Nyanya bwerere sokoni Ilala

KWA mara ya kwanza Soko la Ilala lililopo Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam limevunja rekodi kwa magari kushusha matenga 4,000 ya nyanya kwa mara moja hali inayoonesha biashara ni nzuri.

Kwa kawaida magari yanayoingia kwenye soko hilo hushusha matenga 1,000 hadi 2,000 kwa siku.

Akizungumza na HabariLEO jana, Meneja wa soko hilo, Lusubilo Swiga alisema idadi hiyo ya matenga ni kubwa katika soko hilo ikilinganishwa na siku nyingine katika bidhaa hiyo pekee.

Swiga ambaye amekuwepo katika soko hilo kwa siku 14 sasa, alisema matenga hayo yameshushwa na magari 30 yaliyoingia juzi sokoni hapo.

“Kwa kuwa nyanya zimekuwa nyingi, hivi sasa tenga moja ni kati ya shilingi 17,000 na 20,000. Lakini wiki iliyopita nyanya hazikuwa nyingi hivyo ziliuzwa tenga kati ya shilingi 28,000 hadi 40,000,” alisema.

Alisema soko hilo linauza bidhaa mbalimbali si nyanya pekee bali limegawanyika katika maeneo sita. Alisema kuanzia alfajiri, barabara mbalimbali hutumika kama soko mpaka saa 5:00 asubuhi ambako hutumika kupita kwa kuwa wafanyabiashara wanakuwa wamepungua.

“Kuanzia jioni hasa hasa usiku saa 4:00 magari ya bidhaa mbalimbali yanaingia mpaka saa 12:00 alfajiri. Eneo lote la soko na barabara zinazozunguka soko linakuwa limejaa wafanyabiashara,” alisema.

Alitaja sehemu hizo sita kuwa ni barabara ya Utete ambako kunauzwa mbogamboga za aina zote, barabara ya Bukoba ambako ni lango la kuingiza nyanya pia ni barabara ya wafanyabiashara mbalimbali.

Barabara nyingine ni Nzasa ambako kunakuwapo bidhaa mbalimbali hususani karoti, hoho na bamia.

“Mtaa wa Morogoro kuna bidhaa mbalimbali kama nazi, Mtaa wa Pangani ni lango la kuingizia vitunguu pamoja na matango.”

Alitaja Mtaa wa Moshi kuwa ni lango la kuingizia matango, ndimu na machungwa.

“Hili ni soko ambalo lina maajabu barabara zinakuwa na shughuli za biashara majira ya alfajiri na baadaye kuanzia saa 5:00 asubuhi zinatumika kama barabara,” alisema.

Habari Zifananazo

Back to top button