahitaji yetu ni Megawati 850 ambayo ni karibu nusu ya nishati tunayoweza kusambaza,” alisema Birimumaaso.

Alisema kuwa na umeme mwingi na kutoutumia kutokana na ama kutokuwepo au kuwapo miundombinu dhaifu ya gridi ya taifa, kunaigharimu nchi kwani kila kinachozalishwa kinapaswa kulipwa.

Katika ripoti yake ya 2021, Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali alisema serikali ililipa wastani wa Sh bilioni 87 kwa ajili ya umeme ambao haujatumika.

Katika hatua nyingine, Birimumaaso alidokeza kuwa, kati ya Julai 13 na 15, mwaka huu, Uganda itakuwa mwenyeji wa Maonesho ya Kimataifa ya Nishati na Umeme yatakayofanyika katika Viwanja vya UMA huko Lugogo yakishirikisha waoneshaji zaidi ya 100 kutoka Uganda, India, Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE) na Uingereza.

Kwa mujibu wa Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, Irene Bateebe, maonesho hayo chini ya kaulimbiu: ‘Ungana na Tasnia ya Nishati, Umeme Mbadala na Nishati ya Jua ya Uganda’ yatakuwa fursa kuimarisha mwingiliano wa kampuni za ndani na za kimataifa na kutoa jukwaa pana la kuwezesha ukuaji wa sekta ya nishati nchini.

“Jumuiya ya wafanyabiashara katika sekta hii wana nafasi ya kuonesha teknolojia na kujadili changamoto muhimu za kisera kama vile jinsi ya kuziba mapengo ya kiteknolojia na mifumo ya ubunifu ya kitaifa inayohitajika kukuza maendeleo ya kiteknolojia,” alisema.

Habari Zifananazo

2 Comments
Oldest
Newest Most Voted
Inline Feedbacks
View all comments
Back to top button