Nyota ya Asas yang’ara CCM, upinzani

FEBRUARI 28, 2023, Joseph Mbilinyi, mbunge wa zamani wa Jimbo la Mbeya Mjini kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) katika mkutano mkubwa wa hadhara uliofanyika katika uwanja wa Mwembetogwa mjini Iringa alinukuliwa akimuomba Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa, Salim Asas ajiunge na chama chao.
Katika mkutano huo uliohutubiwa na Mwenyekiti wa Taifa wa chama hicho Freeman Mbowe, Mbilinyi maarufu kwa jina la Sugu alirudia kumtaja Asas akisema mwana CCM huyo ni mtu anayeguswa na kushughulikia matatizo ya wana Iringa kwa kasi ya ajabu.
Sugu alisema katika kushughulikia changamoto za wana Iringa, Asas ni mwana CCM asiyebagua hivyo atakuwa huru na kupata baraka zaidi endapo atajiunga na kambi ya Chadema ambayo moja ya misingi ya kuanzishwa kwake ni kuwasemea na kuwapigania watanzania wavuja jasho bila kujali itikadi zao.
“Tunamuomba Asas ajiunge na chama chetu ili kwa pamoja tushirikiane kushughulikia mateso ya wananchi, kuharakisha maendeleo ya wana Iringa na Taifa kwa ujumla,” Sugu alisema katika mkutano huo ambao Mbowe alitoa ufafanuzi wa kina kuhusu sera yao ya majimbo na msimamo wao kuhusu lugha ya kufundishia shuleni ambayo ni kingereza.
Maoni ya Sugu yanaungwa mkono na baadhi ya wanachama wa Chadema wa mjini Iringa waliosema sio jambo la ajabu kwa chama fulani cha siasa kushawishi au kumpokea mwanasiasa kutoka chama kingine.
“Ni jambo la busara kusifia juhudi za mwanasiasa wa chama kingine anayesababisha au kuchochea maendeleo hata kama ni mpinzani wako kisiasa. Na si jambo baya kuonesha nia ya namna mnavyoweza kushirikiana kwa pamoja au mkiwa katika timu moja kwa faida ya jamii,” anasema Phillip Msungu.
Naye Gerald Mbuma anasema; “Ni muhimu kuelewa kwamba suala la kuungwa mkono kwa kiongozi wa kisiasa kama Asas linaweza kutofautiana kulingana na maoni ya kisiasa, masuala ya sera na mambo mengine.
Hata hivyo Mbuma anasema zipo sababu kadhaa zinazoweza kuelezea kwanini baadhi ya wapinzani wa kisiasa wa Asas wanamuunga mkono na wanatamani ajiunge na vyama vyao.
Anazitaja sababu hizo kuwa ni pamoja na staili yake ya uongozi akisema baadhi ya wapinzani wa kisiasa wa Asas; “Tunavutiwa na staili yake ya uongozi na jinsi anavyoshughulikia masuala ya wananchi katika mkoa wake na hata Taifa kwa ujumla. Kila mtu angetamani kuwa na kiongozi kama huyu, kwanini tumchukie mtu wa maendeleo?”
Anasema Asas ni kiongozi mwenye uwezo pia wa kuhamasisha “matumaini” na ndio maana historia pana ya michango yake ya maendeleo na hata kwa watu binafsi haijawahi kujali itikadi za kisiasa.
“Asas ana uwezo wa kuvuta watu kutoka pande zote za kisiasa. Baadhi ya wapinzani tunamuona kama kiongozi anayeweza kufanya kazi na watu wenye mirengo yote na kushughulikia masuala ya wananachi yanayovuka mipaka ya itikadi za kisiasa na ndio maana tunatama awe mwanachama wa Chadema ili tufanye naye kazi,” anasema.
Naye Janet Samsoni anasema Asas ni kiongozi wa mabadiliko na mageuzi ya masuala yanayohusu changamoto za watu na ndio maana amechangia mabadiliko makubwa katika sekta za afya na malezi, elimu, uchumi, usalama barabarani, michezo na ameshughulikia masuala mengine yanayogusa jamii yanawavutia baadhi ya wapinzani.
