Nyota wa zamani Chelsea aokolewa Uturuki
MCHEZAJI wa zamani wa Chelsea, Christian Atsu ni miongoni mwa waliokolewa kwenye vifusi katika Jimbo la Hatay kufuatiwa ajali ya tetemeko la ardhi lililotokea nchini Uturuki na kuua watu 5000.
Taarifa za kuokolewa zimetolewa na meneja wa mchezaji huyo, Mustafa Özat wakati akizungumza na redio Radyo Gol ya Uturuki, kwa mujibu wa Shirika la Habari la BBC.
Mchezaji huyo raia wa Ghana anayecheza timu ya Hatayspor ya nchini humo alinasa kwenye vifusi baada ya matetemeko ya ardhi kukumba nchi za Uturuki na Syria Jana Februari 6 2023.
Makamu wa Rais wa Hatayspor, Mustafa Ozat amesema baada ya kiungo huyo kuokolewa, jitihada za kumtafuta mkurugenzi wa michezo wa klabu hiyo, Taner Savut ambaye amenasa kwenye kifusi zinaendelea.
Chama cha soka cha Ghana kiliandika kwenye Twitter: “Tumepokea habari chanya kwamba Christian Atsu amefanikiwa kuokolewa kutoka kwenye vifusi vya jengo lililoporomoka na anapokea matibabu. Tuendelee kumuombea .” Mchezaji mwingine Atsu Kerim Alici, rafiki wa karibu, pia ameokolewa.