Nyasaungu kufungua shule ya sekondari
WANAKIJIJI cha Nyasaungu, Kata ya Ifulifu, Musoma Vijijini, Mkoa wa Mara wamekutana na Mbunge wa Jimbo hilo, Profesa Sospeter Muhongo, kutathmini utekelezaji wa miradi ya maendeleo inayotekelezwa na kudhamiria kufungua sekondari yao, ifikapo Januari 2024.
Miradi iliyofanyiwa tathimini na kikao hicho ni ujenzi wa sekondari, ujenzi wa zahanati na uboreshaji wa miundombinu ya elimu kwenye Shule ya Msingi Nyasaungu.
Licha ya wanakijiji hicho kushukuru serikali kwa ujenzi wa sekondari ya kata hiyo, iliyo katika Kijiji cha Kabegi, imeelezwa kuwa Kijiji cha Nyasaungu ni muhimu kukijengea sekondari yake kwa sababu za kijiografia.
Michael Nyasugu, mkazi wa kijiji hicho amesema kipo pembezoni, mbali na vijiji vingine viwili vya kata hiyo, kina mito mingi na vichaka hali inayosababisha kutofikiwa kirahisi hususani nyakati za mvua.
Mkazi mwingine wa kijiji hicho, Sweetbetha Magesa amesema ujenzi wa sekondari yao utawaepusha watoto wao na adha nyingi, ikiwamo kutembea umbali mrefu kufata sekondari ya kata.
Aidha Halmashauri ya Musoma Vijijini imeombwa kuchangia ujenzi wa sekondari hiyo, inayotarajiwa kuwa mkombozi wa watoto wa wafugaji wa kijiji hicho na imekusudiwa kufunguliwa Januari mwakani.
Ujenzi huo umefikia hatua ya kukamilisha vyumba vitatu vya madarasa, choo chenye matundu sita na jengo la utawala.
Kikao hicho kimefikia uamuzi wa kuendelea na ujenzi huo katika hatua iliyofikiwa kuanzia Juni 10 Mwaka huu, huku Prof. Muhongo akiahidi kuendelea kuchangia saruji na mabati.