“Ukienda kwenye sekta ya afya na elimu utaoneshwa majengo mbalimbali aliyojenga na vifaa vya kutolea huduma alivyochangia; kwenye uchumi tupia macho mitaji aliyotoa kwa machinga, mamalishe na babalishe, bodaboda, bajaji na wengineo mmoja mmoja ambao leo mfumo wa maisha yao umebadilika,” anasema.
Amegusia jinsi kampuni zao (Asas Group of Companies Ltd) zilivyotengeneza ajira katika sekta za kilimo na ufugaji, ujenzi na usafirishaji huku akitoa mfano wa kiwanda chao cha maziwa ya Asas kinavyochochea ufugaji na uzalishaji wa maziwa na ajira kwa vijana wengi wanaofanya biashara ya bidhaa hiyo mkoani Iringa na katika pembe tofauti za nchi.
Samsoni ameitaja pia michango ya Asas aliyotoa kufanikisha au kukamilisha miradi ya ujenzi au mipango ya serikali ikiwa ni pamoja na mchango wake katika kuimarisha usalama barabarani na kukuza sekta ya utalii mkoani Iringa.
Asas ni nani?
Asas, mwanachama mtiifu na mwaminifu wa CCM, ni mtanzania wa kwanza mwenye asili ya kiarabu kuwa mjumbe wa NEC kupitia mkoa wa Iringa. Alichaguliwa kushika wadhifa huo kwa mara ya kwanza Desemba 5, 2017 kwa kura 502 dhidi ya kura 74 alizopata Maselina Mkini na kura 15 alizopata Benard Mbugu.
Novemba 22, 2022 Asas alichaguliwa kwa mara ya pili kushika nafasi hiyo baada ya kupata kura 593 dhidi ya kura 34 alizopata Mugabe Kihongozi na kura 18 alizopata Dk Alex Sanga.
Kwa zaidi ya miaka 30, Asas amekuwa katika ulingo wa siasa za mapambano ya ushindi wa chama hicho, huku umaarufu wake ukishika kasi mara baada ya kuwa Kamanda wa Umoja wa Vijana wa CCM Mkoa wa Iringa na Mjumbe wa Mkutano Mkuu wa CCM Taifa akiwakilisha jimbo la Iringa Mjini.
“Akiwa na nafasi mbalimbali za uongozi ndani ya CCM mkoani Iringa, Asas amechangia sana kukiboresha, kukiimarisha na kukiinua chama huku akikipa sura ya kuvutia kwa wananchi. Kiongozi huyu amejenga rekodi kubwa ya mafanikio hasa baada ya kuwa Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa,” anasema Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Iringa, Daudi Yasin.
Yasin anasema wapinzani wake kisiasa wanaweza kujaribu kuyafikia mafanikio hayo na huenda wanaweza kufaulu lakini Asas tayari ana rekodi kubwa ya mambo mengi ambayo ameyafanya kwa CCM hivyo anastahili heshima ya kutukuka.
“Kwa masuala ya ndani ya chama yanayohitaji nguvu au michango ya wanachama wake, Asas ni mwanaCCM mwenye moyo wa hali ya juu wa kujitolea na katika hekaheka nyingi za kisiasa ndani ya mkoa wetu, anaweza kuwa ndiye MNEC aliyewezesha mafanikio kuliko mwingine yoyote,” anasema.
Sifa zinazotolewa na Yasin kwa kiongozi huyo, ndizo hizo au zaidi unazoweza kuzisikia kwa viongozi na wanachama wa ngazi mbalimbali katika wilaya zote za mkoa wa Iringa.
“Huyu ni mtu wa kipekee. Michango yake kwa chama hiki haiesebaki; ukienda kwa wanawake yumo, ukienda kwa vijana yumo, ukienda kwa wazee yumo na kwenye chama ndio usiseme. Sio rahisi kutaja kila alichotoa kwa chama hicho kwani mambo ni mengi sana,” anasema Katibu Mwenezi wa CCM, Mkoa wa Iringa Joseph Lyata.
Mwenyekiti wa CCM Manispaa ya Iringa Said Lubeya anasema moja kati ya mtihani mkubwa aliokuwa nao Asas mara baada ya kuchaguliwa kwa mara ya kwanza kuwa mjumbe wa NEC ambao hata hivyo aliuvuka salama, ni ahadi yake iliyohusu kurejesha jimbo la Iringa Mjini kwa chama hicho katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2020.
