KAIMU Katibu Tawala Mkoa wa Mtwara Nanjiva Mzunda amewata waimbaji wa nyimbo za injili mkoani humu kuimba nyimbo ambazo zinatoa ujumbe wa kusisitiza maadili mema kwa jamii nchini.
Mzunda ametoa wito huo wakati akizundua albamu ya kwaya katika kanisa la TAG, Shangani Miracle Temple.
“Waimbaji wa injili wanafanya kazi nzuri ya Mungu lakini sasa tunaomba waendelee kuisistiza jamii yetu iishi na kuenzi maadili mema ya Kimungu, nyimbo wanazozitunga ziwe nyimbo za kutoa ujumbe wa watu kuishi katika maadili mema.” amesema.
Amesema kwa sasa jamii nyingi hasa vijana wanapita kwenye wimbi la mmomonyoko wa maadili ambapo vijana wengi wanapotea kwa kukosa maarifa ya kuwasaidia kuishi maisha ya yenye hofu ya Mungu na jamii kwa ujumla.
Mchungaji wa kanisa hilo George Mussa ameiomba serikali kuingiza somo la dini kwenye shule za chekechea, msingi na sekondari ili vijana wajifunze neno la Mungu tangu wakiwa wadogo kuwajengea msingi ya kuwa na hofu ya Mungu ili kuepuka kumomonyoka kwa maadili wanapokuwa wakubwa.
“Ushauri kwa serikali, jambo la msingi , waingize elimu ya dini ili kufundisha na kumjengea mtoto msingi wa neno la Mungu kuwa na hofu ya Mungu,” amesema
Amesema zamani waliruhusu masomo ya dini yafundishwe kwenye shule ili kusaidia watu kuwa na hofu ya Mungu.
“Ukiangalia waliosoma shule za seminari zamani wana maadili tofauti sana na wengi wao ni viongozi wazuri sana na ni kwa sababu walijengewa msingi mzuri wa maadili ya Kimungu.” amesema.