Kwa kipindi cha miaka 10, mwaka 2010 hadi 2020, jimbo hilo lilikuwa likiongozwa na Mchungaji Peter Msigwa wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema).
“Hakuna mwana CCM asiyejua mchango wa hali na mali uliotolewa na Asas kufanikisha uchaguzi wa ubunge na madiwani katika jimbo la Iringa Mjini mwaka 2020 na majimbo mengine mkoani Iringa,” anasema Rubeya.
Rubeya anasema mchango uliotolewa na MNEC huyo ulisaidia kukiunganisha chama hicho, wanachama na jumuiya zake zote hatua iliyorahisisha kampeni zao kwa wananchi na hatimaye kupata ushindi wa kishindo.
Katika uchaguzi huo, CCM kwa kupitia mgombea wake Dk Jesca Msambatavangu ilishinda kiti cha ubunge wa Iringa Mjini kwa tofauti ya zaidi ya kura 16,000 kwa kupata kura 36,034 na kumdondosha Mchungaji Msigwa aliyepata kura 19,331 huku kata zote 18 za udiwani zikienda CCM.
Aidha Asas aliahidi katika kipindi chote atakachokuwa mjumbe wa NEC kwamba atahakikisha anarudisha sifa ya mkoa wa Iringa ya kutoa kura nyingi kwa CCM katika chaguzi mbalimbali za viongozi wa serikali, ahadi ambayo utekelezaji wake inasubiriwa katika uchaguzi wa mwaka huu wa serikali za mitaa na Uchaguzi Mkuu wa 2025.
Asas anasema; “Bila wana CCM mimi si chochote, kwangu mimi wanachama wote ni sawa. Kwa kupitia nafasi hii ya uongozi sitaki majungu, fitina, umbea na taarifa zozote zinazoashiria kutugawa au kukigawa chama; uamuzi huu ni nguzo muhimu katika kukiwezesha chama chetu kuendelea kushinda,” anasema.
Pamoja na kuchangia kufanikisha ushindi wa jimbo la Iringa Mjini, Asas amekuwa akitoa michango ya hali na mali ili kufanikisha shughuli mbalimbali za kisiasa za chama hicho pamoja na maendeleo yake na ya wanachama wake.
“Moja ya kazi ya Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa ni kusimamamia utekelezaji wa Ilani ya CCM. Ilani hii inazungumza pia maendeleo ya watu na ndio maana nimekuja na kauli mbiu yangu ya Siasa na Uchumi. Kwahiyo ufadhili na michango ya kila mwenye nafasi umekuwa ukihitajika ili kufikia lengo hili,” Asas anasema.
Moja ya ahadi yake kubwa aliyotoa kwa CCM mkoa wa Iringa baada ya kuchaguliwa tena kuwa MNEC 2022, ni kuhakikisha kata zote 106 mkoani humo zinakuwa na ofisi ya chama, ahadi ambayo utekelezaji wake katika baadhi ya maeneo umeanza ikiwa ni pamoja na kutumia zaidi ya Sh Milioni 151 kati ya Sh Milioni 179 kukamilisha ujenzi wa ofisi ya chama hicho ya wilaya ya Kilolo.
Mwenyekiti wa CCM wiilaya ya Kilolo, John Kiteve na Mwenyekiti wa CCM Iringa Vijijini Costantino Kiwele wanasema kuna haja wakawaomba viongozi wa dini kwa pamoja wamfanyie Asas maombi maalumu ili aendelee kuwa na afya njema kwani mchango wake kwa maendeleo ya watu wa Iringa unazidi kuhitajika.
Februari 28, 2021, CCM Iringa Mjini ilimpa tuzo ya heshima kiongozi huyo inayolenga kutambua mchango wake katika kusaidia jamii na kukisaidia kwa kiasi kikubwa chama hicho kufikia malengo yake.
“Tumempa tuzo hiyo tukitambua mchango wake wa hali na mali kuwezesha shughuli mbalimbali za chama katika ngazi mbalimbali mkoani kwetu. Michango yake ni mingi kiasi kwamba sio rahisi kuweka rekodi zake kwa haraka,” anasema Mwenyekiti wa CCM Manispaa ya Iringa.